DUKA LA ROHO SEHEMU YA KUMI NA NNE
IMELETWA KWAKO NA SIMULIZI MIX ENTERTAINMENT
MWANDISHI FRANK MASAI
ILIPOISHIA
Lisa akaangalia maskani
yake kwa mara ya mwisho, hapo akamuona Gunner akitoka nje ya nyumba yao na
macho yake yakaenda kwenye gari la Malocha. Akakimbia na ghafla alikuwa kama
kaishiwa nguvu baada ya kuuona mwili wa Zakia ukiwa hauna uhai.
Gunner akaufuata ule
mwili na kisha kwa uchungu akaupakata na kulia kwa sauti ya juu. Wakati huo
pikipiki inayoendeshwa na Malocha, ilishatimua vumbi na kuacha tafulani pale
mtaani.
ENDELEA
Gunner akaangalia
pikipiki aliyokuwa anaendesha Malocha ambayo sasa ilikuwa inakata kona kuingia
mtaa mwingine mbali na pale. Gunner akauma meno kwa hasira kisha akaanza kupiga
ngumi chini. Akaona hiyo haitoshi, akaifata ile bunduki ya Zakia na kuijaza
risasi, kisha kwa fujo akaanza kumwaga risasi hizo angani. Ni kama alikuwa
kachanganyikiwa kwa sababu ya kifo cha Zakia.
Baada ya risasi kuisha,
akausogelea mwili wa Zakia na kuutazama tena huku machozi yakimtoka zaidi ya
pale. Lakini kulia siyo suluhisho la tatizo kwa mwanaume yeyote. Na yeye alijua
hilo, akatwaa simu ya Zakia aliyokuwanayo mfukoni na kisha akabofya namba
kadhaa na kuweka sikioni.
"Haloo Lobo.
Wamemuua Zakia." Gunner akaongea na kutulia kusikiliza upande wa pili.
"Ni Malocha na Lisa ndio wamefanya hivi." Gunner akajibu tena na
kumsikiliza Lobo. "Okay. Nataka umuue Lisa. Huyu Malocha nitamuua mimi.
Nenda kule nyumba ya shambani, Zakia kampeleka Martina kule. Kichukue hicho
kifisadi na kukileta hapo kambini, mimi nipo njiani naanza kuja huko ili
tupange." Gunner aliongea kwa hasira huku akianza kuondoka eneo lile
akimuacha Zakia palepale alipofia.
Akaenda kwenye gari lake
ambalo lilikuwa mbali na nyumbani kwake kwa sababu angeliweka karibu, basi
mkewe angelisikia pale wakati anataka kutoroka. Gunner akawasha gari lile na
kutitia sehemu nyingine. **** Majira ya saa mbili usiku, vyombo vya habari hasa
vya matangazo ya runinga, vilikuwa vikionesha taarifa ya masamaria mwema kuuawa
na magaidi hatari waliokuwa hawajulikani kama magaidi bali wananchi wa
kawaida. Picha ya Zakia kama msamaria
huyo, ilioneshwa kwenye runinga na baadaye zikapita picha za Malocha na Lisa
kama magaidi hatari yaliyoondoa roho ya Zakia.
"Nasema hivii. Watu
hawa hatari, watakamatwa na watahukumiwa hadharani adhabu ya kinyongo. Tunatoa
taarifa kwa wananchi wote, kama utawaona watu hawa, toa taarifa kituo cha
usalama chochote, nasi tutakuzawadia zawadi nono ya pesa taslimu. Usikose
zawadi hii kwa kuyaficha haya ........." Runinga ikazimwa na Malocha baada
ya kuitathmini ile taarifa iliyokuwa unasomwa na Kamanda wa Polisi Kanda ya
Mashariki.
"Wapumbavu hawa.
Wamekwisha wekwa dukani na roho zao. Uoga umekithiri katika nafsi zao. Shenzi
kabisa." Malocha aliongea na kuendelea kutakana matusi mbalimbali mbele ya
Lisa aliyekuwa kakaa kwenye kitanda na mawazo tele yakimzonga. Walishafika nyumba ya Kivule na sasa walikuwa
wametulia wakitafakari ili na lile hasa kwa kilichotokea muda uliopita.
"Malocha. Martina
wangu. Sijui nitampataje mwanangu. Naomba mnisaidie jamani." Lisa aliongea
kwa uchungu na chozi la uchungu wa mwana likamtiririka mwanamke huyu.
"Usijali Lisa.
Hawawezi kumfanya chochote na tutampata tu. Najua tumekwisha wachokoza, sasa
hivi wanapanga cha kufanya ili watuvute twende. Huo ndio utakuwa wakati wa
kumwokoa Martina. Hawawezi kumdhulu." Malocha aliongea kwa kumsugua sugua
bega binti yule na kwa faraja hiyo, alijikuta akimkumbatia Malocha.
"Usijali Lisa. Everything will be alright." Malocha kwa kunong'ona
akambembeleza Lisa ambaye kama mama wengine ambavyo wangekuwa na wasiwasi
kuhusu watoto wao, basi na yeye yupo vivyo hivyo.
Baada ya dakika kumi na
tano, usingizi wa mchoko na maumivu ambayo yalitokana na kipigo toka kwa
Gunner, ukamkamata Lisa na bila hiyana akaruhusu usingizi huo uwe kulala. Malocha akamfunika vema Lisa na kisha akatoka
nje ya chumba kile na kuelekea sebuleni ambapo alimkuta Mubah katika hamasa
kubwa ya kutaka kujua nini kilitokea hadi mchumba wake akawa hai na kuwa
anashirikiana na wakina Lobo.
"Niambie Malocha.
Nini kipo katikati hadi tunaanzisha mahusiano na magaidi halafu hata
hamtumbii." Mubah alikuwa anaongea kwa kufoka.
"Ulisahau jana
wakati unataka kumuambia Lisa habari za Gunner, nami nilikuambia, jambo
usilolijua ni sawa na usiku wa kiza." Malocha kwa makini akamwambia Mubah
na kisha akaenda kwenye kochi moja na kukaa kisha akakunja nne kabla hajaanza
kuutikisa mguu wake uliojuu ya mwingine kwa chati.
"Kwa hiyo ulikuwa
unajua kuwa Zakia ni mbwa wa wakina Lobo." Mubah alimuuliza Malocha kwa
kumtolea macho haswa.
"Ndio. Na si wewe
tu. Karibu kila mfanyakazi mle FISSA, anamahusiano na gaidi. Lakini magaidi
hawa si kama wanashirikiana na wakina Lobo, sema wapo kwa ajili ya dharula tu.
Kama hivyo Zakia amekufa, basi anachukuliwa mwingine." Malocha akamjibu
Mubah ambaye kwa hasira akaupiga kofi ule mguu wa Malocha uliokuwa
unatingishika. Akaona haitoshi, akaushusha kwa nguvu mguu ule chini na kumfanya
Malocha atabasamu tu.
"Hakuna GPS
iliyotumika kuifata familia yako. Ni Zakia ndiye aliyetoa taarifa kwa Lobo ni
wapi walipopelekwa. Na wakati huo mimi nilikuwa sijui kama Zakia pia
anamahusiano na Lobo. Nilijua baada ya kufuatilia mawasiliano yote ambayo Lobo
alikuwa akiyafanya. Na baadaye nikafuatilia ya Zakia na hadi hapa jana,
nilikuwa nayafatilia. Hakuna mwanamke
ambaye alikuwa anapendana na Gunner kama Zakia. Gunner alikuwa anampenda huyu
mwanamke mpaka kero na ndio maana nikamuua ili kumpandisha mori yule
mbwa." Malocha alizidi kutiririka ukweli wakati huo Mubah alikuwa
anamuangalia kwa macho ya hasira.
"Kwa hiyo wajua
mengi tu. Mbona hukutuambia wewe mtu. Unakuwa mchoyo wa taarifa za muhimu kama
hizi? We ni mtu gani Malocha." Mubah alibwata kama mbwa aliyeona sura
asiyoifahamu.
"Mapenzi upofu,
Mubah. Ulikuwa kipofu kipindi kile. Ningekwambia kuwa Gunner anatoka na mchumba
wako, usingeamini na zaidi ungeniona mchonganishi. Hiyo yote ni kwa sababu
ulikuwa umependa. Na isingetokea kwako tu, hata kwa Lisa." Mubah
akatafakari na kuyachambua maneno hayo na kuona undani wenye ukweli kuhusu
hilo. Akapunguza jazba na kukaa kwenye
kochi huku kajiinamia.
"Lakini Mkuu,
ungeniambia tu! Ningekuwa makini japo ni kweli nilikuwa nampenda huyu
mshenzi."
"Ukishakuwa ndani ya
mapenzi, ni sawa na kuwepo ndani ya pango lenye giza na hujui wapi pa kutokea
wala wapi pa kushika. Unaweza kuisikia sauti inaita, lakini hujui pa kuanzia
ili uiombe msaada. Ungesikia
nilichokwambia, lakini ungekuwa huna uwezo wa kuamini." Malocha akazidi
kuufunua ukweli ambao ulikuwa ni kiza kinene mbele ya macho ya Mubah.
"Nimekuelewa sana
Mkuu. Lakini naomba safari hii, aliyeshiriki kuangamiza familia yangu, huyu
Lobo, msimuue. Nahitaji kumuua mimi mwenyewe kwa risasi zenye idadi ya familia
yangu." Mubah aliongea kwa hamasa na kumfanya Malocha akubaliane na ombi
hilo. Swali likabaki, wataweza? **** Mida ya saa nne usiku, ndani ya kambi
kubwa ya Gunner iliyopo katika pori moja huko nje kidogo ya Jiji Dar es Salaam,
watu kadhaa walikuwa kwenye chumba cha kompyuta wakijaribu kutafuta mawasiliano
ya Malocha. Ilikuwa ngumu sana kwani safari hii Malocha hakuwa tayari
kufuatiliwa kama wakati yupo ndani ya FISSA. Lobo alijaribu kumbembeleza
Martina ili aseme ni wapi wapo wakina Malocha, lakini mtoto yule alikuwa hana
uhakika wa akisemacho. Mara tulienda sokoni, mara barabara inamaji, mara
tukapanda na kushuka daraja, haeleweki. Huko ndio kuelekeza alikokuwa
anaelekeza Martina.
"Boss." Sauti
nzito na yenye ukatili ndani yake ilimuita mkuu wake. Alikuwa ni kijana mrefu na mwenye misuli na
asili ya Kirusi ilikuwa imemtapakaa kila sehemu ya mwili wake. Gunner akasogea pale alipoitwa na mtaalamu
yule aloyekuwa nguli wa kompyuta katika kambi ile. "Tumekosa mawasiliano
ya hawa watu kwa njia hii." Jamaa yule alijibu kwa uhakika na kumfanya
Gunner kutulia kwa sekunde kadhaa akitafakari jambo huku akikuna kidevu chake
chenye ndevu za kiasi na zimechongwa kwa ufahamu na mtaalamu sijui kutoka wapi.
Macho ya Gunner yalikuwa
hayatulii katika anga la jumba lile lililokuwa limetapakaa nyaya za umeme mkali
ambao waliutengeneza wenyewe kwa kutumia madini hatari ya sumu ya Yellowstone.
Haijulikani madini hayo ya njano yanachimbwa wapi, lakini ni madini yanayoweza
kuwa hatari kuliko hata Uranium.
"Fungua SGT."
Maneno hayo yakamfanya yule mtaalam wa TEHAMA kubaki akimshangaa mkuu wake kwa
maamuzi mazito kama hayo.
"Mkuu. Lakini ni
mapema sana kufungua SGT. Tutakamatwa mapema sana kabla ya mpango wetu
kukamilika." Yule mtaalam akatoa wazo lake.
"Nimeshasema Boyka.
Just Do It." Yule bwana aliyejulikana kwa jina Boyka akaamua kufanya
alichoambiwa. Akafungua mtambo ghali
kabisa duniani ambao uliibwa toka mikononi mwa Wachina na watu wasiojulikana na
ulikuwa unaogopwa na yeyote ambaye anahusika uhalifu, uliweza kunasa wahalifu
karibu sitini baada ya kuindwa.
SGT (Satellite GPS and
Traces). Ni mtambo ambao unaweza kuzima Satellites zote duniani na vifaa vyote
vinavyoweza kufuatwa kama vina GPS. Hapa nazungumzia simu, kompyuta na vifaa
vyote viwezavyo kutumia Internets.
Mtambo huu, Gunner
akishirikiana na wenzake baadhi kuuiba. Waliuiba kwenye Chuo cha Sayansi
kilichopo nchini China baada ya kukamilika kufanyiwa majaribio na kuwa tayari
kutumika kwa ajili ya kuiba siri mbalimbali hasa za kipelelezi.
Marekani walipopata sifa
za mtambo huo, udenda ukawatoka na kutaka kuumiliki. Wakatengeneza mtambo wao
mdogo kutokana na wazo walilopewa na Wanasayansi wao wakuu. Mtambo
walioutengeneza waliuita Ant-SGT. Yaani hata wakiwasha STG mtambo huo hauwezi
kuzima na unaweza kuungwa kwenye kompyuta zaidi ya trilioni duniani. Lakini kwa
kuwa Marekani ni wa binafsi na wanataka SGT uwe wao, wakaamua kuwapa FBI ili
wautafute mtambo ulioibwa na Gunner.
Sifa nyingine ya hatari
kuhusu SGT, unaweza kuangamiza eneo ambalo wanalishuku linawaharifu. Inamvuto
wa hatari ambao umetengezwa kwa madini ya Uranium. Mvuto huo upo kama sumaku au
nguvu ya ukinzani, ukichomoka, huwa kama upepo na sifa yake huaribu kwa kulipua
eneo zima lililotakiwa kuharibiwa.
Sifa mbaya ya Ant-SGT,
mtambo uwezao kuufatilia SGT mahala ulipo, wenyewe huweza kung'amua SGT upo
wapi baada ya dakika tatu za mtambo huo kuwaka.
Tatizo hilo, kundi la
Gunner ulilitambua na ndio maana hakuwa na shaka sana kuhusu akifanyacho.
Boyka akaanza kubofya
vitufe vingi vilivyo kwenye kiparaza (keyboard) cha kompyuta yake
anayoitumia. Mara eneo la nje ya jumba
lile kukasikika mtikisiko mkubwa ambao unafanana na tetemeko la ardhi.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment