Thursday, June 22, 2017

IMELETWA KWAKO NA SIMULIZI MIX ENTERTAINMENT
MWANDISHI ZUBERY RAZUUR MAVUGO.

SEHEMU YA TANO.

ILIPOISHIA:
   ‘’Hospitali ni sehemu ya wagonjwa tu na si watu wazima. Hata hivyo, unaonekana kijana mdogo sana ambaye bado matatizo hujayazoea. Ni watoto wengi na hata wakubwa wenye matatizo tena zaidi yako wanakuja hapa na kuomba kama unavyoomba wewe, lakini tunashindwa jinsi ya kuwasaidia. Labda nikusaidie kwa kusema. Mwanaume wa kweli huwa hayaogopi matatizo, nenda hukohuko yalipo ili uweze kukuwa ki akili na kutengemaa kifikra, sisi pia tumepitia magumu, na kupitia hayo tumejifunza na kuwa hapa tulipo leo.’’

  ENDELEA... Hayo nd’o yalikuwa majibu ya Daktari; majibu ambayokwa kiasi fulani yaliweza kummaliza kabisa nguvu mtoto yule.

Mtoto yule mchafu kwa jina la Maduhu alibaki amechoka huku pumzi ya kukata tamaa ikimtoka. Akakosa jinsi. Akaona eneo lile kwake si sahihi. Taratibu akaichukuwa miguu yake na kuanza safari ya kuondoka huku mikono yake kaiweka juu ya kichwa chake kuashiria jinsi ambavyo mambo yamemzidi.

 Wakati akiwa njiani, kichwa chake kilikuwa na wingi wa mawazo haswa. Hakupanda daladala ingawa zilikuwepo nyingi sana jijini pale. Aliiamini miguu yake hivyo alikuwa akitembea tu. Kuna wakati alijikuta akikoswakoswa mpaka na magari kutokana na wingi wa mawazo.

Kwanini watu hawanahuruma? Ina maana huyo daktari hana watoto? Mbona ananifanyia hivyo mimi? Kipi ambacho nimemkosea hadi kunifaradhishia matatizo katika maisha yangu. Kwanini lakini inakuwa hivi, kwanini? Sina pakwenda, wapi nielekee? Maneno yale yalitembea ndani ya kichwa cha yule mtoto. Akiwa njiani peke yake aliendelea kuikata mitaa mbalimbali ya jiji hilo la Mwanza. Kama kawaida alijishauri aelekee angalau nyumbani alipokuwa akiishi na wazazi wake maana nyumba ilikuwepo. Kwakuwa nyumbani kwao hapa kuwa mbali sana, hivyo haikumchukuwa muda sana kufika.

 Hata alipofika, hakuna ambacho alikiona cha muhimu kufanya. Nyumba ilimtisha huku kila akiwa ndani kumbukumbu za wazazi wake zikimwijia. Mawazo ya kitoto yakizidi kumrubuni, huku mengine yakimhakikishia kuwa, endapo ataendelea kukaa eneo lile, basi mizimu ya wazazi wake itamwijia na kumchukuwa maana ni yeye tu aliyebaki duniani.

     Kuna wakati alihisi jambo lile ni hofu yake binafsi anayojiwekea ndani ya akili zake.

‘’ Mimi ni mtoto wa kiume.. Siogopi chochote.’’ Alijitia matumaini kisha akakiendea kitanda kwa ajili ya kwenda kujipumzisha maana alikuwa amechoka sana. Akiwa juu ya kitanda, usingizi ulimchukuwa. Hapo hakuelewa tena chochote kilichokuwa kikiendelea ndani ya dunia hii.

 Masaa kadhaa baadae aliamka.  Haja kaa sawa tumbo likamuunguruma kumuonesha kuwa alikuwa na njaa kali.

 ‘’ Ah! Ndani hamna chochote, sasa nitakula vipi mie?’’ Alisema huku akiendelea kufunua masufuria na macho yake yakiangaza huku na kule ndani ya nyumba yao, lakini hakuna alichoambulia.

   Akaendelea kutafakari jinsi gani anaweza kupata chakula. Hisia za mtembea bure si sawa na mkaa bure zikamwijia mtoto yule. Hapo akatamani kutoka nyumbani kwao na kwenda kutafuta chochote kitachomwezesha kukidhi haja ya tumbo lake.

   Aliliendea genge moja lililopo karibu na nyumbani kwao. Akamkuta mamantilie akiendelea na kazi za upishi. Akamsalimu mamantilie wa genge lile na baada ya hapo aliagiza chakula alichohitaji. Naam, alikuwa na kiburi cha mchango aliyochangiwa na wasamalia wema waliyohudhuria mazishini, hata hivyo mchango ule haukuwa mwingi lakini ulimtosha kuyaendesha maisha yake kwa siku kadhaa.

   Hata alipomaliza kupata chakula, akajichanganya mitaani, huko alisurura mpaka majira ya usiku yalipofika. Hapo akarejea nyumbani kwake kwa ajili ya kulala.

   Maisha mapya ya kujitegemea akayaanza mtoto yule. Akawa yeye nd’o baba, yeye nd’o mama.

    Siku zikaanza kwenda. Hata hivyo, pesa alizokuwanazo pia hazikuchukuwa hata wiki, zikawa zote zimemwishia.

  Kila alipojaribu kwenda kuomba msaada, hakuupata. Njaa ikawa rafiki yake kipenzi, haikuhitaji kumtenga wala kumsahau kila muda ilikuwanaye. Mtoto yule wa miaka saba pekee, maji yalimfika shingoni, akakitazama kile kibanda ambacho ameachiwa kama urithi na wazazi wake. Akafikiria jinsi ambavyo njaa inamsumbua hana mbele wala nyuma, msaada hapati. Hasira zikamwijia, hapo akaona atoke na kwenda kuzurura walau aipoze njaa ama akajaribu kutafuta namna ya kuitoa.

   Katika pitapita zake ndani ya mitaa, aliweza kupita karibu na sehemu moja ambapo kunauzwa pombe za kienyeji, akiendelea na safari, mara alisikia maongezi ya walevi ambayo ingawa mwanzoni hakuyatilia maanani lakini baada ya kuyasikiliza kwa umakini alijikuta akivutikanayo kwa kiasi fulani. Akatamani kusogea eneo lile ili walau aweze kuyasikiliza kiundani zaidi.

     ‘’ Vitu kama vile nyumba, viwanja... Sijui godoro, ni mambo ambayo huwa tunayanunua ili siku moja yaweze kutufaa... Wewe vipi bwana! Hujui kama kuna siku maji yanaweza kukufika shingoni ukapatwa na tatizo halafu kiwanja ama nyumba uliyojenga vikawa msaada kwako?’’

   ‘’ Nyumba na viwanja ni msaada kwa wanangu na si kwangu bwana. Hebu usiniletee.’’

   ‘’  Ah! Wewe nd’o hamnazo kabisa. Ina maana upo radhi ufe njaa ilhali nyumbani una nyuma na kiwanja? Unashindwa vipi kuuza sasa. Wewe uza iliupate pesa ya chakula. Usikubali kufa wakati yumbani kwako un a nyumba bwana.’’

   ‘’ Ila kweli. Ukifa na njaa, nyumba utamwachia nani? Nimekwelewa binamu... Hebu mwambie Maua aongeze gongo hapa tunywe.’’

     Ingawa mada ya walevi wale ilibadilika lakini yeye kuna jambo ambalo lilimwijia ndani ya akili zake. Akajikuta akishughulishwa na jambo lile, huku kichwani akiitafakari nyumba yao ambayo kwake haioni faida yoyote, lakini pia aliifikiria njaa iliyokuwa ikiusokota utumbo wake. Hapo akazidi kuchoka zaidi na zaidi.

 Siku hiyo alijitahidi walau kuombaomba mtaani lakini hakuna binadamu aliyonesha kumjali. Kila mmoja alikuwa na matatizo yake wala asifikiri kuhusu yeye. Kijana yule njaa ikiwa imemzidi zaidi, aliamua kurejea nyumbani kwake kwa hasira na kwenda hadi kitandani kisha kilio cha uchungu kikamfika.

   Alilia sana, lakini kulia kwake hakukuwa njia ya kuiondoa njaa aliyokuwanayo. Hapo ndipo mawazo ya walevi yalipomrejea kwa mara nyingine. Akautumia muda wake kuyatafakari mawazo yale kwa umakini yeye mwenyewe huku akiiomba njaa yake ushauri.

   ‘’ Kati ya nyumba na chakula bora nini?’’ alijiuliza. Majibu yalikuja ndani ya kichwa chake na hapo akaamua. ‘’ Nauza nyumba niloachiwa na wazazi wangu. Ilimradi nisife njaa.’’

 Hatimae Mtoto yule aliibuka na suluhisho la namna ile, hapo sasa usingizi wa amani ukamwijia. Akalala usiku ule kwa raha mustarehe huku akitamani paweze kukucha iliatafute mteja ataeweza kununua nyumba ile.

     ***

Siku iliyofuata, mtoto Maduhu akiwa kama mmiliki halali wa nyumba ile aliyoachiwa na wazazi wake. Hakuhitaji ushauri kutoka kwa yeyote aliyemzidi umri. Alitangaza mnada wa nyumba ile ambayo nd’o urithi wa pekee alioachiwa na wazazi wake. Kipindi cha nyuma baba Maduhu alipopata kiasi fulani cha pesa, aliamua kununua kiwanja na kujenga nyumba ile kwa ajili ya yeye na familia yake waweze kujistiri lakini leo hii mwanae shida zimemjaa na kuona njia pekee ya kutatua matatizo yake ni kuuza nyumba. Mshauri mkuu akiwa ni tumbo lake.

            ITAENDELEA.


 USIKOSE SEHEMU YA SITA PAPA HAPA SIMULIZI MIX ENTERTAINMENT

0 comments:

Post a Comment