DUKA LA ROHO SEHEMU YA SITA
IMELETW KWAKO NA SIMULIZI MIX ENTERTAINMENT
MWANDISHI FRANK MASAI
ILIPOISHIA
Miili minne, akiwepo na
yule mtoto ambaye walimfanya kama mjomba wa Muba ilikuwa imelala kifudifudi
kwenye viti walivyokalia huku moshi mdogo ukiwatoka midomoni mwao. Nyuso zao
zilijikunyata na kuwa kama za wazee wa miaka mia moja. Damu ilikaushwa katika
miili yao kwa kutumia sumu kali inayosambaa kwa hewa.
Mubah alipoangalia sehemu
alipokanyagia kile kibanio, alikuta kuna majivu machache ambayo yalitokana na
kile kibanio kuungua.
ENDELEA
"Nadhani umeona.
Sikutaka kukuua wewe. Na hata hicho kimdoli mlichokifanya ni kitoto kidogo,
nacho kingekuwa na uhai, ningeua tu! Na nitakiua hichi nilochonacho huku baada
ya dakika tatu kupita." Lobo aliongea kwa sauti iliyojaa chuki. "Hiyo
sumu inatoka kwenye madini ya yellowstone. Madini yafananayo na almasi sema
yenyewe ni ya njano na yanayeyuka. Husambaa kwa sekunde thelathini baada ya
kuchomwa moto na hupotea kwa sekunde kumi na tano baada ya kusambaa. Kibanio
hicho nilieweka jiwe dogo sana la madini hayo. Na nilitega kifyatulio ambacho
kikifyatuka, hutengeneza moto. Nimefanikiwa hilo Mubah, asante kwa kuniletea
wateja hao. Bado dakika mbili." Lobo akamaliza kuongea na kuacha simu
hewani ili asikie upande wa pili.
"Nooooooo. Don't do
that Lobo. Please." Mubah alijikuta akipiga kelele ya nguvu huku akijaribu
kuomba msamaha. Kelele hizo zikawafikia
walinzi wa nje nao wakakimbilia ndani wote, hata wale wadunguaji nao ikabidi
kushuka kule juu haraka na kwenda ndani kutazama kile kinachoendelea.
Walichokikuta ndani, hakika kiliwatoa machozi na kuwaacha katika mshangao. Sasa
hivi miili ile ilikuwa ikipukutika kama majivu ya karatasi na mwisho wake
yakabaki mafuvu yamekaa kwenye viti.
"Sasa naweza
kukusikiliza Mubah, unadakika moja. Toka nje na mtu yeyote asikuone kama
umetoka. Nataka nikuoneshe kitu." Sauti ya Lobo ilisikika ikimuongelesha
Mubah kwenye simu. Mubah akafanya kama
alivyoambiwa.
"Sogea mbali na
nyumba yako. Na itazame kwa macho ya umakini, utaona kitu cha kukupendesha.
Zimebaki sekunde kumi na tano muda wetu uishe." Lobo alitoa ombi ambalo
Mubah alilifanya haraka na kukazia macho yake kwenye nyumba yake ambayo ndani
yake kulikuwa na wafanyakazi wenye uhai wapatao kumi na moja.
"Tano, Nne,
Tatu." Lobo akaanza kuhesabu sekunde zilizobaki hadi akafikia moja, kisha
sifuri. Macho ya Mubah yakajawa na
taharuki ya ajabu. Hakuwahi kufikiria katika maisha yake kuwa kuna siku
atashuhudia kile anachokishuhudia kwenye nyumba yake. Alishazoea ni kwenye
filamu za kivita tu! Ndio awezapo kuona yale mambo. Lakini sasa anajionea kwa macho yake yale
ambayo alikuwa anayaona kwenye filamu.
Nyumba yake ililipuka
yote na kuteketea kama vile uonavyo kwenye filamu ndege au meli inapopigwa
bomu. Nyumba ikazidi kuteketea na kuteketea hadi vile vilivyomo ndani.
Mubah akapiga magoti na
kulia kwa sauti huku akipiga chini ngumi kadhaa lakini bado hakukuta simu bali
kusikiliza kilichokuwa kinataka kujiri.
"Woooou. I like that
sound of boom, yoo. (Waau. Nimeipenda hiyo sauti ya buum, yoo)" Lobo
alisikika akiongea hayo kwenye simu baada ya ule mlipuko mkubwa kutokea kwenye
nyumba ya Mubah.
"Please Lobo, naomba
uiache familia yangu. Nakuomba Lobo, nitaacha kazi kama utakavyo." Mubah
akikuwa anaomba msamaha huku kapiga magoti katikati ya barabara ya lami
iliyokuwa inapitwa watu huku na huko kukimbia ule mshikemshike wa bomu.
"Too late Mubah.
Umechelewa mwenyewe kufanya chaguo lililo sahihi na mimi huwa sikwepeshi kauli
yangu." Lobo aliongea hayo na hapohapo sauti ya 'kitoto kichanga' ikaanza
kulia.
"Muache mwanangu we
kafiri. Na kwambia muache." Sauti ya dada wa Mubah ilisikika na kupenya
kwenye ngoma za Mubah. Wakati huo sauti ya. kichanga iliendelea kulia na mara
ikakata ghafla baada ya mlio mkali wa bastola kutoka.
"Nooo." Sauti
ya dada wa Mubah ilisikika mara moja na baada ya hapo haikusikika tena. Lobo
akiwa anachalaza mluzi usioeleweka ni wa wimbo gani, akaongea kwenye simu
ambayo Mubah alikuwa bado hajaikata.
"Dada yako kazimia
baada kuona mwanaye mdogo nikitoboa kichwa chake kwa risasi yangu. Hahahahaaa.
Nasikitika hutoona maiti zao kwa macho yako bali utaona picha za maiti yao.
Naua na kupiga picha." Lobo alimpa taarifa Mubah ambayo ilimzidishia
maumivu moyoni.
"Lobo tafadhali,
nisamehe. Kuwa na utu we' mtu. Naomba uniachie familia yangu." Mubah
aliongea kwa sauti ya kitetemeshi iliyojaa kilio.
"Ankoo tuokee."
Sauti ya mjomba kipenzi wa Mubah ilisikika.
Mubah akahisi mwenye kutaka kufa lakini hakufa bali alizidi kushikilia
simu yake sikioni.
"Anko kwa heri.
Labda tutakuja kuonana tena. Nakupenda sana ank....." Yule mjomba wa Mubah
hakumaliza kuongea kitu akamezwa na mlio wa bastola ya John Lobo na hapohapo
hakusikika tena. Mubah alilia kwa sauti ya juu ambayo ilimfanya adondoke kwenye
lami alipokuwa kapiga magoti na wakati anadondoka, akaliona gari moja jeusi
likipita karibu yake na mtu aliyekuwamo mle ndani, alimuangalia kisha
akatabasamu kwa tabasamu pana kabla hajafunga kioo cha upande wake kilichokuwa
cheusi. Sura ile ya kiume haikuwa ngeni kwake, lakini alisahau kaiona wapi. Na
wakati huo alikuwa hana nguvu zozote za kuinuka pale alipo ili akimbize lile
gari. Badala yake, alilala pale chini taratibu huku akianza kuona giza likitanda
usoni pake.
"Huyu nimeingiza
bastola mdomoni na kufumua ubongo wa nyuma kwa bastola yangu. Ha ha haaa raha
sana kuua." Hiyo ndiyo sauti ya mwisho ya kutoka kwa Lobo ambayo Mubah
aliisikia. Fahamu zikapotea kwa sababu ya
machungu tele yaliyojengeka moyoni mwake.
****
Ilichukua karibu saa moja kwa Mubah kuamka na
kushtuka tena baada ya kukumbuka yale ya nyuma. Tayari alikuwa yupo ndani ya
FISSA baada ya wafanyakazi wenzake kuja kumuokota pale chini alipokuwa kazimia.
"Husna, Husna,
Husna, Husnaaa. Kweli umeenda uncle wangu niliyekupenda kuliko wote nyumbani?
Nitacheka na nani tena, nani atanifurahisha pale niwapo na machungu. Ooh! Mungu
wangu nisaidie." Mubah alikuwa akilia kwa uchungu mbele ya wafanyakazi
wengine ndani ya FISSA.
"Nyamaza Mubah. Pole
sana. Hakuna ambaye hana hayo machungu. Tuliizoea familia yako na tuliwazoea
wafanyakazi wetu, lakini wote hatunao tena. Inatuuma sana." Dada mmoja
mrefu na mweusi lakini mwenye mvuto wa aina yake, alijaribu kumbembeleza Mubah
aliyekuwa akilia kama mtoto mdogo.
"Atalipa tu huyu
mbwa. Nitamuua kwa risasi zangu. Nitamuua Lobo na washirika wake wote.
Nishamuona mmoja, nitamsaka na kumuadhibu pumbavu yule." Mubah aliongea
kwa hasira huku akinyanyuka katika kitanda cha dispensari iliyopo mlemle ndani
ya FISSA. Akashika kitasa cha mlango wa kituo kile cha afya na kutoka humo
kituoni na kuanza kuelekea ofisi za kipepelezi hasa kule zinapokaa kamera
maalumu za kufatilia mienendo yote ya kazi za FISSA.
"Niwekee mkanda
wenye tukio zima la pale nyumbani." Mubah aliongea mbele ya mwanakaka
mmoja aliyekuwa anacheza na kompyuta za mle. Yule jamaa hakuwa na kipingamizi
hasa kwa kuwa ule mkanda unamgusa sana aliyemuamuru auweke. Akauweka na kisha
ukaanza kucheza matukio yote yaliyokuwa yanaendelea siku hiyo kabla Mubah hajazimia.
Mkanda huo ukaenda hadi mahali ambapo nyumba ya Mubah ilipolipuliwa.
"Rudisha hapo
kidogo." Mubah akamwambia maneno yale yule opareta. Jamaa bila ubishi
akarudisha sehemu ambayo inaonesha nyumba ya Mubah ndio inataka kulipuka.
"Umeona hapo?"
Mubah akaonesha kwa kidole sehemu husika anayotaka yule opareta aione. Opareta
akatazama kwa makini, alipoona kama hapaoni, akapavuta kwa ukaribu kisha akatoa
mawimbi ambayo yanasababisha picha isionekane vema.
"Okay. Hili ni bomu
toka kwenye RPG hili." Opareta akaongea baada ya kugundua hilo jambo.
"Sasa kumbe John
Lobo hayupo peke yake. Wakati nyumba hii inalipuka, mimi nilikuwa naongea naye
na alikuwa na familia yangu mbali na pale nyumbani. Lazima tuwasake hawa
washenzi." Mubah aliongea kwa hasira na kukita ngumi nzito kwenye meza
iloyomo mle ndani. Kwa hasira akageuka nyuma na kutaka kuanza kutoka lakini
baada ya kugeuka, akakutana na sura ya Malocha.
"Mubah. Unatakiwa
kupumzika kwa miezi miwili. Hii kesi tuachie sisi, tutaimaliza tu!"
Malocha alimwambia Mubah ambaye alimtazama kwa jicho kali na la ghasia.
"Huu ushauri
ungenipa kabla familia yangu haijaondoka duniani. Ungeniambia niache kazi
kabisa ili familia yangu ipone, lakini siyo sasa hivi. Nitapigana kufa na
kupona ili huyu mbwa nimkamate. Nimeshajua hayupo peke yake, nitamsaka
tu!" Mubah alimueleza Malocha na kumpita pale aliposimama kwa kutaka
kutoka ndani ya ofisi ile. Lakini Malocha akamkamata mkono na kumrudisha mbele
ya upeo wa macho yake.
"Nilipoteza familia
yangu kwa mkono wa huyuhuyu Lobo. Kwa risasi tano alizopewa, hakumkosa yeyote
katika familia yangu. Nilijawa na jazba kama wewe hivyo, nikapania kumuua na
nilifanikiwa kukamatiwa huyu mtu, nikawa naye uso kwa uso akicheka kwa dharau.
Nilikata shingo yake, kisha nikamvunja miguu kwa risasi mbili na tatu
nikamchapa nazo kifuani (MKASA HUU UPO KWENYE RIWAYA YA JINA). Nikadhani
amekufa, lakini leo hii tunapambana naye tena. Naona ni kama mzimu au shetani
ambaye hafi, au jini. Lobo huwezi kupambana naye peke yako na ukashinda vita
yake. Utapotea Mubah." Malocha aliongea kwa makini na kwa upole huku
machozi yakiwa yanataka kumtoka kwa mbali.
"Baada ya kupoteza
familia yako, ukamsaka na kumpata kisha ukamuua. Niachie na mimi, nimepoteza
familia yangu, nimsake nimpate kisha nitakuletea kiwiliwili chake." Sauti
ya kujiamini toka kwa Mubah ilipenya masikioni mwa wale wanaofatilia yale
maongezi, akiwemo Malocha.
"Nimekwisha kwambia,
acha hiyo kesi. Ni amri siyo ombi. Nakupa miezi miwili ya kupumzika, utake
usitake, utaenda mapumziko." Malocha ikabidi atumie nguvu za uongozi wake
kuwasilisha hisia zake. Mubah akatulia kwa muda kabla hajarudi kwa yule opareta
na kuchukua ule mkanda wenye tukio zima la siku hiyo.
ITAENDELEA...
KWENDA SEHEMU YA SABA BOFYA HAPHA>> SEHEMU YA SABA
0 comments:
Post a Comment