DUKA LA ROHO SEHEMU YA KUMI
IMELETWA KWAKO NA SIMULIZI MIX ENTERTAINMENT
MWANDISHI FRANK MASAI
ILIPOISHIA
"Lisa yupo hatarini
bila yeye kujitambua. Mume wake si mtu kama anavyodhani, muda wowote anamgeuka.
Huyo ndio sababu ya Lobo kujua njia nyingi za FISSA kwa sababu anamuwekea GPS
kila anapojua zimetolewa. Nakwambia haya lakini usimwambie chochote kile.
Atakuja kuju a ya kumaliza mambo haya." Malocha alimuelekeza Mubah mambo
kadhaa, kisha kuanza kumpa siri za Lisa ambaye alikuwa anacheza na mwanaye anayesheherekea
siku yake ya kuzaliwa.
"Kwa hiyo mume wa
Lisa anashirikiana na Lobo."
ENDELEA
"Hilo ndilo
jibu." Malocha akamjibu kifupi na kumuacha Mubah bila swali na badala yake
akatwaa simu yake na kubofya namba kadhaa ambazo alimpigia simu Lisa.
****
Ukimya ulitawala ndani ya gari alilochukua
Mubah kwenda Kivule yalipo makao mapya ya FISSA ndogo ikiongozwa na Malocha.
Ukimya huo ni kwa sababu Lisa alichimba mkwara ambao Mubah alikubali yaishe
kuliko kuzidi kuchongoa mdomo wake.
Baada ya dakika kadhaa,
walikuwa wamekwishafika kwenye nyumba hiyo ambayo wanaitumia kama makazi yao.
"Heee! Malocha leo
upo huku." Lisa akamuita mkuu wake jina ambalo walishazoeana kuitana
shuleni.
"Leo nimekuja
kuwatembelea aisee." Malocha akajibu huku anatabasamu.
"Mmmh! Haya
karibu." Lisa aliongea kwa sauti ya furaha huku akisogea kwenye kochi
lililo sebuleni pale walipofikia.
"Hey. Martina,
hujambo mama." Malocha akamsalimia Martina mtoto wa Lisa.
"Sijambo
shikamoo."
"Marahabaa. Mimi ni
Anko Malocha."
"Shikamoo Anko
Malocha."
"Leo sherehe yako ya
kuzaliwa. Nikupe zawadi nisikupeee." Malocha alimuuliza kwa furaha
Martina.
"Nipee Ankoo."
Martina naye akajibu huku mikono yake akiipunga kama vile kaungua. Malocha
akatabasamu baada ya kumuona mtoto mwenye furaha kiasi kile.
Akaenda chumba fulani
kisha akatoka na baiskeli moja ya rangi ya pinki, rangi ambayo hakuna watoto wa
kike wasiyoipenda.
"Asante Anko."
Martina alimshukuru Malocha na kumkumbatia kwa nguvu.
"Haya Martina. Nenda
na yule pale mkaendeshe baiskeli huko." Malocha alimkabidhi Martina kwa
jamaa mmoja ambaye alimchukua Martina na kumpeleka uwani mwa nyumba ile
walipoanza kufurahia zawadi hiyo.
"Okay Lisa.
Nimekuita hapa kukwambia kuwa FISSA tumefukuzwa kazi lakini tutarudi baada ya
mambo fulani kukamilika. FISSA sasa hivi wameingia watu wapya lakini ni watu
ambao kwangu mimi siwapi sana nafasi." Malocha akaweka tuo kabla ya kuzidi
kutiririka. "Sasa kwa kuanzia,
tuanze na kazi ya kuutafuta ukweli kuhusu Lobo. Ila kwanza nataka kusikia kama upo
tayari kufanya kazi na sisi." Malocha akatupa swali kabla hajaendelea na
mengine.
"Nimezaliwa kufanya
hayo. Siwezi kukataa na wakati huyo ndiye mimi." Lisa akajibu kwa
kujiamini na Malocha akamchukua mwanadada huyu jasiri na kwenda naye kwenye
chumba maalumu kwa ajili ya upelelezi. Wakati huo Mubah alikuwa kimya
akiwafuata wafanyakazi wenzake kwa nyuma.
"Kazi yetu inaanzia
hapa." Malocha akamuonesha gari ambalo waliling'amua namba zake. Maelezo kadhaa yakaanza baada ya kumuonesha
gari lile. Hiyo yote ni katika kumuelekeza Lisa ili aelewe nini sababu ya
kuoneshwa picha hiyo.
"Sasa tumekwisha
fatilia gari hili ni la nani na ninataka wewe na Mubah muongozane hadi kwa huyu
bwana kisha mumuhoji maswali kadhaa. Kama hatojibu, basi tumieni mbinu za
kumchukua na kumleta huku. Atajibu tu." Malocha akamaliza maongezi yale na
kuwatazama watu wale.
"Hamna tatizo. Ila
naomba mkae na Martina vizuri." Lisa akatoa ombi na.kuchukua dhana kadhaa
kwa ajili ya kujilinda na kujijulisha (vitambulisho). Baada ya hapo akatoka nje
na kuwaacha Mubah na Malocha wakiwa na opareta wao wakijadiliana.
"Mkuu. Wakati
nazimia nilikwambia nimemuona mtu kwenye hii gari. Mtu huyo ni Gunner, mume wa
Lisa. Kitu kilichonifanya nijue ni kibanio cha Martina ambacho ni sawa na kile
ambacho kilimwaga sumu kule nyumbani. Na mbaya zaidi, huyu mtoto anafundishwa
ujasusi na baba yake." Mubah akatoa taarifa kadha wa kadha hadi pale
aliporidhika ndipo alipoamua kutoka nje akiongozana na Malocha.
"Hicho kibanio
lazima kibaki ili nacho tujue ni wapi kimetoka." Malocha aliongea huku
wakiendelea kwenda sehemu nyingine.
"Sawa mkuu. Ngoja
sisi twende." Mubah alikubali wakati alipofika sebuleni na kumuona Lisa
akiwa anawasubiri.
"Umemuaga kijana
wetu." Malocha alimuiliza Lisa kama kamuaga Martina.
"Ndio. Naona hana
tatizo. Yupo na furaha." Lisa akajibu huku akinyanyuka ambapo alitoka nje
na kukwea gari ambalo wameandaliwa kwa ajili ya kwenda walipopanga. **** Majira
ya saa moja jioni, Mubah, Lisa wakiwa na dereva wao, walifika eneo la Sinza na
moja kwa moja wakaenda nyumba ambayo walipata maelezo kuwa mtuhumiwa wao
anapatikana. Lakini cha kushangaza walipofika, walikuta watu wamefurika na
vilio vikisikika huku na kule.
Walisogea na kuuliza kuna
nini, wakajibiwa kuwa Mzee Mofo, ambaye ndiye walimfuata amefariki dunia kwa
kuchinjwa kama kuku.
Ilikuwa ni hadithi ya
kusikitisha kwenye kila kichwa cha aliyeisikia, lakini hakuna ambaye alikuwa
tayari kuingilia hayo maswala kwa kuwashuku watu fulani.
"Lisa tunafanyaje
sasa. Doa limeshaingia kwenye nguo nyeupe kama uonavyo." Mubah alimuuliza
Lisa baada ya kufuata watu kadhaa na watu hao kutotoa ushirikiano wowote katika
kujibu.
"Mambo magumu hapa
Mubah. Ila tujitahidi tuonane na mke wake kabla hawajaenda mazikoni hiyo
kesho." Lisa alishauri huku macho yakiwa yametua mbele ya mwanamke mmoja,
mnene kiasi na mwenye weupe wa asili.
Alikuwa katika majonzi mazito na baadhi ya wanawake wenzake walikuwa
pembeni yake wakimpooza kwa kila neno zuri.
Mara kwa mara alijigonga
kifua na kuwa mtu wa kulalamika kwa lugha ya Kidigo.
"Sawa sawa.
Yaonekana kuna jambo analalamika kwa sababu ya kifo cha mumewe. Ikibidi tumtoe
pale sasa hivi tukamuhoji pembeni." Mubah alishauri kitu ambacho Lisa
hakukawia kukifanya. Akasonga hadi pale ambapo yule mwanamke anapolia, na kisha
kwa chati akamuomba watoke eneo lile mara moja wakazungumze.
Ilikuwa ngumu kwa
mwanadada yule kukubali, lakini baada ya Lisa kujitambulisha vema, hatimaye
mwanamke yule alikubali na kwenda naye katika chumba ambacho aliona ni sawa kwa
kumpasha yote yaliyojiri.
"Sijui dada yangu.
Roho inaniuma sana kumpoteza mume wangu. Ila yote hiyo ni kwa sababu ya
upinzani wa kibiashara tu. Wameniulia mume wangu ofisini kwake, na kisha kwenye
ukuta ule wameandika Duka La Roho." Ni maneno ya yule mwanamke akijaribu
kuelezea kilichokuwa kinaendelea mbele ya Lisa, wakati huo Mubah alikuwa nje.
"Ofisi yake ipo
wapi."
"Zipo Ukonga,
Madafu."
"Okay. Ngoja twende
huko tukaangalie taarifa yoyote. Naomba funguo za huko na kibali pia."
Lisa aliongea na yule dada, kisha akamuacha atafute alichokihitaji. Baada ya sekunde kadhaa, mke wa Mofo alikuwa
amekamata funguo za ofisi zile za akiba na karatasi moja ambayo itasimama kama
kibali.
Lisa akapokea vitu hivyo
na kisha akataka kutoka mle ndani. Lakini ni kama Mke wa Mofo alikuwa kasahau
jambo, akamuita huku akiwa na uoga mkubwa machoni pake.
"Dada. Maisha yangu
pia yapo matatani kwa sababu ya mume wangu. Roho yangu pia ipo dukani. Njia ya
kuinunua ni kutosema ukweli juu ya hili jambo. Lakini siwezi nikakaa na siri
hii kwa sababu tayari mume wangu si naye tena. Naomba nikwambie wewe." Mke
wa Mofo alikuwa akiangalia huku na huko wakati akitamka haya.
"Eheee! Niambie dada
yangu." Lisa akasogea karibu na kumshika mkono na kumkalisha kwenye
kitanda cha chumba kile.
"Mume wangu alikuwa
anauza madawa ya kulevya na ni mshirika mkubwa wa makundi haya makubwa ya kuuza
madawa. Watu kama Mafia, Yakuza nakadhalika, alishirikiana nao sana. Baada ya
kuona kapata mafanikio, akaomba kujitoa kundini ili aendeshe maisha yake
kiuhalali. Kitendo hicho kilimpa machaguo mawili. Kama anataka kujitoa basi
auze roho yake au anunue. Yaani angetaka kununua roho yake, akubali kufirisiwa.
Angetaka kuuza, basi afe lakini mali zitabaki chini ya familia yako. Wakampa
siku mbili ya kununua au kuuza.
Mume wangu akadhani ni
utani na hakuna ambaye ataweza kumuua. Akajidhatiti na kuweka walinzi nyumbani
na popote alipokuwapo. Siku ya pili inatimia tu! Mume wangu akauawa na maiti
kukutwa ofisini huku mwili umekaa kwenye kochi na kichwa kimewekwa juu ya
meza." Mke wa Mofo alimaliza maelezo kadhaa anayoyajua.
"Hiyo kampuni ni
yake kweli?" Lisa akatupa swali lingine na kumfanya yule dada kuzidi kuwa
na mashaka. Ila kwa kuwa aliyavulia maji nguo, basi kuyaoga ni njia inayofuata.
"Si ya kwake. Na
ndio ofisi kubwa ya kusambaza madawa nchini Tanzania." Akajibu dada wa
watu.
"Sasa ipo chini ya
nani?" Mke wa Mofo akaangalia tena pande kadha wa kadha ijapokuwa chumba
kile walikuwamo wawili tu. Akasogea karibu zaidi kwa Lisa na kwa sauti ya chini
akaanza kujibu.
"Ipo chini ya tajiri
mmoja Mkam......" Kimya kikamkumba dada yule. Hakumaliza sentensi yake.
Lisa alipomuangalia mwanamke mwenzake, alimshuhudia akidondoka kitandani kama
mzigo huku damu zikimvuja kichwani palipokuwa pana tobo la risasi. Ukuta nao
ulikuwa umechafuka kwa damu hizo.
ITAENDELEA
KWENDA SEHEMU YA KUMI NA MOJA BOFYA HAPA=>SEHEMU YA KUMI NA MOJA
0 comments:
Post a Comment