Friday, April 14, 2017

IMELETWA KWAKO NA: SIMULIZIMIX ENTERTAINMENT
MWANDISHI: ZUBERY RAZUUR MAVUGO.
                        UTANGULIZI.
     Katika maisha yake alidhani labda kutoka kwa mwanga hadi kuingia kwa giza huenda lazma mchana uonekane kisha usiku uingie nd’o giza lichukue hatamu yake, fikra zake zilimtuma kitamu kuwa kichungu huenda mpaka yangekuwa mabadiliko ya muda mrefu sana. Hakuwaza kama ni swala la kufumba na kufumbua kila kitu kina uwezo wa kubadilika ndani ya dunia hii.    Macho yaliendelea kumtoka kama mtu aliyechomwa na kitu chenye ncha kali kwenye tumbo lake. Ingawa dakika kadhaa nyuma tendo lile alikuwa akilichukulia kama filamu, lakini hivi sasa akili yake ilikuwa imeshamuhakikishia kuwa, hakuwa ndani ya ukumbi wa sanaa za maonesho bali alichokiona ndicho.

   Mikono iliyokuwa ikiutikisa mwili ambao haukuonesha hata hisia zozote, aliona aitoe na kuuacha ukiwa mpweke juu ya kitanda chake. Shuka zikiendelea kutumbua macho utadhani mlalaji ni zimwi, godoro likijilaani kimoyo moyo kwa nuksi ile. Kitanda nacho kikiendela kutoa dhihaka kimyakimya, Huku mwili usiyozisikia laana wala dhihaka zile ukiendelea kuwepo juu ya kitanda kile. 

  Hivi sasa hakuna alichokuwanacho ndani ya kichwa chake isipokuwa mawazo. Hakuona haja ya kushangaa kama ilivyokuwa awali, wala hakuiona haja ya kumuita mtu asiyeamka. Kwa muda ule ni kama alikuwa mfalme mwenye taji la machozi, yalimtoka katika macho yake kama maji yatokavyo kwenye maporomoko, huku yakisahau kama yeye ni mwanaume asiyependa kulia. 

Makamasi nayo hayakuwa mbali, yalijitutumua kutoka ndani ya madilisha mawili ya pua, iliyaweze kuichungulia dunia. Hakukubali jambo hilo. Kwa hali ya ajabu aliiagiza hewa kutoka nje iweze kupita ndani ya pua zake na kumsaidia kuyavuta makamasi yale. Kisha akautazama mwili ule kwa jicho la laana ya machozi.

     ‘’ Kwanini umeamua kwangu? Hivi unajifanya hujui ni mizigo mingapi ya matatizo ambayo inayakabiri maisha yangu, sasa mbona umeniongezea mzigo mwingine mkubwa zaidi, unadhani safari niliyoitamani, naweza ifikia? Ah! Sikujua. Mbona umenitenda hivi. Ina maana katika dunia nzima, umekosa sehemu nyingine ya kuutoa uhai wako, Mpaka nyumbani kwangu. 

  Nadhani unajua kila kitu baina yangu mimi na wewe. Kijana wa mtaani, nisiye hata na ramani ya mbele kuhusu maisha yangu, bado umeona haitoshi na kunishushia mzigo huu. Tazama, ni nani nitamweleza kuwa wewe umefariki kwa mipango ya Mungu nae akaniamini? Mioyo ya binadamu iliyojaza hasira, unadhani inaweza kunivumilia. Mbona lakini umenifanyia hivi?

   Sikujua, kwanini usingesema mapema kama ulikuwa unahitaji kuondoka katika hii dunia, kwanini lakini hukunieleza jambo hilo nami nikakupeleka walau hata nyumbani kwenu hivyohivyo ingawa sipatani na wazazi wako.

Nilijitahidi sana kujiweka mbali na wewe, nikaamua hadi kuanzisha pendo la hiyari kwa mwanamke asiye na mbele wala nyuma kama mimi, unajua hilo Sikujua. Lakini mbona uliamua kuja kwangu? Unadhani nitamjibu nini mpenzi wangu wa sasa, unafikiri hata nitachomjibu, bado atanielewa? Ah! Vipi kuhusu wazazi wako waliyo niahidi mabaya endapo nitaendelea kuwa na wewe. Tafadhali, amka Sikujua.. Amka japo nikupeleke kwenu kisha ufariki ukiwa huko.

   Eh! Mola wangu, kipi nilichokukosa mimi mja wako? Ama huku duniani hakukuwa sehemu yangu sahihi? Mbona nimekuwa mtu wa matatizo, kila kukicha afadhali ya jana? Ina maana katika dunia nzima hujawaona wengine wa kuwapatia matatizo haya mpaka mimi? Tafadhali, naomba niokoe katika hili. Wewe pekee nd’o tegemeo langu... Nakuomba, muamshe Sikujua walau kwa dakika moja ili niweze kumpeleka kwao.

   Wewe Sikujua... Sikujua.. Eh! Bado hunisikii tu? Ina maana umeridhia kuwaona walimwengu wakiniangamiza na kunipatia majina ya ajabu ajabu kisha kunifanya niiage hii dunia kwa aibu kubwa? 

Kama kweli unanipenda, mbona umeniletea matatizo? Uliniahidi kwamba, utanisaidia katika kila hatua, iweje leo unakuwa chanzo kikuu cha tatizo hili kubwa kuliko matatizo yote ndani ya hii dunia, kwa upande wangu? 

 Hakika upendo wangu kwako bado upo, lakini nakuomba, jirejeshe tena duniani, na uithibitishie dunia kuwa, mimi sina makosa. Unadhani walimwengu wataniacha hivi hivi? Unafikiri nani atahisi kuwa jambo hili ni mipango ya Mungu? Inuka japo mara moja, nakuahidi sintotoa siri kama wewe ni mfu uliyeamka... Bali nitafurahi na kuuamini upendo wako.

 Lakini mbona unakuwa hivyo? Hivi unadhani mimi nitaenda wapi? Unataka niende wapi mimi? Niende kwa mpenzi wangu wa sasa na kumweleza hili? Atanielewa kweli. Wewe sikujua, hebu fikiria hata kama ungekuwa wewe nd’o mimi na mimi nd’o wewe. Je, ungeenda wapi? Unataka niende kwa wazazi wako; wazazi ambao hawahitaji hata kuiona sura yangu. Kwanza nikifika tu, nadhani nitakuwa maerehemu niliye hai. 

Kama umegoma kuamka, basi naomba nijibu tu walau swali langu. Unataka mimi niende wapi ilikuyanusuru maisha yangu?’’  Ni kama alikuwa kichaa wakati huo, maneno yote hayo kwa nini yamtoke, tena kwa binti ampendae ambaye kwa wakati huo alikuwa amelala, bila pumzi. Uhai wake ukionesha dhahiri kutokuwepo katika dunia hii.

  Akili yake ya wakati ule, ilianza kumlazimisha asubiri jibu kutoka kwa mwili mfu wa binti yule kwa jina la Sikujua. Ingawa alikuwa na machungu ya kufiwa binti ampendaye, lakini machungu makubwa zaidi yalikuwa ni kufiwa binti ampendaye katika wakati ambao hakuna apendaye awenae kutokana na sifa zake tena amefariki akiwa kwake baada ya kwendakumuona kwa mujibu wa maneno yake kabla hajaiaga dunia.


    HAKIKA HII SI YAKUKOSA. FUATILIA HADITHI HII AMBAYO ITAKUFANYA UBAINI MAWAZO MENGI PEVU YALIYOMO NDANI YA KICHWA CHA MTUNZI WETU.  INAITWA NIENDE WAPI? MBONA KUNA SEHEMU NYINGI ZA KWENDA, KWANINI MTU HUYU AFIKIE KUULIZA AENDE WAPI? MAJIBU YOTE YAMO NDANI YA RIWAYA HII YA MAISHA.

KUSOMA SEHEMU YA KWAZA BOFYA HAPA NIENDE WAPI 01

UTAPATA HADITHI HII  NA NYINGINE NYINGI ZITAKAZOLETWA KWAKO NA SIMULIZI MIX ENTERTAINMENT KATIKA BLOG www.simulizimix.com FACEBOOK, INTAGRAM NA TWITTER @simulizimix .. YOUTUBE Simulizi Mix Entertainment WHATSAPP 0712505163 ... TUMA NENO GROUP KUONGEZWA KWENYE MAGRUP YA SIMULIZI MIX ENTERTAINMENT AU TUMA NENO INBOX KUPATA SIMULIZI ZETU INBOX YA SIMU YAKO., UKITUMA NENO INBOX HAKIKISHA UMASAVE NAMBA YETU KWENYE SIMU YAKO.

SHARING IS CARING, USISAHAU KUCOMENT LAKINI PIA KUSHARE HADITHI ZETU KWA UWAPENDAO NDUGU JAMAA NA MARAFIKI ILI UWEZE KUBURUDIKA NA KUELIMIKA PAMOJA NAO.

SIMULIZI MIX ENTERTAINMENT WE TOUCH YOUR FEELINGS


                        
Next
Newer Post
Previous
This is the last post.

0 comments:

Post a Comment