Thursday, June 15, 2017


 IMELETWA KWAKO NA: SIMULIZI MIX ENTERTAINMENT         
 MWANDISHI: ZUBERY RAZUUR MAVUGO.
                       SEHEMU YA PILI

        ILIPOISHIA:
  Alitoka mbiombio kutoka pale hadi nyumbani kwao huku akimshukuru Mungu njia nzima.. Alipofika alimkuta mama yake akiendelea na kazi ya kumpepea baba yake kwa kanga iliaweze kupata hewa maana jasho lilikuwa likimtoka kwa wingi. Akamsogelea mama yake na kumweleza kuwa tayari ameleta chakula hivyo ale kwanza kisha ataendelea na kazi ile aliyokuwa akiifanya. Akamwita na mdogo wake, wakaungana kwa pamoja kwa ajili ya kukamatisha.

  ENDELEA.. Kaka mtu akachukuwa jukumu la kufuata maji na kuanza kuwanawisha. Alianza na mama yake akafuatia mdogo wake.
   
            ‘’ Maduhu, mbona huli?’’ Kaka mtu alihoji baada ya kumuona mdogo wake amekaa tu akitizama. Wakati guo mama yao ni kama alikuwa tonge la tatu.

             ‘’ Naomba uanze kwanza wewe kaka, kisha mimi nitafuata.’ Mtoto wa miaka saba aliyetambuliwa kwa jina la Maduhu alisema hivyo. Kaka yake akaonesha hali fulani ya kupatwa na upweke.

‘’ Sawa, basi naomba unilishe.’’ Kaka mtu alisema.

 Mdogo wake akaingiza mkono ndani ya mfuko ule mweusi ambao kwa ndani ndipo kulikuwa na chakula, akatoka na ukoko mzuri uliyojaa mafuta vyema huku kachumbari ikiupamb a kuachilia mbali mchuzi wa nyama pamoja na maharage vilivyokuwa juu yake. Akautwaa ukoko ule hadi mdomoni mwa kaka yake; kaka yakenaye kwa kutambua aliamua afumue mdomo wake na hata kukiacha kinywa chake wazi. Hapo mdogo wake akaweka chakula kile kinywani mwa kaka yake na kisha akamuacha aanze kutafuna.

Kaka mtu alipomaliza kutafuta mpaka kumezanae akachukuwa chakula ilikuanya kama kile alichofanya mdogo wake. Alipofikisha kinywani, mdogo wake hata hakufungua mdomo, alibaki akimtazama kwa macho ya huzuni tu.

   ‘’ Vipi, mbona huli wewe? Hebu achama basi.’’ Kaka yake alisema.

    ‘’ Nashukuru kwa nyie kula, lakini siwezi kula na chakula ikatulia kwa raha ilhali baba yangu tangu juzi sijamwona akila... Njaa niliyonayo mimi, baba yangu anayo mara nyingi maana hata kutapika ametapika sana tangu juzi.’’ Mtoto kwa jina la Maduhu aliamka maneno yale. Matamshi yake yakawa kama chungu ya chakula kile kwa mama na kaka yake. Wakabaki wameyabunda matonge mdomoni huku macho yao yakimtazama mtoto yule.

 Kaka mtu machozi yakamlenga lakini akayaomba uvumilivu, mama mtu yeye hakuwa hata na lakuongea.

 ‘’ Tafhadhali, naomba ule. Baba atakula tu, usiogope.’’ Kaka yake alisema.

  ‘’ Sitaki... Hata siwezi kula mimi.’’ Maduhu aliukabili msimamo wake.

   ‘’ Hata hivyo, leo asubuhi wakati wewe umelala, baba yako alikula... Na sasa hivi tunamlisha baada tu yakula, tunaomba ule, eti mwanangu?’’ Kwa kiasi fulani maneno ya mama yake yakawa yamemlainisha. Akakubali kulipoka tonge lililokuwa hewani ambalo kaka yake alikuwa akigombana na mdomo kuliomba liweze kuingia kwenye kinywa chake.

 Furaha ikaingia, lakini furaha ile hata haikudumu. Ilitoweka ghafla baada ya mgonjwa wao kubadili ratiba. Hali ya kukoroma kwake walikuwa wameshaizoea na kuichukulia kawaida kidogo, lakini hivi sasa hakuwa akikoroma tu, bali alikuwa akivikaza viungo vyote vya mwili wake na kuwa kama anashindana na kitu fulani hivi. Hali ile ilimpelekea jasho kuzidi kumtka kwa wingi, macho yakiwa nje huku kayatumbua, misulinayo haikuacha kumsimama haswahaswa.

  Kitendo kile kilipelekea walaji wa chakula wakisahau chakula chao na kumkimbilia mgonjwa wao. Wakaanza kumwita, mwenye kuita baba aliita mwenye kuita mume wangunaye pia aliita.  Mtoto wake mkubwa wa kiume mwenye umri wa miaka kumi na mitatu ajulikanaye kwa jina la Shukuru, hali ile alishindwa kuivumilia. Akatamani kuondoka nyumbani kwa ajili ya kwenda kwa mara nyingine mtaani kutafuta pesa ya kumpeleka mzazi wake kwenye matibabu.

  Akatoka mbiombio ndani mwao pasina hata kusikiliza kauli ya mama yake wala mdogo wake waliyokuwa wakimuomba. Mkononi alishikilia mkoba mdogo ambao aliuchukuwa ndani kwao; mkoba ule kwa ndani ulikuwa na vifaa vya kazi vya baba yake ambavyo ni; kiwi pamoja na blashi kadhaa huku sole fulani za viatu zikiwa ndani mule pamoja na uzi na sindano.

 Akaianza safari ya kuelekea mtaani, hata alipofika huko, alianza kufanyakazi ya kutazama miguu ya watu, yeyote mwenye suti alimvagaa.

   ‘’ Shikamoo Baba...’’ Wapo waliyomjibu, ‘’ We, chokoraa, sina mtoto mchafu na mjinga kama wewe.’’ Lakini hiyo haikuwa sababu ya yeye kutokwenda kwa mwingine na kumsalimia tena.

 Waliyoiitikia salamu yake aliwaongezea sentensi, ‘’ Nilikuwa naomba nikusaidie kung’arisha viatu vyako upesiupesi.’’ Wengine walimdhihaki, huku wengine wakamkubalia, akawang’arishia viatu vyao, lakini wengi kati yao, hawakumlipa chochote zaidi ya kumshukuru. Hata alipojaribu kuwauliza kwanini awamlipi, walimjibu, ‘’ Siumeomba utusaidie... Au ulidhani tunapesa za kuchezea.’’

 Kijana yule hakukata tamaa, akaendelea na safari yake, jua kali likizidi kumchoma kuliko kawaida, jasho jingi lilimtoka lakini hakujali. Hivi sasa alikuwa amechoka, ila kila akiikumbuka hali ya baba yake pamoja na mama yake huku akimfikiria mdogo wake kwa jina la Maduhu, hapo nguvu zake zinamuijia upya na kuanza tena kazi ile kwa mara nyingine.

 Alipita sehemu na kukutana na rundo la wanafunzi wengi wakitoka shuleni, wakampita huku wakijadili mambo kadha wa kadha kuhusiana na masomo. Aawatazama kwa jicho la wivu haswa! Kumbukumbu zikamrudisha nyuma kidogo.

  ***

‘’ Hivi wewe Shukuru pamoja na mdogo wako, mbona ninyi kila siku mnakuja hapa na sare zilizo chanika? Nguo zilizooza mnatuletea hapa kila siku... Hamuoni mnatuaibisha, hata wakija wageni shuleni ama wakaguzi kiukweli mnatia kinyaa. Ni muda mrefu tumewavumilia lakini bado wazazi wenu wanaonesha kutokuwanunulia ninyi nguo, najua ni kwakuwa hamuwaambii tu.’’

  ‘’ Hapana mwalimu, nyumbani hali ngumu. Baba ana dunduliza kutwa nzima hata pesa ya chakula ni kazi. Kiukweli kuna wakati hadi tunashindwa kumwambia jambo hili kutokana na kumuhurumia.’’ Shukuru alisema bila hofu.

  ‘’ Kwahiyo, una nijibu eh!’’

   ‘’Sivyo, ninakuelezea hali halisi.’’

    ‘’ Haya, na hii swala la nyie kuwa na daftari moja halafu mpo madarasa tofauti, linaetelezwa na nini? Kla siku mnakuja bila viatu... Sio dharau hizo?’’

  ‘’ Mwalimu, ni mara nyingi tumekuwa tukikweleza kuhusu jambo hili. Nyumbani kipato chetu cha chini mwalimu.’’

    ‘’ Ni baba gani mwenye malengo na wanae ambaye anakubali wasome bila hata mahitaji? Baba gani huyo, huo si upuuzi? Sasa nasema hivi, leo nawafukuza shule, chukuweni na hii barua, sitaki kuwaona tena... Mkirudi hadi muhakikishe mnakuja na sare za shule na si matambara deki haya, viatu vije, madaftari pia... Halafu msisahau pesa ya mlinzi na walimu wa kujitolea.’’

 ‘’ Lakini mwalimu... Tunao...’’

  ‘’ Potea hapa, sihitaji mjadala.’’

      ***

 Kumbukumbu za Shukuru ziliisha ghafla baada ya kumuona kijana mmoja nadhifu aliyeonekana kuvalia mavazi smati huku pembezoni mwa kijana huyo kukiwa na mwanamke aliyevalia mavazi ya ileo yaliyompendeza haswa. Wawili wale walionmekana kupendezana na umri wao ulikuwa ni kivuko cha miaka kumi na minane.

  Mapigo ya moyo wake yakamdunda, akili ikamtuma awakimbilia. Akafanya hivyo.

   ‘’ Shikamoo kaka’’  Wa kiume akaitika. ‘’ Shikamoo dada’’ na yule mwanamke akaitika pia.

 ‘’Samahani wakubwa zangu, nilikuwa naomba niwang’arishie kidogo tu, viatu vyenu iliangalau muweze kunipatia chochote, nyumbani kuna wagonjwa  hawaja..’’

  ‘’ Usijali dogo... Chukuwa hii hapa nadhani itakufaa.’’ Kijana yule ambaye alikuwa na msichana, hakuona haja ya kuyasikiliza maneno ya mtoto Shukuru. Alimpatia noti ya shilingi elfu tano kisha akaendelea na safari zake.

 Shukuru hakuyaamini macho yake, akauliza ‘’ Yote hii umenipa.’’ Akahakikishiwa. Hapo akatoka mbio kwa furaha kwelikweli huku akiamini lazma baba yake angepata vipimo. Akatoka mbiombio kuelekea nyumbani kwao.

           ***

     SAA MOJA NA NUSU KABLA.

Baada ya Shukuru kuondoka nyumbani kwao, huku nyuma hali ya baba yake ilizidi kuwa mbaya. Aliendelea kutokwa na jasho jingi akihangaika sana. Mke wake alijitahidi kumloanisha na maji yaliyokuwa kwenye kitambaa lakini wapi? Dakika kadhaa mbele, mzee yule aliganda wala asiendelee kujikurupua tena. Mkewe alihakiki na kugundua kuwa mumewe tayari ameshaiaga dunia.  Alilia sana, hata na mwanae mdogo alilia vilevile. Majonzi yaliiandama nyumba ile.

   ‘’ Mume wangu... Kwanini umeondoka na kutuacha katika hali hii? Unadhani tutaishi vipi sisi... Tazama, hakuna chochote ambachoumetuachia, rudi mume wangu usitufanyie hivyo...’’ Mke mtu aliendelea kulia na kuomboleza mulemule ndani. Mtoto wake kwa jina la Maduhu aliendelea kuyamwaga machozi yake vilevile huku akiushika mwili wa marehemu baba yake.

  Akili yake haikumtuma kuendelea kuwepo pale ilhali kaka yake mpendwa hayupo. Akatamani kumtafuta iliaweze kumjuza kuhusiana na taarifa ile kwa ajili ya kujua nini kitaendelea. Hapo akatoka nyumbani mbiombio kwa ajili ya kumtafuta kaka yake, akamuacha mama yake akiwa ndani pamoja na mwili wa marehemu.

  Maduhu, alimtafutasana kaka yake lakini asimpate. Hakuchoka, aliendelea hivyohivyo kumsaka huku akilia njia nzima.

     HIVI SASA.

 Akiwa katika harakati zake, furaha ikiwa imemjaa. Hakuangalia mbele hata kidogo alichojua ni kukimbia tu. Mpaka hivi sasa alikuwa ameshakatiza kona mbalimbali na muda mchache alitaraji kufika nyumbani kwao kutokana na mwendokasi aliyokuwanao. Alilifikia barabara kuu. Furaha yake ilimfanya azisahau sheria mbalimbali za barabara ikiwemo kuangalia kushoto na kulia.

  Aliupeleka mwili wake mzima mzima bila kujali.

Mungu wangu!

  Macho ya wapita njia pamoja na wafanya biashara waliyokuwa eneo lile walijikuta wakikumbwa na mshangao, wapo ambao mishangao yao iliambatana na kuwaita mama zao, lakini pia wapo waliyomuita Mungu wao. Kufumba na kufumbua mwili wa mtoto yule ulikuwa nyang’anyang’a huku akionekana kusumbuka kama kuku aliyekatwa kichwa. Lahaulah! Gari lililofanya kazi ile ya kumpitia lilibakiza vumbi tu wala lisijulikane lilipoelekea.

       ITAENDELEA.
Mh hivi kijana wetu shukuru ataweza kupona kweli? Na kama akipoteza Maisha na mzee wetu tayari hatunae katika dunia hii… Mama yule atakua ktk hali gani… Na vipi kijana wetu mdogo Maduhu ataweza kumlinda mama yake ili hali kaka yetu shukuru tutakua hatunae tena…. YANGU MACHO YENU MASIKIA TUKUTANE SEHEMU YA TATU KUJUA NINI KILIENDELEA KTK FAMILIA HII MASIKINI.


0 comments:

Post a Comment