IMELETWA KWAKO NA: SIMULIZIMIX ENTERTAINMENT
MWANDISHI: FRANK MASAI
SEHEMU YA KWANZA
SAA 2:50 ASUBUHI.
JIJINI DAR ES SALAAM, MAENEO YA SINZA AFRICA SANA.
Wanaonekana watu wawili wakiwa wanafukuzana huku
mfukuzaji akiwa kakamata bastola aina ya Baleta ikiwa imefungwa kiwambo cha
kuzuia sauti. Baadhi ya wananchi walikuwa wamesimama wima wakitizama uwezo wa
wale watu wawili kukimbia na kuruka baadhi ya magari ambayo yalikuwa yanakuja
mbele yao kwa kasi.
Licha ya wananchi hao kuwa makini na kufuatilia
mtanange ule kwa ukaribu zaidi, hawakujua ni nini sababu ya wanaume wale wa
shoka kukimbizana tena kimya kimya. Wakashindwa kumsaidia mfukuzaji kwa sababu
ugomvi hawakuujua. Kilichobaki kwa hawa wananchi ni kuendelea kujitazamia
ufanisi mzima wa wale watu.
"Kimenuka huko. Boya lazima atakuwa kafumwa
anakula mzigo wa watu pale Rombo Green View." Alisikika kijana mmoja
ambaye alionekana kama muhuni muhuni kwa jinsi alivyo na hata lugha
anayoitumia.
"Mmmh! Matepa. Rombo hadi huku Sana bado
hawajachoka tu kufukuzana? Halafu yule kaka wa nyuma ana bastola, we unadhani
ni kufumaniwa au yule wa mbele kakwapua cha watu kwenye gari. Maana huu wizi
kwenye magari umekuwa mkubwa sana." Dada mmoja ambaye naye alikuwa
kasimama kando ya barabara sawia na yule muhuni, alichangia maongezi kwa
kumpinga yule muhuni.
"Aah! Sister Angel, mwizi gani kapiga suti matata
kama ile. Suti ya laki saba ile. Angalia viatu na hata muonekano wa lile jembe.
Yule kafumwa tu anakula manzi wa mkuu, acha afundishwe adabu leo." Yule
muhuni aliyejulikana kwa jina moja la Matepa, alitetea pointi yake kwa vigezo
vichache ambavyo kila mmoja alikubaliana navyo kasoro Angel.
" Mmmh! Matepa, siku hizi, mwenye suti ndio mwizi
na mwenye muoneokano kama wako, ndio msamaria mwema. Hawa wezi wa siku hizi
wajinga sana lakini wana akili kama nchwa." Yule dada ambaye naye
alijulikana kwa jina moja la Angel, aliongea huku akianza kuondoka eneo lile
maana watu aliokuwa anawafatilia walishatitia kutoka eneo lile.
" Umeona Sister Angel eeeh, hawa wavaa suti ndio
washenzi sana. Lakini wakishavaa hivyo, wanaficha hata macho ya jeshi letu na
kufanya sisi wavaa majinzi au kaptula kwa tisheti, kuonekana ndio waharifu.
Hapo dada yangu umebonga." Matapa aliunga mkono kauli ya Angel ambaye
badala ya kuchangia chochote, alipunga mkono wake hewani na safari ya kupotea
eneo lile ikazidi kushika hatamu.
Wale majogoo wawili ambao walikuwa wanafukuzana,
hakuna ambaye alisimama na kusaliti amri kwa mwenzake. Kasi ilikuwa inaongezeka
kila dakika ambayo walikuwa wanakimbia kuifata barabara ya kwenda Makumbusho. Yule mwanaume wa mbele ambaye alikuwa kavaa
suti ya gharama, rangi ya kijivu. Chini viatu vya damu ya mzee, navyo
vikionekana ni vya gharama. Ndiye alikuwa kivutio cha macho ya watu wengi
waliokuwa wamesimama kando ya barabara. Aliweza kuruka baadhi ya magari kwa
sarakasi mwanana zilizochanganyika na mbwembwe nyingi kama nyimbo za kibantu.
Kuna muda aliruka sarakasi na kutua juu ya gari lililokuwa kasi, kisha
anajiachia kama mwenye kujitupa ndani ya maji kumbe anajitupa kwenye rami.
Anapofika chini ya rami hiyo, hujiviringa kiustadi na kisha huinuka haraka na
kuzidi 'kuchanja mbuga'. Manjonjo yote hayo, yalikuwa yanamkosesha raha yule wa
nyuma kwani shabaha zake kumrenga mtuhumiwa wake, zilikuwa haziendi ipasavyo.
"Mkuu, mpo wapi? Huyu mtu si mtu asee, muda si
mrefu tunampoteza." Yule jamaa wa nyuma alishika sikio lake ambapo kama
utamwangalia kwa makini zaidi, utagundua kuwa kavaa 'earphones' ambazo huvaa
wapelelezi au walinzi wakubwa duniani hasa katika kusaidia mawasiliano baina
yake na kundi husika.
Na hapo yule jamaa alikuwa anawasiliana na kundi lake
kuona kama atapata msaada juu ya mtu yule anayemfukuza.
"Okay. Basi mtegeni hapohapo maana naona wazi
anakuja eneo hilo." Sauti ya yule mkimbizaji ilisikika tena ikijibu
maelezo ya upande wa pili. Baada ya hapo, aliachia kisikizio kile na kuzidisha
mbio ili kumkaribia yule jamaa wa mbele yake.
Wakiwa katika kasi ya hatari, ghafla mbele ya yule jamaa wa mbele,
inatokea gari aina ya Noah na kupiga msele mkali ambao uliifanya ile gari
iseleleke tairi za nyuma lakini ni kama ilikuwa imepangwa itokee hivyo. Kwani
baada ya mseleleko huo, ule ubavu wa nyuma wa ile gari, ulimpiga kikumbo kikali
yule jamaa aliyekuwa anafukuzwa. Kikumbo hicho kikamfanya arushwe hatua kama
nane kwenda nyuma, na wakati huohuo, yule jamaa wa nyuma naye hakuwa mbali na
tukio lile.
Jamaa aliyepigwa kikumbo, akajikuta anarushwa bila
kutegemea. Na katika kujiokoa ili asitulie viungo vya mwili ambavyo ni rahisi
kuvunjika, akajikuta kasimama mbele ya jamaa mwenye mwili wa wastani na unaonekana
kukumbana na mazoezi ya kutosha kila kukicha. Tabasamu likajitokeza kwenye uso
wa kijana yule aliyerushiwa mtuhumiwa.
"Gotcha (Nimekupata)." Sauti ya ushindi
ilisikika kwa jamaa yule na kutaka kumkamata mtu aliyekuwa anamfukuza kwa
karibu saa moja na robo. Lakini kabla hajamkamata, alishtukia akipigwa ngumi
kali mbili za maeneo ya mabegani na kufanya bastola na pingu zake kudondoka.
Kabla hajakaa sawa, mtuhumiwa wake tayari alikuwa kamsogelea na kumgonga kochwa
kizito cha pua kilichomfanya yule mfukuzaji kuyumba kidogo na kusimama tena
lakini hapohapo mtuhumiwa wake alikuwa kisharuka angani kidogo na kumsindikiza
na teke la kifua ambapo safari hii alishindwa kijizua bali kukubali kwenda
chini na kusalimia rami iliyopo maeneo yale.
Ni kama jamaa yule hakukumbwa na gari kwa jinsi
alivyokuwa anajimudu kwenye kurusha mateke na kuruka sarakasi ambazo zilikuwa
chachu tosha katika kumuadabisha mpinzani wake ambaye alishindwa kujibu mapigo
na hivyo kugaa-gaa pale kwenye rami kama swala aliyechomwa upinde wenye sumu.
Yule kidume ambaye alikuwa amekwishamiliki mchezo mzima, sasa akawa anajiandaa
kummaliza mpinzani wake kwa pigo ambalo yule jamaa aliyekuwa anamfukuza
alipoliona, alikumbuka ni jinsi gani lilivyobeba uhai wa watu wengi akiwemo
Mkuu wa Upepelezi kanda ya kati, Mzee Ismail Ambazeki. Askari muadilifu kupata
kutokea katika nchi ya Tanzania.
Wakati Mzee Suma Ambazeki anapigwa pigo hilo, huyu
kijana ambaye anajiandaa kupokea pigo hilo, alikuwa askari mdogo sana kicheo.
Cheo chake kikamfanya awe dereva wa Mzee Suma au Ismail. Na siku wakati
mtuhumiwa wake anampa pigo bosi wake, yeye alikuwa ndani ya gari akitetemeka
hasa baada ya kuona mapigo 'konde' ya jamaa yule.
Akafumba macho yake ili asione jinsi lile pigo
litakavyokita mwilini wake. Yule jamaa ambaye alikuwa anafukuzwa, tayari
alishajitutumua na kujifua ipasavyo kwa ajili ya kumdondoshea pigo au tufani,
yule kijana wa watu. Akaruka juu huku sauti ya juu ya kikomando ikisikika
tayari kwa kumwingizia pigo takatifu yule mfukuzaji.
Ni kama wote wawili walikuwa ndotoni. Hapa
nawazungumzia yule aliyekuwa anapigwa na anayepiga. Mpigwaji, aliona kama
Malaika mwokovu kamtokea na kumsaidia, lakini mtuhumiwa wake alijiona kama
Malaika mtoa roho kamtembelea kwa wakati ule.
Akiwa juu huku akitoa sauti yake ya kikomandoo,
alijikuta akipigwa teke zito la ubavu lililokata hadi sauti yake hiyo mbaya.
Kabla hajaelewa wala kujiweka sawa kuangalia ni nini kilichompata, akapokea
teke lingine la kijizungusha (round kick) ambalo lilimkuta kidevuni na kuzidi
kumrudisha chini badala ya kumsimamisha.
Dhoruba ikazidi kumuandama yule mbabe wa mwanzo kwani safari hii
alijikuta akikaliwa kifuani na kuanza kupigwa ngumi mfululizo kana kwamba mwili
wake uligeuka kuwa begi la kupigia ngumi hizo.
Ndani ya dakika zisizozidi mbili, tayari yule mbabe alikuwa hoi huku uso
wake ukiwa umelowa damu zilizochagizwa na kupasuka usoni.
"Hey. Mubarak, fanya kazi yako." Ni sauti
iliyomuamuru yule aliyepewa kichapo na mtuhumiwa wake. Sauti ilienda sambamba
na kurushiwa pingu ambazo aliziokota baada ya mbabe mmoja kuzifanya zitoke
kwenye mikono ya mwanausalama Mubarak.
"Yes Madame (sawa mama)." Mubarak au Mubah
kama alivozoeleka kuitwa na wenzake, alinyanyuka na kuziweka pingu alizorushiwa
vema na kumwendea mtuhumiwa wake.
Japo yule mtuhumiwa alishasaliti amri, lakini Mubah ni
kama alikuwa hajui hilo. Akaanza kumshushia mateke mazito tumboni yule
mtuhumiwa.
"Hey Mubah, mfunge pingu, acha ujinga."
Sauti ileile ya kike ilimfokea na Mubarak hapohapo amri akaifuata kwa kumfunga
pingu yule mtuhumiwa wao na kumnyanyua, tayari kwa kumpeleka kwenye ile Noah
iliyompa kikumbo. Baada ya dakika moja, Mubah alikuwa tayari amekwishamaliza
kumfunga pingu mtuhumiwa wake na kumuingiza kwenye ile Noah. Ndani ya Noah
kulikuwa na wanaume wengine watatu, mmoja akiwa dereva na wengine wawili wakiwa
wanacheza na mitambo zikiwemo kompyuta ndani ya gari ile.
Yule mwanamke, alikaa upande wa kushoto wa siti ya
nyuma ya dereva, na Mubah akakaa upande wa kulia wakati huo mtuhumiwa wao
akikaa katikati yao.
" Lisa Lindsay. Mwanamke niliyekupenda kwa moyo
wangu wote. Upo mke wangu?" Sauti ya kukeresha ilimuuliza yule mwanamke
huku muulizaji mwenyewe akiwa kajiinamisha kichwa chake bila kumuangalia usoni
amuulizaye. "Kwa nini umeamua kufanya kazi kama hii? Umekosa kabisa hata kazi
ya kuuza vitumbua na sasa unajiweka katika kazi za utumwa kama hii? Kazi za
kuhatarisha maisha yako na ya uwapendao." Jamaa alizidi kuongea lakini
hakuna aliyemjibu.
"Ooh! Naona maongezi yangu hayawaingii vichwani
mwenu. Ngoja nijaribu maongezi haya." Safari mtuhumiwa alinyanyua uso wake
na kumuangalia Lisa. "Frank yupo wapi?" Swali likamtoka mtuhumiwa na
kumfanya Lisa amwangalie usoni kwa mshtuko. "Nimegusa penyewe hapo.
Anapenda kujiita Man'Sai. Mwanaume aliyetikisa dunia kwa kuiba "UKURASA WA
HAMSINI" (Hii ni hadithi nyingine ambayo inaanza pale riwaya ya JINA
itakapoishia). Mwanaume ambaye tulikuwa hatulali baada ya kugundua Lisa Lindsay
anatoka naye kimapenzi. Yupo wapi sasa hivi. Yale maneno matamu ya nakupenda na
porojo nyingi, vimeishia wapi? Hayupo tena nawe, kwisha habari yako." Yule
jamaa aliongea na kumalizia kwa cheko ndefu iliyokera kila mtu mle kwenye gari.
Lakini hakuna aliyethubutu kuongeza neno wala kufanya kitendo chochote cha
ajabu.
"Martina Gunner Bokwa. Jina la mtoto wako."
Yule mtuhumiwa akaongea maneno mengine yaliyovuta hisia za Lisa na kubaki mdomo
wazi. "Kwa nini ulimuita mtoto majina ambayo si yake?" Jamaa akazidi
kumshangaza Lisa kwa maneno ambayo yaligusa undani wa Lisa. Akiwa kafungwa
pingu na mikono yake ikiwa mbele, jamaa yule aliingiza mkono kwenye mfuko wa
koti ulio maeneo ya kifuani kwake na kutoa picha ambayo ilimuonesha mtoto wa
kike mwenye umri kati ya miaka miwili hadi mitatu. Kwa mshangao na kwa
kushtukiza, Lisa akampora ile picha yule jamaa huku uso wake ukijawa na
hamaniko la haja.
"Umetoa wapi hii picha we mpumbavu?" Lisa
alimuuliza yule jamaa huku akiwa tayari kamvamia na kumkaba shingoni. Ni Mubarak ndiye akiyemuondoa kwenye mwili wa
mtuhumiwa na kumpunguza hasira ambazo tayari zilikuwa zimemkamata kooni Lisa. Wakati
huo gari lao, lilikuwa linazidi kuacha maeneo kadhaa ya jiji la Dar es Salaam,
na kuna sehemu Noah ile ilisimama kwa muda mrefu sababu ya foleni kubwa
inayoendelea kutesa katikati ya jiji lile.
"Koho kohoo." Yule mtuhumiwa alijikohoza
baada ya roba ya Lisa huku akijitengeneza na kukaa sawa kwenye kiti cha gari
ile.
"Mubah. Hii ni picha ya Martina, nilimpiga
mwenyewe na nilikuwa nimeiweka kwenye mkoba wangu. Sasa huyu kaipataje na mkoba
huo nauficha kwani una vitu vingi vya siri." Lisa aliongea kwa sauti
iliyojaa machungu huku ikichagizwa na hali ya kutaka kulia.
"Navijua vitu vyote vya siri. Ukaamua kuolewa na
Gunner ili kuficha aibu. Hujui chochote kilicho nyuma ya ..... .." Jamaa
yule hakumaliza sentensi yake, tayari Mubah alikuwa kamtandika ngumi nzito ya
shavu hadi damu kiasi zikamrukia Lisa.
"Ooooh! Ni Prince Mubarak." Jamaa yule
aliongea baada ya kujifuta damu zilizokuwa zinamchuruzika. "Na swali.moja
tu kwako, na usipolijibu, nitakupa onyo tu." Jamaa alimtazama Mubah kabla
hajauliza swali lake. "Kwa nini umeamua kuweka dukani roho za
uwapendao?" Jamaa alimuuliza Mubah lakini badala ya Mubah kujibu, yeye
akachukua gundi aina ya 'sole tape' na kuizungusha mdomoni mwa mtuhumiwa yule
mwenye mdomo wa kero na kukereketa.
"Thats will help, I think. (Hiyo itasaidia
nadhani)" Lisa aliongea akikubaliana na kitendo kilichofanywa na Mubah.
ITAENDELEA
USIKOSE KUFATILIA SEHEMU YA PILI KUMJUA HUYU MTU NI NANI? KWA NINI AKAMATWE? AMEWEZAJE KUJUA SIRI ZA MWANAMKE HUYU? ANAMANISHA NINI KUMUULIZI MUBAH KUA KWA NINI KAWEKA ROHO ZA AWAPENDAO DUKANI....
KUSOMA SEHEMU YA PILI BOFYA HAPA DUKA LA ROHO 02
UTAPATA HADITHI HII NA NYINGINE NYINGI ZITAKAZOLETWA KWAKO NA SIMULIZI MIX ENTERTAINMENT KATIKA BLOG www.simulizimix.com FACEBOOK, INTAGRAM NA TWITTER @simulizimix .. YOUTUBE Simulizi Mix Entertainment WHATSAPP 0712505163 ... TUMA NENO GROUP KUONGEZWA KWENYE MAGRUP YA SIMULIZI MIX ENTERTAINMENT AU TUMA NENO INBOX KUPATA SIMULIZI ZETU INBOX YA SIMU YAKO., UKITUMA NENO INBOX HAKIKISHA UMASAVE NAMBA YETU KWENYE SIMU YAKO.
SHARING IS CARING, USISAHAU KUCOMENT KULIKE LAKINI PIA KUSHARE HADITHI ZETU KWAUWAPENDAO NDUGU JAMAA NA MARAFIKI ILI UWEZE KUBURUDIKA NA KUELIMIKA PAMOJA NAO.
SIMULIZI MIX ENTERTAINMENT WE TOUCH YOUR FEELINGS
0 comments:
Post a Comment