IMELETWA KWAKO NA:SIMULIZI MIX ENTERTAINMENT.
MWANDISHI: ZUBERY RAZUUR MAVUGO.
Ni kama dunia na vilivyomo, alivikosea. Si yeye wa kuwa ndani muda ule na kulalama kwa unyonge akijigeuza huku na kule, mwili wake haukuwa na uvumilivu hata kidogo, kuna wakati alikuwa akishangaa na kujiuliza maswali ya kipuuzi ati, Kwanini Mungu asimtazame mmoja kati ya wanae wawili na kumpatia matatizo hayo, hadi yeye? Mtafutaji mkuu wa familia. ingawa alijuawazi kuwa maradhi humpata yeyote yule hivyo anapaswa kukubaliananayo maana muumba ndiye ayaletaye, lakini yeye bado alijiona kama mwenye kuonewa haswa! Ni vipi awe wakitandani ilhali familia nzima inamtegemea?
Kila akitazama kulia mwaubavu wa kitanda chake, alimuona mkewe akimuhurumia, kushoto mwanae wa kiume mwenye umri wa miaka kumi na mitatu alionekana kiwa katika majonzi. Hata hivyo mtoto mwingine mdogo mwenye umri wa miaka saba mpaka nane, alionekana akiwa kakumbata mikono yake huku mwili wake kauegesha kwenye ukuta dhaifu wa nyumba. Bila shaka alikuwa mmoja kati ya wanafamilia na ni yeye anayekamilisha uwepo wa watoto wawili wa mwanaume yule ambaye kwa wakati huo alikwa kitandani bila kujitambua. Njaa iliendelea kumsumbua mtoto yule lakini hakuhitaji kujionesha.
Hata kama angelia, ni kama angekuwa akiyaongeza machungu ndani ya nyumba, alitambuawazi ndani hakukuwa na chochote kile, hata hivyo, angemweleza nani? Mama yake mwenye mawazo muda wote? Ama baba yake aliye kitandani akisumbuliwa na ugonjwa ambao hata haujulikani. Yote hayo, kaka yake aliyatazama.
Si kwamba vipimo havipo. Ni jambo dogo sana la kumchukuwa mgonjwa na kumpeleka hospitali lakini hata kama wangempeleka hospitali, hakuna ambacho angesaidiwa zaidi ya kutazamwa kama sanamu la maonyesho. Hawakuwa na chochote kile ambacho duniani kinatambulika kwa jina la pesa. Ati hospitali mtu anapimwa bure! Hiyo ni hadithi ya ukweli ndani ya vichwa vya wasiyo na matatizo lakini kwa waliyopatwa matatizo ya kuuguliwa, hutambuawazi nafasi ya pesa katika hospitali zenye huduma.
Hali ya bwana yule ilionekana kuzidi kuwa mbaya sana. Hivi sasa alikuwa akikoroma kama mtu aliye ndani ya usingizi mzito, wakati kiuhaisia alionekana akiyatumbua macho yake na kujigeuza kama ilivyokawaida yake. Maneno hayakumtoka mdomoni ila kwa dharura, na hata alipo bahatisha, alisema... ‘’ Ninakufaa mimi’’ hakika kauli ile ilimuhuzunisha sana mkewe, ingawa alijilazimisha kwa taabu kujibu. ‘’ Huwezi kufa mume wangu, bado tunakuhitaji.’’
Hata hivyo, mama baada ya kukumbuka kuwa, ni muda mfupi mumewe aliweza kupatiwa dawa aina ya Mwarobaini na kufanikisha kuinywa, lakini pia ndani ya muda huo, aliitapika. Hapo ikabidi atamani kumpatia nyingine kwakuwa ile haikumridhisha hata kidogo, zaidi aliishia kuiona hali ya mumewe inazidi kuwa mbaya.
‘’ Shukuru, hebu leta mwarubaini tujaribu kumnywesha labda atakunywa safari hii.’’ Mama alisema. Mtoto yule mkubwa akanyanyuka na kwenda hadi nje kisha akalifuata sufuria moja jeusi ambalo ndani yake lilikuwa na maji pamoja na majani. Akachukuwa kikombe kimoja ambacho hakikuwa kisafi, akamimina maji yaliyokuwemo ndani ya sufuria lile jeusi na kumpelekea mama yake.
Hapo mama yule akachukuwa kikombe na kuanza kumuomba mumewe afumbue mdomo iliaweze kunyweshwa dawa ile. Hata alivyofumbua mdomo na kunyweshwa dawa ile, ni kama hakuna ilichosaidia maana ilijaa ndani ya mashavu wala isipite katika koromeo. Mwisho wa siku dawa ile ilishindwa kuvumilia na kuanza kutafuta njia ya kutokea. Ah! Tayari ilipita na kuanza kumwagika kwenye godoro dhaifu, godoro ambalo lilikuwa limejawa na ramani za nchi mbalimbali ambazo bado hazijavumbuliwa katika dunia hii kutokana na kuchanganyikana kwa maji na uchafu juu yake.
Mama hakukata tamaa. Aliendelea kummiminia mume wake dawa ile huku akimsihi ajaribu kufungua koromeo lake, lakini wapi?
Yule mtoto mdogo ambaye muda wote alikuwa amesimama na kufanya kazi ya kuificha njaa aliyokuwanayo. Tayari tumbo lake lilianza kumuumbua. Minyoo ilinyonga na kutoa sauti zenye kuashiria njaa kali. Huku akipiga mbinja kila muda. hapo yule mtoto mkubwa akashindwa kuivumilia hali ile. Akanyanyuka na kuliendea shati moja mfano wa tambara deki, kisha akalivaa bila hata kuaga akaanza kuondoka.
‘’ Shukuru unaenda wapi? Huoni hali ya baba yako ilivyo?’’ Mama yake alisaili baada ya kumikia mwanae akiaga, ilhali muda ule alitakiwa awepo pale kama mtoto wa kiume mkubwa.
‘’ Naenda kutafuta pesa?’’ alisema.
‘’ Pesa?!’’ Mama alishangaa.
‘’ Ndiyo mama.’’ Mtoto kwa jina la Shukuru alisema tena bila hofu.
‘’ We Shukuru wewe, mdogo hivyo, pesa utatoa wapi? Unadhani pesa nizakuokota?’’ Mama alisaili.
‘’ Nitajua hukohuko, sasa wewe unaona bora niendelee kushuhudia baba akihangaika na magonjwa ambayo hata hayajapimwa, wacha nikatafute pesa mama.’’
‘’ Mh! Wewe Shukuru, hebu rudi hapa usije ukaenda kuiba vya watu na kuleta matatizo.’’
‘’ Mama, tangu juzi usiku unga ulipoisha, mpaka leo hakuna aliyekula chochote. Siwezi kuvumilia kukaa hapa na kuyashuhudia yote haya... Mi naenda kutafuta. Ona kama baba, tunampa mwarobaini unao tibu magonjwa ya tumbo, je tuna uhakika anaumwa magonjwa hayo? Akh!’’ Shukuru aliongea, akashindwa kuvumilia na kujikuta anatoa msonyo wa hasira. Kwakutambua maneno matupu hayavunji mfupa, hapo akaondoka zake nyumbani kwao Akimwacha mama yake akidondokwa na machozi wala asijue nini kitafuata, mdogo wake pia aliyatazama yote yale, ingawa alikuwa mdogo lakini moyo ulimuuma sana. Baba akiendelea kukoroma kitandani bila hata chaziada.
***
Mtoto mwenye hasira na maisha ya nyumbani kwake, alianza kutembea mtaani huku na kule akitafuta kazi. Ni muda mrefu ulipita tangu aanze kuhangaika huku na kule, alipita sehemu ambazo alitukanwa bila msaada. Kuna sehemu alihurumiwa lakini pia kuna sehemu walimwona chokoraa wa mtaani. Nani mwenye kuwa na imani na chokoraa?
Katika harakati zake alipita sehemu na kukutana na mgahawa. Akatazama kwa umakini na kugundua kuwa, mtu aliyekuwa akishughulika na kazi eneo lile alikuwa mama mmoja mwenye uso mpole na lugha nzuri mbele ya wateja aliyokuwanao. Alipoangaza zaidi alibaini rundo la vyombo, tabasamu likamtoka na hapohapo akaishikamanisha mikono yake kwa furaha kisha akaenda mbiombio hadi kwa mwanamke yule. Alipofika, alisuiri wateja ambao walikuwa na maongezi na mama yule wamalize, hata walipomaliza na yee akautumia muda huo.
‘’ Shikamoo mama.’’ Alisalimu.
‘’ Marahaba mwanangu, nikusaidie nini?’’ Mama yule alisema.
Mtoto yule ni kama alikuwa na hamu na swali kama lile kutoka kwa yule mama, ‘’ Samahani mama, naomba unisaidie walau kazi ya kukusaidia kuosha hututuvyombo.’’
Mama yule akabadilisha kauli na kuwa mkali kidogo. Lakini kijana yule machachari katika mdomo, alijitahidi kuyatumia maneno yake kiustadi,
Mama yule baada yakuona kijana ni mwingi wa maneno akasema, ‘’ Sina pesa ya kukulipa mwanangu... Wewe nenda tu, nisijekukufanysha kazi bila malipo.’’
‘’... Mama, mimi hata kama ukinipatia huo ukoko, nitafurahi sana... Nyumbani nimewaacha katika hali mbaya.’’
Muda si mwingi tayari kijana yule alikuwa ameshajinyakulia kazi. Mikono yake ilikuwa ikishughulika kuosha vyombo kama alivyohitaji. Naam, alifanya juhudi kwelikweli na ndani ya dakika arobaini na tano tayari vyombo vyote vilikuwa visafi. Akawekewa ukoko ndani ya mfuko mweusi na kuondoka.
Alitoka mbiombio kutoka pale hadi nyumbani kwao huku akimshukuru Mungu njia nzima.. Alipofika alimkuta mama yake akiendelea na kazi ya kumpepea baba yake kwa kanga iliaweze kupata hewa maana jasho lilikuwa likimtoka kwa wingi. Akamsogelea mama yake na kumweleza kuwa tayari ameleta chakula hivyo ale kwanza kisha ataendelea na kazi ile aliyokuwa akiifanya. Akamwita na mdogo wake, wakaungana kwa pamoja kwa ajili ya kukamatisha.
ITAENDELEA.
TUMEANZIA HAPA..
0 comments:
Post a Comment