IMELETWA KWAKO NA SIMULIZI MIX ENTERTAINMENT
MWANDISHI FRANK MASAI
SEHEMU YA NNE
ILIPOISHIA
ENDELEA
Mzee Pujini alikuwa kachomwa na kisu kirefu walichokuwa wanatumia kutesea watuhumiwa. Kisu hicho kiliingia kwenye jicho lake la kulia na kubaki kimenata hapohapo. Haikuwa hivyo pekee, bali pia shingo yake ilikuwa imechinjwa na alama ya mkato huo wa kisu, ilijitokeza na kuonesha koromeo lake.
Picha nyingine ni ya Beda, msaidizi wa Mzee Pujini. Shingoni, upande wa kushoto kulikuwa na tobo refu kama liliingizwa msumari wa nchi kumi hadi kumi na mbili. Katika paji la uso, pia kulikuwa na kisu kimenatia hapo. Ilikuwa inatisha kuangalia mara mbili.
Walipoanza kutazama huko na huko ndani ya FISSA, waligundua pia kuwa wafanyakazi wao saba walikuwa wameuawa kwa njia kama ambazo Beda na Mzee Pujini walivyokufa. Ni visu na mikasi ndivyo vilivyohusika kuwamaliza wafanyakazi hao.
Na kuna maiti ilikutwa haina mavazi. Ni wazi John Lobo alivaa mavazi ya maiti hiyo kabla hajaenda kwenye Jet P112, ndege ya kivita inayokimbia kuliko zote duniani (Nimeilezea kwenye simulizi ya Jina). Na kutoroka nayo.
"Nadhani alijikamatisha ili aje kuiba hii ndege." Malocha aliongea kwa huzuni baada ya ndege hiyo ghali kuibwa na Malocha. Ni ndege ambayo Afrika zipo mbili tu! Tanzania na Afrika Kusini.
Wakati anaongea hayo, yeye na wafanyakazi wengine, walikuwa wanatazama mkanda wa jinsi Lobo alivyokuwa anatoroka. Alionekana akivunja mkono wa kiti kwa kujitutumua, na baadaye akachomoa mkono wa kulia na kile kilichomshika mkono wakati yupo kwenye kiti, kilibaki kwenye mkono huo kikiwa na msumari mrefu uliokuwa umekamata kiti.
Mzee Pujini alipokuwa anataka kwenda kumshika Lobo, Lobo akawahi kisu kikali alichokirusha kiustadi na kwenda kumchoma kwenye jicho. Kabla ya Mzee yule hajakaa sawa wala kusikilizia yale maumivu, Lobo tayari alishadaka kisu kingine na kuruka sarakasi ya chinichini na kisha akamcharanga mzee yule shingo yake. Wakati huo Beda alikuwa akihangaika kufungua mlango lakini alishindwa kwa sababu ya kutetemeka kwa woga.
Wakati yupo hapo mlangoni, alisikia sauti ya Lobo ikimwambia Mzee Pujini kuwa alimuahidi kuwa atamuua wa kwanza. Beda akafanya kosa kubwa kugeuka na kuangalia tukio la mwenzake kufa, kwani kile kisu kilichopita shingoni kwa Mzee Pujini, ndicho kilichorushwa na kutua sawia kwenye paji lake la uso wake. Kabla hajadondoka, Lobo alimuwahi na kuingiza shingoni ule msumari uliokuwa umeshika kile kishikio cha kiti. Na hapohapo akauchomoa kwa fujo huku ukimuacha Beda akidondoka kama mzigo wa gunia la maharage.
Na baada ya picha ile mbaya ya mauaji ya Beda na Mzee Pujini, Lobo alionekana akienda kwenye mlango wa chumba kile na kubonyeza namba maalumu ambazo hufungulia mlango ule, na baada ya kubofya, mlango ukafunguka.
"Inaonekana anajua mengi sana ndani ya FISSA. Hadi namba za siri za kufungulia ule mlango." Malocha alionesha wazi mshangao wake wakati video ile ukiendelea kucheza.
Lobo akatoka nje ya chumba kile lakini baada ya dakika kama moja akarudi tena na kisha akachukua visu kadhaa kwenye ule mkoba maalumu wa kuhifadhia visu hivyo.
Hakuishia hapo, pia akaenda kwenye mkono wa kushoto wa Mzee Pujini na kumvua saa yake. Akaangalia kama inaenda sawa na ya ukutani, na aliporidhika, akaenda karibu na kamera iliyokuwa inachukua ule mkanda wanaouangalia wakina Malocha muda ule. Kisha akatoa ishara kwa kutembeza kidole kama ufanyavyo mshale wa saa, na mdomoni kwake alionekana akitaja maneno yasemakayo TICK TOCK, hiyo ni sauti ya mshale wa saa.
Baada ya kitendo hicho, uso wa Mubah ukabadilika na kujawa hofu zaidi kwani Lobo ujumbe ule alikuwa anamuelekezea yeye. Mubah akawa hana raha hata kidogo hasa baada ya kuona mauaji ya hatari anayoendelea kuyafanya Lobo.
Visu alivyovichukua mle 123F6 vilikuwa vinarushwa kiustadi na kuwakuta baadhi ya wafanyakazi ambapo mmojawapo alivuliwa nguo, na nguo hizo, Lobo akazieweka mwilini mwake kabla hajakwea ndege aina ya Jet P112 na kuiondoa kwa kasi toka kwenye shirika lile la siri la kipepelezi. ****
"Kuna kitu kinaendelea nchini kwetu kikubwa sana. Haiwezekani huyu Lobo akawa anajua ramani nzima ya jengo letu. Lazima kuna mtu toka humu au nje, anatoa siri za FISSA. Tunatakiwa kumjua na kumkamata mara moja." Malocha aliongea kwa hasira na kugonga meza moja kubwa ambayo ipo katika chumba maalumu cha mikutano ndani ya FISSA. Mkutano huo uliitishwa na Malocha baada ya kumaliza mkanda mzima aliokuwa anaufanya Lobo. Wafanyakazi wapatao ishirini, ambao wote ni wakuu katika idara fulani, waliitwa kujadili suala ambalo limetokea saa moja lililopita. Hakuna aliyejaribu kuchangia mjadala ule wakati Malocha akishindwa kuzuia hasira zake na kuanza kuiadhibu meza.
"Mkuu." Sauti moja iliita toka mlangoni. Ni yuleyule aliyekuja kuwapa taarifa kuwa Lobo katoroka. Na sasa alifungua mlango wa chumba kile kutoa taarifa nyingine. "Mr. President anakuhitaji kwenye simu." Jamaa alitoa taarifa na kufunga mlango ule na kwenda eneo husika kwa ajili ya kuendelea na kazi yake.Kwa kuwa simu ya mezani ilikuwa mlemle kwenye kile chumba, Malocha aliipokea na kuweka sauti ya juu ili kila mmoja asikie.
"Heshima yako mkuu." Malocha alisalimia baada ya kuipokea simu ile.
"Ni nzuri. Nasikia Lobo kaondoka na Jet P112." Sauti ya Rais iliitikia salamu na kuunganisha na swali.
"Ndio, lakini tutaipata tu Mkuu." Malocha akuongea kwa sauti ya kukata kata.
"Mnajua ndege hiyo wanaenda kufanyia kazi gani? Mbona mmefanya uzembe wa hali ya juu nyie washenzi" Rais alifoka kwa sauti kali. "Mnajua azimio la kuchukua ndege hiyo. Vipi wakienda kulipua nchi za watu huko!? Mnadhani Tanzania tutapona? Sasa nasema hivi, ndani ya wiki moja, ndege hiyo iwepo humo. Vinginevyo, watu mtakuwa hamna ajira na maisha yenu yataishia jela. Fanya nachokwambia Malocha." Rais akakata simu ile bila hata kusikiliza upande wa pili.
"Nadhani mmesikia. Sasa ni kazi tu." Malocha aliongea kwa unyonge huku akitembea kuelekea mlango wa kutokea, lakini kabla hajafanikiwa kutoka, yule mtoa taarifa akaingia tena na taarifa mpya.
"Prince Mubarak. Simu yako. Kuna mtu anashida na wewe." Baada ya taarifa hiyo, jamaa akaondoka na Mubah bila kuchelewa akaenda kwenye ileile simu na kufanya kama Malocha alivyofanya. Malocha akiwa anaelekea kutoka, alijikuta akisimama mlangoni baada ya kusikia sauti itokayo kwenye simu ile.
"Haloo Mubah. John Lobo hapa." Lobo alijitambulisha na kumfanya Malocha ageuke na kusimama wima akimwangalia Mubah. "Nipo kwako hapa. Na mchumba wako ananitibu majeraha mliyonipa huko. Oooh! Ana nywele laini sana, na zinanukia pia." Lobo aliongea kwa sauti ya chini huku pua zake zikisikika zikinusa kitu. Baada ya kunusa huko, sauti ya kike ya mtoto ilisikika ikiwa na furaha kwa kulitaja jina la Uncle Mubah.
"Usijali Mubah. Mama, Mchumba wako, dada na wajomba zako wapo salama. Huyu mjomba mwenye mwaka mmoja, ni mzuri sana Mubah. Fanya chaguzi sahihi, uza au nunua roho zao. Acha kazi yako au endelea na kazi yako, chagua ni lako Mubah. Yamebaki masaa ishirini. Tick Tock." Baada ya maneno hayo toka kwa Lobo, simu ikakatwa.
"Nifanye nini?" Swali la kwanza kuliuliza Mubah baada ya simu ile kukatwa. Alikuwa kama hajielewi pale alipouliza swali lile.
"Hiyo ndio nafasi pekee ya kumkamata huyu mbwa na kumfikisha mahakama za uharifu duniani." Malocha aliongea hayo huku akirudi katika sehemu yake aliyokuwapo mwanzo. "Tutaweka ulinzi wa kutosha katika nyumba yako, hakuna ambaye ataingia ndani wala kusogelea eneo lile. Snipers na walinzi wenye mbwa wawezao kunusa kilometa kadhaa, watazagaa kila eneo la mtaa wako. Hakuna atakayeumia siku hiyo. Usijali kuhusu hilo." Malocha aliongezea kuhusu mkakati wake na kumtoa hofu Mubah ambaye alikuwa akihisi kama anataka kufa.
"Hapana mkuu. Familia yangu ndio kila kitu kwangu. Kazi si kitu, naomba niache kazi hii mara moja kuikoa familia yangu. Huyu si mtu wa maskhara hata kidogo, ni hatari kama moto. Naomba niachane na hii kazi, naombeni sana." Mubarak alijikuta akiomba kuacha kazi sababu ya ule mkwara mzito.
"Utakuwa mjinga kama ukiacha kazi ka sababu ya mtu mmoja kama Lobo. Sikiliza Mubah, tunakuhakikisha usalama wa familia yako. Pale walipo, tunawatoa kisiri siri na kuwapeleka nyumba nyingine zenye usalama zaidi ya pale. Na hapo kwako ndipo tutaweka watu wenye sura kama za familia yako lakini wenye uwezo wa kupambana. Usiogope kuhusu maisha ya familia yako, watakuwa salama." Mubah akashusha pumzi ndefu kama ahueni ya maneno yale toka kwa Malocha, mkuu wake wa kazi.
"Asante mkuu." Mubah akashukuru na baada ya hapo, mkakati kabambe ukaanza kupangwa na wanamkutano ule. ****
"Lakini Mkuu, mkumbuke huyu Lobo si mtu wa kuchezea. Na mbaya zaidi tunahisi humu ndani kuna vibaraka wanaosaidiana naye. Huoni kama tutakuwa tunaiuza familia ya Mubah kwa bei rahisi kabisa." Lisa alikuwa ofisini kwa mkuu wake baada ya kutoka kwenye ule mkutano mfupi. Alienda katika ofisi ile ili kumpa ushauri kama huo Bwana Malocha.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment