NIENDE WAPI? ‘’Dunia imenichukia’’
IMELETWA KWAKO NA SIMULIZI MIX ENTERTAINMENT
MWANDISHI ZUBERY RAZUUR MAVUGO.
SEHEMU YA KUMI.
ILIPOISHIA:
Uvumilivu ulimshinda mtoto yule, yaani
hajaiba cha mtu halafu anaumizwa namna ile kwanini hasa? Hapo akayachukuwa
macho yake mawili na kuyaangazisha chini, kisha akaanza kuyatembeza huku na
kule mpaka hapo alipofanikiwa kuliona jiwe lililokuwa limeshangaashangaa
mchangani, tabasamu lakujilazimisha likamtoka. Akalifuata jiwe lile kwa mwendo
wa upesi, hata alipoliokota kitendo bila hata kuuliza wala kuomba ushauri kwa
yeyote alilivurumisha jiwe lile hadi alipokuwa mwanamke yule.
ENDELEA.. ‘’ Yalaa! Mtumee! Nakufaa... Jamani
nakufaa...!’’ Mwanamke aliangua kilio cha namna ile baada ya jiwe kutua vyema
mkabala na jicho lake kitendo kilichompelekea apate maumivu ya haja. Hapo yule
mtoto amani ikamwingia, kitendo bila kuuliza akaianza safari ya kutimka eneo
lile na kukatiza wala asionekane na asijulikane wapi alielekea.
‘’ Wewe... Wewe kaka, simama tafadhali.’’
Binti ambaye muda wote alikuwa akimfuatilia, hakuhitaji kumwachia hata kidogo,
safari hii alipoona mbio za mtoto yule zimemshinda akaamua kumwita. Mtoto
Maduhu hakuhitaji hata kugeuka nyuma, nd’o kwanza aliongeza mwendo wa kukimbia,
mpaka hapo alipoisoma sauti ile vyema ndipo alipogeuka na kumgundua binti yule.
Akarejea kumfuata.
‘’ Hivi
wewe... Unanitafuta nini hasa?’’ Alisema.
‘’ Usiniulize maswali ya kipuuzi,’’ Binti
yule mwenye umri wa miaka kumi na mmoja alisema maneno yale. Wakati huohuo hata
bila kuuliza swali, aliuvua mtandio wake aliyokuwa kajifunga; mtandio ambao
aliununua kufuatia malipo ya mwezi wa awali aliyofanyia kazi. Akauchana bila
kuuhurumia na kuuchukuwa mkono wa Maduhu ambao ulikuwa na kidonda, akaustiri
mkono ule kwa kuufunga na mtandio ule huku yeye kichwani akibakiza kitambaa
kidogo pekee.
‘’ Kwanini umefanya hivi?’’ Maduhu alihoji
huku akiendelea kumwangalia binti yule kwa mshangao.
‘’ Kwasababu sipendi kumuona mtu akiwa
katika hali kama hii’’
‘’ Lakini sijakuomba msaada.’’
‘’ Kwani hata mimi nimetaka kukusaidia?’’
‘’ Donda sila kwangu?’ kwanini likutie
kiherehere’
‘’ Hata kama, ila mimi sipendi kutazamana
na watu wenye vidonda kama wewe’’
‘’ Sawa, kwakuwa sikukuomba, sina haja ya
kukushukuru ila siku moja nitakulipa gharama ya mtandio wako uliyoupoteza.’’
‘’ Nami naisubiri siku hiyo, andika deni
katika maisha yako.’’
‘’ Nitakupatia wapi?’’
‘’ Sihitaji kutafutwa, kwanza wachamie
niende zangu.’’
Binti yule alipomaliza kuyanena yale, hapo
akaianza safari ya kuondoka zake huku Maduhu akimshuhudia wala asijue amfuate
ama aendelee kuwepo eneo lile. Maswali mengi kichwani yalimuijia, akijiuliza,
huyo binti ana roho gani? Mbona ni yeye aliyeonesha msaada na si wengine. Ina
maana binti yule anawazidi mioyo watu wengi ndani ya jiji hilo? Lakini asipate
majibu.
Aliamua kuendelea na safari yake huku akiwaza
mambo yake binafsi kuliko kujishughulisha na jambo lile. Akiwa njiani kuelekea
asipopajua, alipita kwenye dumu la uchafu wa genge na kukuta ukoko umemwagwa,
hapo hata hakuuliza swali, akaukimbilia ukoko ule, hata alipoufikia alianza
kuula kwa pupa, baada ya hapo tumbo lake lilikuwa limejaa kiasi kwamba
alitamani asinzie tu na sikufanya chochote.
Usingizi ulimchukuwa pembezoni mwa genge
alilopatia mlo wake. Hapo akawa hajitambui tena ndani ya usingizi mzito huku
akiufidishia na ule wa siku iliyopita maana hakulala zaidi ya kushambuliwa na
mbu kituoni.
***
Siku
zilizidi kuyoyoma, hatimae ile siku ambayo bwana Mashaka alikuwa akiisubiria
kwa hamu iliwadia. Siku hiyo aliitwa na daktari kisha akaambiwa kuwa tayari
mkewe anaendelea vizuri na ruhusa ingetoka sikuhiyohiyo. Hapo akajionea fahari
haswa. Baada ya muda aliruhusiwa kwenda kumtazama mkewe, hakuamini kama mke
wake alikuwa akipumua vyema na kuongea vizuri, alimshukuru sana mola wake.
Hata pale daktari alipotoa ruhusa yake,
wallifurahi wote wawili na moja kwa moja wakatafuta usafiri wa taxi na kuelekea
nyumbani kwao.
Mashaka
hakuwa ndani ya nyumba ambayo alikuwepo awali, nyumba isiyo tamanika, isiyo
heshimika wala isiyolalika. Hivi sasa alikuwa ndani ya nyumba moja ya haja
ambayo alikuwa tayari ameilipia kodi ya miezi sita; nyumba yenye umeme, na kila
kitu cha kawaida.
‘’ Ha! Mume wangu? Upepatia wapi pesa za
kupaga kwenye nyumba nzuri kama hii? Nakumbuka mara ya mwisho tulikuwa tukilala
ndani ya kibanda tena chini... Vipi tena?’’ Mkewe alihoji.
‘’ Mke wangu, mwenyezi Mungu humpatia rizki
amtakae bila hata kumuhesabia... Wakati ukiwa hospitali hakika kichwa changu
kilivurugika sana. Nikalihisi kaburi langu likiniijia.’’
‘’ Sio wewe tu, hata mimi. Binafsi nilikuwa
nimeshakata tamaa, sikuwa na imani tena wala sikuwaza kama wewe utaweza yaokoa
tena maisha yangu... Nashukuru sana mume wangu.’’
‘’ Hata hivyo, niliamua kujivika ngozi ya
chui ilikuhakikisha yote yanatimia.’’
‘’ Una maana gani katika maneno yako?’’
‘’ Sina maana yoyote ile mke wangu, hebu
ingia chumbani kapumzike wachamie nitulie hapahapa sebuleni maana nimechoka
hatari.’’
Mashaka aliamua kujipumzisha sebuleni huku
akitazama runinga, akiwa usingizini mara ndoto moja kali ilimwijia. Akaota
anakimbizwa sana na mtu aliyeshikilia panga. Ingawa alijitahidi sana kukimbia,
lakini kamba ya kiatu chake ilimponza baada ya kujifungua na kumtega mguuni
kitendo kilichompelekea aweze kuanguka chini, hapo yule mtu mwenye panga
akamfikia. Alipomtazama sura hakuwa mwingine bali ni yule mtoto kwa jina la
Maduhu.
‘’ Unajua ninateseka kwa kiasi gani mpaka
hivi sasa? Ina maana uliamua kuniibia pesa zangu na kumfaidisha mkeo huku
ukifaharika kwa kupata mtaji pamoja na kodi ya nyumba eh! Sasa leo nakuua ili
ukayahisi maumivu yangu huko kuzimu’’ Mtoto Maduhu baada ya kutamka maneno
yale, hapo akalichukuwa panga na kuamua lizamisha mwilini mwa bwana Mashaka.
Kitendo kile kiliweza kumfanya apige makelele. Hapo akashtuka ghafla huku bado
ukelele ukimalizia kumtoka.
‘’ Nini tena mume wangu? Mbona unanishtua
wakati nimejipumzikia chumbani?’’ Mkewe alihoji baada ya kutoka chumbani mwake
mbiombio.
‘’ Ah! Hakuna kitu, ni ndoto tu.’’ Mashaka
alijibu huku akiwa katika hali ya woga.
‘’ Ndoto? Mchana huu?’’ Mkewe alisaili.
‘’ Hata mimi ninashangaa...!’’
‘’ Mh! Haya nieleze umeota nini hicho
kilichokufanya uwe katika hali hiyo na kupiga makelele hovyo.’’
‘’ Hakuna kitu mke wangu... Wala usijali.’’
Hata hivyo Mashaka alimficha mkewe ndoto
aliyoiota. Hapo akatoka nje na kwenda zake kwa ajili ya kulitafakari jambo lile
kiundani na kuangalia kama lina ukweli ama ni ndoto tu.
Akiwa katika tafakari mara alisikia simu
yake ikiita.
‘’ Eh!
Haloo... Ule mzigo tayari umeshafika, ni wewe tu tunayekusubiri mpaka hivi
sasa.’’
‘’ Basi sawa nakuja muda simrefu.’’
‘’ Sawa usichelewe.’’
Mashaka
baada ya kupokea simu ile akajikuta mawazo yote yakimwisha na moja kwa moja
akamfuata mkewe kisha akamwachia kiasi cha shilingi elfu kumi. ‘’ Nunua
chochote ule, bado sijanunua jiko na vyombo vya kupikia... Kuna sehemu naelekea
nitaporejea tutaongea zaidi.’’
Alipoagana na mkewe akatoka, na moja kwa moja
akaelekea kwenye kituo cha daladala, hata alipofika alipanda magari yaelekeayo
mjini. Yalimtua na yeye akaanza safari ya kulifuata soko kuu. Alipofika ndani
ya soko hilo alielekea upande wa wauzaji wa kuku na moja kwa moja akawafuata
mabwana watatu waliyokuwa wamesimama pembeni kidogo, akawasalimu na wao wakamwitika kama kwamba wanafahamiananaye
kisha, wakamlaumu kwa kuchelewa, alizikubali lawama zile na mazungumzo
yakaanza.
ITAENDELEA.
KWENDA SEHEMU YA KUMI NA MOJA BOFYA HAPA=> SEHEMU YA KUMI NA MOJA
0 comments:
Post a Comment