IMELETWA KWAKO NA SIMULIZI MIX ENTERTAINMENT
MWANDISHI FRANK MASAI
SEHEMU YA TANO
ILIPOISHIA
"Lakini Mkuu, mkumbuke huyu Lobo si mtu
wa kuchezea. Na mbaya zaidi tunahisi humu ndani kuna vibaraka wanaosaidiana
naye. Huoni kama tutakuwa tunaiuza familia ya Mubah kwa bei rahisi
kabisa." Lisa alikuwa ofisini kwa mkuu wake baada ya kutoka kwenye ule mkutano
mfupi. Alienda katika ofisi ile ili
kumpa ushauri kama huo Bwana Malocha.
ENDELEA
"Usijali Lisa. Hilo
pia nimelifikiria kwa kina na ndio maana pale mkutanoni, nimesema sehemu ambayo
tutaificha familia ya Mubah. Lakini kiukweli, sipo huko ambapo tutawapeleka.
Wataenda sehemu nyingine kabisa." Malocha alimtoa wasiwasi Lisa huku
akimpa vipande baadhi ambavyo walivifanya katika ule mkutano wao.
"Okay. Hapo sawa. Na
kingine tukumbuke kuwa yule pia ni Sniper, nadhani unakumbuka sana
alichokifanya nyuma. Tuwe makini zaidi tukiwa maeneo ya mtaa ule. Kila baada ya
kilometa mbili, kuwe na mlinzi juu na chini. Hiyo itasaidia sana."
"Usijali Lisa,
nimekuelewa na nitafanyia kazi hilo." Malocha alionesha shukurani zake kwa
Lisa ambaye baada ya kutoa ushauri huo, alitoka ofisini mle na kuelekea kwa
Mubah ambapo napo alikuwa anamtia moyo na kumueleza mikakati waliyoipanga.
****
Saa tatu asubuhi, yakiwa
yamebakia masaa kuna na matano ili ahadi aliyotoa Lobo itumie, gari moja nyeusi
ilisimama nje ya nyumba moja kubwa kiasi na baada ya sekunde kadhaa, alishuka
kijana Mubah na kuelekea katika nyumba hiyo.
Katika shirika la siri la
kipelelezi, sehemu ambayo Mubah anafanyia kazi, si ruhusa kwa mfanyakazi yeyote
kutoka ndani ya shirika hilo mida mibaya hasa usiku. Na ndio maana hata Mubah
alipopokea simu ya matatizo ya familia yake, hakuondoka hadi asubuhi hiyo
ambayo kwake ilikuwa kama mwaka kuifikia.
"Oooh! Mubah.
Ulikuwa wapi mwanangu." Mama yake Mubah ambaye alionekana wazi uzee umemchukua,
alimkimbilia kwa shida mwana wake kabla ya familia nzima nayo haijafanya hivyo.
"Usijali mama. Nipo
salama kabisa na nimekuja kwa ajili yenu." Mubah aliwapa moyo ndugu na
familia yake.
"Jana alikuja mtu
anaumwa, akamuomba wifi amsaidie kutibu majeraha. Sisi tulikuwa tunamwogopa,
ila akasema anafahamiana na wewe. Na hata baadae alipopiga simu, tukasikia
sauti yako. Sema akaenda kuongelea nje na baada ya kurudi alimuomba wifi afanye
alichokiomba mwanzo. Yaani amtibu yale majeraha." Dada wa Mubah alitoa
taarifa ambazo kwa Mubah alibaki akiwa kakodoa macho tu. Ye' alidhani Lobo
alikuja na kuitishia amani familia yake, na kumbe alikuja kwa njia za
kiutu. Akakuna kichwa chake kijana huyu
huku akishindwa afanye nini kwa wakati ule.
"Pia alipoanza
kuondoka aliacha ujumbe ule pale." Dada wa Mubah alisonta kidole chake
ukutani na kuonesha ujumbe aliouacha John Lobo.
Alisogea karibu maana ni
kama alikuwa hauoni japo ulikuwa na maandishi makubwa meusi kwenye karatasi
nyeupe iliyochomwa kwa kisu kwenye ukuta huo wa nyumba iishiyo familia ya
Mubah. Ujumbe ulisomeka "TICK TOCK" na kwa juu yake saa ya ukutani ya
Mubah ilikuwa ikienda taratibu kwa mlio huo wa tick tock. Mubah akahisi
kuchanganyikiwa.
"Anko. Anko yule
mwingine kanipa hii hapa na ......" Kabla ya yule mtoto wa dada yake,
mtoto mwenye umri wa miaka saba hadi nane hajamaliza kauli yake, Mubah tayari
alimpora kile kitu ambacho alikuwa kakishika yule mjomba wake. Kilikuwa ni
kibanio kizuri cha nywele kilichonakishiwa na madini ghali ya dhahabu. Mjomba yule wa Mubah alikuwa anafuraha kila
alipokiangalia, lakini kitendo cha Mubah kumpora na kuanza kukikanyaga kanyaga,
kikafanya yule mtoto asiseme kitu kingine ambacho kapewa. Alikuwa kavaa pambo
zuri katika nkono wake, pambo hilo pia alipewa na John Lobo.
Mjomba wa Mubah
akakimbilia chumbani kwa mama yake na huko safari ya kilio ikachukua nafasi
yake. Aliona kama Mjomba wake kamkatili sana nafsi yake kwa kile kitendo.
Watoto bwana.
"Naomba mjiandae.
Leo saa mbili usiku tutaondoka katika nyumba hii. Tupo katika hatari kubwa
sana. Na ninaomba, jirani au mtu yeyote asijue ni wapi au muda gani tunatatoka
hapa. Tupo katika hatari." Mubah akiongea huku uso wake ukiwa na mashaka
makubwa sana hali iliyofanya familia yake kuzingatia maneno yake. Familia nzima
ilimjua Mubah kama askari wa Tanzania. Hivyo aliposema maneno hayo, kila mmoja
akaamini kuna kitu cha hatari hasa pale walipovuta sura ya yule mtu aliyekuja
usiku wa jana yake.
"Usiwe na wasiwasi
dear. Mambo yote tutayafata." Ilikuwa ni sauti ya Zakia Bin Ashib ikimfariji
mpenzi wake walipokuwa chumbani wakipanga baadhi ya vitu vyao kwa ajili ya
kuondoka usiku huo. Maneno hayo ya faraja, yalikuja pale Mubah alipomueleza
mkasa mzima uliomsibu siku ya jana yake tangu alipoanza kukimbizana na Lobo
hadi unyama alioufanya kule FISSA. Ndani
ya maongezi hayo, Mubah hakuthubutu kuongea kuhusu ndege iliyoibiwa au mahali
ambapo anafanyia kazi.
Zakia Bin Ashib, kila
kukicha alikuwa anamuomba mpenzi wake amueleze ni wapi anafanyia kazi zake,
lakini Mubah alikuwa anakataa kusema ukweli kwa sababu ya masharti ya shirika
lake.
****
Saa mbili usiku, kwa
kutumia handaki dogo lililo katika sebule la Mubah, familia yote iliingia huko
na kutokezea katika zizi la ng'ombe, kilometa kadhaa kutoka kwenye nyumba ya
Mubah. Hakuna aliyewahi kufikiria kuwa nyumba ya Mubah inahandaki hilo. Awe
mama yake au mchumba wake. Hivyo kitendo cha wao kuingizwa huko na kutokea
kwenye zizi la ng'ombe, likawa ni hadithi nyingine ya kusisimua ambayo Mubah
alipaswa kuilezea.
Baada ya kuibukia zizini
huko, gari moja ya kimarekani, ilifunguka milango yake na watu idadi ya familia
ya Mubah, walijitojeza. Macho ya familia ya Mubah ikazidi kushangazwa hasa wale
watu wanavofanana nao.
Watu wale, wakaipita
familia ya Mubah na kuingia katika handaki lile lile ambalo walitokea familia
ile. Familia ya Mubah, ikapanda na gari ile na safari ya kwenda pasipojulikana
ikachukua nafasi yake wakati huo Mubah alirudi nyumbani kwake na kuanza kutoa
maelezo yote yanayofaa.
Huko nje ulinzi ulikuwa
ni wa hali juu kuliko hata ule ambao huwekwa rais wa nchi fulani akifika
nchini. Wapelelezi walikuwa wakipita katika mtaa huo kama wapita njia na hakuna
ambaye alihisi kuwa wale ni wapelelezi. Wadunguaji (Snipers) walikuwa kila
upande katika eneo lile wakiwa na bunduki zao maalumu kwa ajili ya kudungulia
mtuhumiwa wao.
Huko FISSA, Lisa na
Malocha walikuwa wanawapa taarifa watu wao wa kazi hasa kwa picha ambazo
zilikuwa zinatumwa kwa satellite. Kila mtu tofauti waliyemtilia mashaka
akipita, FISSA walitoa taarifa kwa kikosi kazi chao kilichoongozwa na Mubah.
Hatimaye zikabaki dakika
kumi na tano za ahadi ya Lobo kutimia. Kila mtu moyo ukawa unamdunda kwa sababu
mtu wanayemtega si mtu mdogo. Ni eidha wamkamate hai au akiwa maiti. Lakini
je!? Uhakika wa kumkamata upo? Swali hilo ndio likafanya mioyo ya wachapakazi
wale kutokuwa na amani.
Mbwa wasiojua kubweka
bali kufanya kazi yao, nao wakawa wananusa kila sehemu walipopitishwa. Ulinzi
ulikuwa mkubwa haswa. Mtaa mzima anaoishi Mubah ulitapakaa ulinzi wa hali ya juu.
Zikiwa zimebaki dakika
saba za jambo alilopanga Lobo kutimia, simu ya Mubah ilianza kuita mbele ya
familia yake ile mpya. Namba ya mpigaji haikuonekana bali kuandika neno
'private call'. Mubah akawapa ishara
wale watu waanze kutimiza maadhimio waliyoyapanga.
Bila kuchelewa, meza
kubwa ya mle ndani ikafunuliwa na watu wote wakasogea pale mezani na kutazama
mahanjumati na mapochopocho kadhalika yaliyoandaliwa kiufundi na wafanyakazi wa
FISSA. Wakaanza kusali kwa sauti na ndipo Mubah akasogea pembeni kidogo na
kupokea simu ile.
"Hallow." Mubah
akaita baada ya kupokea simu.
"Heloo Mubah.
Niambie kamanda wangu." Sauti ya Lobo iliitikia upande wa pili na wakati
huo wale waliondaliwa kupambana na Lobo, walizidi kupamba moto kuombea chakula.
"Stupid Lobo."
Mubah akatoa tusi dogo.
"Mmmh! Siku hizi
mmeokoka Mubah. Mnasalia chakula kwa kukemea kwa jina la Yesu. Muislamu halisi
kama wewe!?" Lobo aliongea na kucheka sana na hapohapo wale washirika wa
Mubah walikatisha sala zao na kugundua kuwa walikuwa wanasali Kikristo wakati
familia ya Mubah ni Waislam. Japo Mubah alikuwa mbali nao, lakini wao pia
waliyasikia yale maongezi kwa kutumia vinasa sauti vilivyokuwa masikioni mwao
kama vishikizo. "Okay. Ondoa shaka Kamanda, siwezi kuingilia maisha
uliyoyaanza na familia yako ya kujibambika.
Nipo hapa kukukumbusha
kuwa zimebaki dakika tano na sekunde kadhaa ili ahadi yetu itimie. Huku
ulipoileta familia yako, nadhani panafaa sana kufanya kazi yetu. Na kingine,
kabla sijafanya chochote kwa huo ugeni ulioniletea kwako, naomba utoke nje na
ushuhudie mara ya mwisho mtaa wako. Toka, waweza kuniona navyoua vimbwa
vyenu." Lobo akamaliza kuongea lakini hakukuta simu. Mubah akawa kama kachanganyikiwa, akatoka nje
kasi na kuanza kuangaza huko na huko, akasogea hadi barabarani na kuzidi
kushangaa. Aliweza kuwaona wapelelezi wenzake na wakamuoneshea ishara ya
kumuuliza vipi? Lakini Mubah ni kama alikuwa kapandwa na kichaa na wakati huo
simu ikiwa sikioni kwake.
"Ha ha hahahaaa.
Mubah, Mubah, Mubah. Bado dakika mbili. Embu ongea kwanza na mjomba wako."
Lobo alisikika tena kwenye simu ile aliyoipiga.
"Ankoo tusaidie
tumefungwa kamba na jambaziii." Mjomba wa Mubah alipiga kelele kwa nguvu
na kumfanya Mubah ahisi kama anamabawa lakini hawezi kupaa kwenda kutoa msaada.
Akabaki katikati ya barabara na simu ikiwa sikioni kwake.
"Ooh! Nasikia pia
ulikanyaga-kanyaga kibanio changu. Zawadi nzuri kabisa kutoka Malyasia.
Nimemletea anko wako lakini umekiharibu. Ila hamna tatizo, bali tatizo
litakuwepo kama pale chini ulipokikanyagia kitabaki palepale. Najua kipo
palepale, embu nenda kakiangalie." Mubah akatoka mbio tena na kuingia tena
nyumbani kwake. Hapo alichokishuhudia, hakika hakuwahi kukifikiria katika
kichwa chake. Miili minne, akiwepo na
yule mtoto ambaye walimfanya kama mjomba wa Muba ilikuwa imelala kifudifudi
kwenye viti walivyokalia huku moshi mdogo ukiwatoka midomoni mwao. Nyuso zao
zilijikunyata na kuwa kama za wazee wa miaka mia moja. Damu ilikaushwa katika
miili yao kwa kutumia sumu kali inayosambaa kwa hewa.
Mubah alipoangalia sehemu
alipokanyagia kile kibanio, alikuta kuna majivu machache ambayo yalitokana na
kile kibanio kuungua.
USIKOSE SEHEMU YA SITA.. PAPA HAPA SIMULIZI MIX ENTERTAINMENT
0 comments:
Post a Comment