NIENDE WAPI? ‘’ Dunia imenichukia’’
IMELETWA KWAKO NA SIMULIZI MIX ENTERTAINMENT
MWANDISHI:
ZUBERY RAZUUR MAVUGO.
SEHEMU YA SABA.
ILIPOISHIA:
Eh! Mungu wagu, nadhani unayatambua
matatizo yangu tena kuliko hata mimi. Nakuomba nisaidie hizi pesa zote ziingie
mikononi mwangu. Tazama, endapo nitazikosa bila shaka mke wangu atapoteza
maisha nakuomba mwenyezi Mungu naomba unihurumie mimi. Najua pengine hii ni
njia ya wewe kuniokoa hivyo naomba pia unisimamie. Bwana Mashaka aliongea
maneno yale huku akiwa amejibanza sehemu, akifuatilia kila kilichokuwa
kikiendelea. Mate yakitamani kumtoka, moyo ukimwenda mbio, hakuna alichokuwa
akikifikiria zaidi ya kuokoa maisha ya mke wake.
ENDELEA... Sehemu
ile alikaa kwa muda mrefu pasina kujua nini ambachokilikuwa kikiendelea ndani.
Nani kwanini watu wale walichelewa kutoka namna hiyo? ingawa alikuwa pia na
mashaka kama jina lake lakini alijipa imani lazma mambo yangemalizika muda si
mwingi. Akabaki ametulia hivyohivyo huku macho yake yakiendelea kufanya
uchunguzi.
***
‘’ Sasa inabidi hapa
usaini kwa ajili ya uthibitisho kuwa umeuza hiki kiwanja.’’
‘’ Ah! Wazee.. Mbona
siioni haja ya mimi kusaini? Kwakuwa tumeshakubaliana, nisingependelea
tusainishane... ama hatuaminiani?’’
‘’ Hahahhaha..
Maduhu, kukwambia usaini haina maana kwamba huaminiki...’’
‘’ Kumbe maada yake
nini dalali? Mnadhani hiki kiwanja sio urithi wa baba yangu? Ama nini?’’
‘’ Hii maana yake ni
uthibitisho kuwa kiwanja umeuza kiuhalali. Haya maandishi ni msaada kwako na
kwa mnunuzi hivyo kama kumsaidia, inabidi uweke sahihi yako hapa.’’
‘’ Haka katoto
bwana, mbona maneno mengi mdomoni?’’ Mnunuaji wa eneo alisema.
‘’ Hawa
ni watoto wa kisasa bwana.’’
Kicheko cha furaha kikawatoka.
‘’ Hata
hivyo, mimi naona kama mnanichanganya tu.’’
‘’
Kwanini?’’
‘’Katika
maisha yangu bado sijabahatika kusoma, hivyo sijui hata hiyo saini
inaandikwaje.’’
‘’ Ina
maana kumbe ujanja wote huo hujui hata kusaini?’’
‘’ Ah! Wengine bado hatujabahatika kusoma, wenyewe
simnaona umri wangu ulivo mdogo?’’
‘’ Haka katoto kana umri mdogo lakini kana
mambo makubwa... Loh!’’
Ha! Hapo ikabidi kazi iwe nyingine. Lakini
hakukuwa na tatizo maana kwa mwenyekiti wa kitongoji hakukuwa mbali,
kwakulitambua hilo akaomba atoke kidogo kwa ajili ya kumfuatia muhuli wa dole
gumba mtoto yule iliaweze kutimiza haki yake.
Wakati anatoka, Mashaka kidogo moyo wake
ukapata afadhali maana alikuwa ameshaanza kuhisi huenda wasingetoka mida ile.
Hapo pumzi nyingine zikamwijia, nguvu mpya za uvutaji subra zikamfikia. hata
hivyo mwenyekiti yule hakuchukuwa muda sana tangu atoke, alirejea kwa mara
nyingine na kumpatia mtoto yule haki yake. Hapo ndipo alipopatiwa na pesa zake
zote, huku akimwachia dalali kiwango walichokuwa wamepangiana.
Hakuwa na utani kwenye pesa hata kidogo,
aliushikilia mkoba vyema kabisa tena bila masihara.
‘’ Vipi bwana naona una mashaka sana...
Tukuitie maaskari wakusidikize?’’ Alitania mmoja kati ya wale watu waliyonunua
kiwanja kile baada ya kumuona mtoto yule akiwa katika hali ya kutojiamini
kutokana na kutowahi kushikilia pesa nyingi namna ile.
‘’ Hii haihitaji usaidizi wakubwa... Maaskari
wataniomba kitu kidogo mimi sitaki kutoa chochote, niacheni tu mwenyewe.’’
Mtoto Maduhu aliongea maneno yale yaliyowapelekea wanunuzi wa kiwanja kile
waangue kicheko. Hata hivyo hawakukawia sana, waliamua kulifuata gari
walilokujanalo na moja kwa moja wakapanda kisha wakaianza safari ya kwenda
walipopajua wenyewe.
Dalali alimuaga mtoto yule na yeye kuchukuwa
hamsini zake huku mwenyekiti akiwa ni kama ameshachukuwa dakika kadhaa tangu
afike nyumbani kwake.
Hivi sasa mtoto Maduhu alikuwa peke yake.
Akitembea kwa kujishtukia huku pesa zilizokuwa ndani ya mkoba akiwa kazikumbata
juu ya kifua chake. Alipita njia isiyo na watu wengi akihofia kupita njia yenye
msongamano wa watu iliasije kuibiwa bure. Mawazo yake yote yalidhani huenda
katika safari alikuwa yeye peke yake, kumbe sivyo.
Bwana Mashaka alikuwa akimfuata muda wote.
Kila Maduhu alipoigeuza shingo yake, Mashaka nae alijigeuza na kujifanya yupo
bize na jambo tofauti, kumbe malengo yake yote yalikuwa ni ule mkoba ambao
aliamini akiupata tu, atakuwa amepata kila kitu na kuyaokoa maisha ya mkewe.
Hata Maduhu alipopita kwenye njia
iliyohifadhi kiuchochoro kidogo. Hapo ndipo bwana Mashaka nadhiri yake
alipotamani kuitoa. Kile alichodhamiria kukifanya aliona ni muda muafaka sasa.
Kwa usaidizi wa maneno ya wahenga yasemayo, ‘Chelewa chelewa utakuta mwana si
wako’ alimfuata kwa nyuma na kumpiga kabali shingoni mtoto yule kitendo
kilichompelekea ashindwe hata kupiga kelele akabaki akifurukuta, macho
yakimtoka huku akimwona malaika mtoa roho kwa mbali akimtamani.
Kwa haraka ileile, Mashaka aliuchukuwa mkoba
ule uliyokuwa mikononi mwa mtoto yule bila huruma akamsukumia pembeni ambako
kulikuwa na miiba kitendo kilichompelekea aiparamie miia ile. Hapo Mashaka
akapotea bila hata kuonekana machoni mwa mtoto yule. Maumivu ya miiba
yalimfanya mtoto yule alie kwa uchungu huku akiishikilia shingo yake na
kujitahidi kumeza mate maana koromeo lilikuwa limemkauka. Akajiinua huku
akapiga ukunga akijaribu kumfukuza mtu
ambaye hakujua hata ni wapi alipoelekea. Saa moja lilipita akitafuta, masaa
mawili, matatu lakini hakuchoka, moyoni mwake alijipa imani huenda angemwona
mwizi wake. Aliendelea kuhangaika kutafuta hatimae giza lilianza kuingia ndipo
hapo alipogundua kuwa, pesa zake zimeibwa na hawezi kuzipata tena.
Hapo
ndipo akili zikamtuma aelekee kituo cha polisi kwa ajili ya kutoa taarifa
iliaweze kupatiwa msaada.
Hata alipofika kituo cha polisi na kuelezea
shida yake ni kama alikuwa amedhamiria kuwachekesha na mwishowe kuwakera
maaskari waliyokuwa zamu usiku huo.
‘’ Mimi mwenyewe na ukubwa wangu sijawahi
kushika milioni tano.. Ije wewe mtoto mdogo tena uliyevalia mavazi ya watoto wa
mtaa ni.’’
‘’ Afande, naomba mnielewe... Pesa zangu
nimeibiwa sina mbele wala nyuma.’’
‘’ Hivi wewe mtoto, unavuta bangi eh! Ama
umeona hauna sehemu ya kulala giza limeingia sasa unakuja kutusumbua ilitukupe
hifadhi ya kulala. Afande Masele hebu chukua huyu mtoto weka ndani mara moja
kwa kosa la kuvuta bangi na kuja kuleta vurugu kituoni.’’ Mtoto Maduhu hakuna
msaada aliyoupata zaidi ya kuchukuliwa na kuwekwa rumande.
Ndani ya maisha yake hakuwahi kuwaza hata siku
moja kuingia sero. Alikuwa akiishia kuzisikia simulizi na mateso wayapatayo
wale ambao wamewahi kuingia ndani mule. Kila alipozisikia simulizi zile,
alimuomba Mungu asijewahi kuingia ndani
mule hata siku moja. Leo hii amejikuta yupo tena kiurahisi haswa! Hakuwaza kama
kuja kwake kuomba msaada kungempelekea kufanyiwa tkitendo kama kile.
Wakati mwingine wale tudhaniao ni wema kwetu
na kuwaamini kama misaada, waweza kuwa chanzo cha maumivu na majuto kwetu. Moyo
wa mwanadamu haubadilishwi kwa kazi anayofanya ama mavazi anayovaa bali kwa
mapito aliyopitia.
***
Mashaka alikuwa katika hali ya kujilaumu sana.
Alijiona ni mmoja kati ya watu waliyoshiriki dhambi kubwa kuliko zote
ulimwenguni. Katika maisha yake yote, amelelewa chini ya misimamo ya kidini,
hakuwahi kuwaza hata siku moja kuchukuwa cha mtu bila ridhaa yake wala kuiba
cha mtu. Ni amri kumi za torati ambazo hakuhitaji hata siku moja awahi
kuzivunja lakini shida pekee ndizo zilizompelekea huko.
Muda huo alikuwa ndani ya chumba chake ambacho
ndicho alichopanga baada ya kukosa mbele wala nyuma. Pesa zile alizomnyang’anya
mtoto wa watu, aliendelea kuzitazama hukuakihisi laana yake ina mwandama. Roho
ilikuwa ikimuuma sana, akifikiria ni kwanini amemuumiza kiasi kile mtoto wa
watu? Na je, mtoto yule aliyeonekanawazi kabisa kuwa anashida za muhimu mpaka
kufikia kuuza kiwanja, ni wapi alipo muda huo? Je, Mungu atamsamehe kwa jambo
lile.
Usiku mzima nafsi ya Mashaka ilikuwa katika
Mashaka tu.
Hata
hivyo, kila alipokumbuka umuhimu wa maisha ya mkewe, hofu yote ilimwondoka. Akijisemea,
‘ Mungu anisamehe, maana sijafanya vile kwa kupenda’ huku akiiombea siku mpya
iweze kuingia na yeye aelekee moja kwa moja hospitali kwa ajili ya kupeleka
pesa na mkewe aanze kufanyiwa uparesheni maana alikuwa katika hali mbaya sana.
Alijing’ang’aniza kuutafuta usingizi, ingawa hofu lilimchukuwa na kuutwaa
usingizi wote lakini baada ya muda pasina hata mwenyewe kujielewa alijikuta
akisinzia.
ITAENDELEA.
KWENDA SEHEMU YA NANE BOFYA HAPA=> SEHEMU YA NANE
KWENDA SEHEMU YA NANE BOFYA HAPA=> SEHEMU YA NANE
0 comments:
Post a Comment