NIENDE WAPI? ‘’Dunia imenichukia’’
IMELETWA KWAKO NA SIMULIZI MIX ENTERTAINMENT
MWANDISHI ZUBERY RAZUUR MAVUGO.
SEHEMU YA SITA.
ILIPOISHIA:
Siku
iliyofuata, mtoto Maduhu akiwa kama mmiliki halali wa nyumba ile aliyoachiwa na
wazazi wake. Hakuhitaji ushauri kutoka kwa yeyote aliyemzidi umri. Alitangaza
mnada wa nyumba ile ambayo nd’o urithi wa pekee alioachiwa na wazazi wake.
Kipindi cha nyuma baba Maduhu alipopata kiasi fulani cha pesa, aliamua kununua
kiwanja na kujenga nyumba ile kwa ajili ya yeye na familia yake waweze
kujistiri lakini leo hii mwanae shida zimemjaa na kuona njia pekee ya kutatua
matatizo yake ni kuuza nyumba. Mshauri mkuu akiwa ni tumbo lake.
ENDELEA... Mnada ulikuwa mnada, watu wakanadika. Madau
mbalimbali yakapandiliwa kutokana na
kwamba kiwanja kile kilikuwa kikubwa na licha ya ukubwa wake vilevile kilikuwa
eneo zuri la mjini huku sehemu ile ikiwa njema kwa biashara.
‘’ Haya, huyu
amesema milioni moja na laki tano... Wapi mwingine?’’ wakatokea wengi tu. Hapo
dalali akaendelea kupandisha dau huku moyoni mwa Maduhu akifurahi na kuuambia
kimoyomoyo umasikini kwa heri. Alijiwazia mwenyewe endapo angepata pesa hizo
basi tatizo la chakula lingemwisha na milele asingehangaika kabisa, huku mawazo
yake yakiwa ni kutafuta biashara ya aina yoyote ile iliaweze kuifanya
itakayompelekea asiwe na matatizo. Ngawa alikuwa mdogo lakini alitambua mengi,
ni wazi kabisa, baba yao alikuwa ni mtu mwenye mitazamo chanya na aliwajenga
watoto wake katika misingi ya utafutaji ingawa walikuwa bado wadogo.
Wenye malengo na
kununua kiwanja kile kilichokuwa na nyumba mbovu waliendelea kupanda madau yao.
Hakuna aliyekubali kuzidiwa dau hata kidogo, wakifikiria ni jinsi gani kiwanja
kile kinaweza kuwaingizia fedha nyingi sana endapo wakijenga na kuanzisha
biashara zao eneo lile. Hapo dalali akafika kwenye milioni tano na nusu.
‘’... Tano
na nusu mara ya pili, nani anapanda dau? Tano na nusu mara ya tatu? Nne, tano?
Sita? Saba? Nane? Tisa? Kumi?’’ Hakuna hata mmoja aliyeonekana kunyoosha mkono,
isipokuwa mmoja tu. Dalali akamtangaza mtu yule kuwa yeye nd’o ameibuka
kujinyakulia kiwanja kile.
Maduhu
alifurahi sana, binafsi hakuwaza katika maisha yake kama ipo siku angeweza
kumiliki hata laki moja. Leo kupitia nyumba ya wazaz wake anasikia wazi kabisa
kuwa, muda si mwingi atamiliki mamilioni. Alijiona tajiri ghafla. Kabla hata
hajazitia mikononi pesa zile alimshukuru sana Mungu.
‘’ Ebwana eh! Mimi pesa zangu zipo
nyumbani... Sasa sijui twedeni mkachukuwe moja kwa moja? ‘’
‘’Eh! Twende hata sasa?’’ Maduhu aliwahi.
‘’ Wewe Maduhu, tulia.. Huruhusiwi kuongea,
muongeaji ni mimi hapa.’’ Dalali alisema kisha akaongeza, ‘’ Kwenda nyumbani
kwako hatuwezi. Si jambo zuri kumchukuwa mwenye kiti wa kitongoji mpaka mtaa
unaoishi wewe. Unachotakiwa ni wewe kuja hapahapa ama tutafute sehemu tulivu
kwa ajili ya jambo hili.’’
‘’ Oh! Sawa, basi ondoeni mashaka... Kwakuwa
mimi hiki kiwanja nimekipenda sana, lazma nirudi... Wacha nikafuate pesa kisha
nakuja hapahapa.’’
Wakakubaliana. Lakini jambo lile kwa Maduhu
aliona ni kama Dalali msumbufu tu, iweje jambo la watu kupeana pesa lichukuwe
hatua nyingi kiasi hicho? Lakini hakuwa na namna kwa vile tayari
alishakubaliananae.
Wakabaki wamemsubiri yule mteja wao.
***
‘’ Mke
wako hawezi kufanyiwa uparesheni bila wewe kutoa hizo pesa... Halafu ni muda
mchache umebaki, ukizidisha sana unaweza kumpoteza.’’
‘’ Dokta? Ina maana hakuna njia nyingine ya
kumsaidia? Tafadhali naomba unisaidie nikiwa kama mwanaume mwenzako. Nampenda
sana mke wangu dokta. Nisaidie, nimejitahidi sana lakini nimeishia kupata
shilingi elfu themanini. Tafadhali naomba msaada wako, mie hayo mamilioni kwa
sasa sina uwezo wa kuyapata dokta?’’
‘’ Kiukweli bwana Mashaka, hapo sina njia ya
kukusaidia. Hakuna namna, wewe leta hicho kiasi cha pesa ulichoambiwa,
ilkituyaokoe maisha ya mwanao hivi sasa.’’
Hakuwa na jinsi bwana yule kwa jina la
Mashaka. Ni siku kadhaa tangu afukuzwe kazi kutokana na tuhuma ya upoteaji wa
pesa katika kitengo alichokuwa akikisimamia ndani ya kampuni moja alilokuwa
akifanyia kazi.
Muda
huo hakuwa pesa, kila alipojitahidi kutembea kwa watu wake wa karibu na wao ni
kama walimtenga wala wasiwaze kunisaidia hata kidogo. Kila akifikiria ni kipi
hata angeweza kuuza ambacho kipo mikononi mwake, aliishia kukosa, ni bora hapo
nyuma wakati akiwa na nyumba yake kubwa yenye kila kitu, kipindi hicho akiitwa
bosi, kila sehemu yeye na suti. Si hivi sasa baada ya nyumba yake ya haja
kupigwa mnada na kampuni alilokuwa akifanyia kazi, huku magari yake yote mawili
yakiuzwa kwa bei ya kawaida ilimradi kampuni iokoe pesa zake ilizopoteza
kitendo kilichompelekea apoteze kabisa mwelekeo wa maisha yake binafsi, asijue
nini afanye.
Hivi sasa aliamua kutoka ndani ya hospitali
ile kubwa ya Bugando, hospitali ambayo hapo awali alikuwa akiifuata huku akiwa
na usafiri wa gari, lakini kwa sasa alikuwa yeye pamoja na miguu yake.
Hakuhitaji hata kumtazama mkewe ambaye hali yake ilikuwa hairidhishi. Machozi
yalimtoka kwa wingi mtu mzima yule, akifikiria ni jinsi gani angeweza kuzipata
hizo milioni mbili kwa ajili ya kuyaokoa maisha ya mkewe.
Akapanda usafiri wa daladala baada ya kugundua
kumbe mfukoni alikuwa na shilingi mia nane. Daladala ilipofika mjini alishuka
na kuendelea na safari yake asijue wapi anaelekea. Akiwa njiani aliamua
kuingiza mikono yake ndani ya mifuko ya suruali, hapo akakumbwa na mshangao
kidogo.
‘’ Ina maana sijalipia daladala? Mbona konda
hakunidai?’’ Akajicheka na kuamini kweli hakuwa katika hali ya kawaida, huku
akiwaza, ni vipi konda amemruhusu kuondoka bila kulipia wakati yeye awajuavyo
makonda, hakuna konda wa namna hiyo.
Akiwa maeneo fulani mara aliweza kuliona
gari moja la haja likipaki. Kisha akateremka bwana mmoja aliyefuatiwa na
mabwana wawili, mkononi bwana yule alikuwa ameshikilia mkoba. Hakuwajali,
akatamani kuendelea na safari zake, akiwa katika hatua mara alisikia.
‘’ Ila hizi pesa ni chache sana kwa kiwanja
kama kile, lakini wacha tukakinunue tu. Halafu yule mtoto anaonekana ana njaa
sana.’’
‘’ Bila shaka kile kiwanja ni cha urithi...
Sasa mtoto huyo pesa atapeleka wapi?’’
‘’ Atajua yeye mwenyewe maana sisi hatuwezi
kujua.’’
Maongezi ya mabwana wale watatu yaliendelea na
kuyavutia masikio ya bwana Mashaka.
Hapohapo kwa harakaharaka bwana Mashaka
akajikuta akipata wazo fulani ambalo liliikimbilia akili yake.
‘’ Milioni tano na nusu? Mungu wangu! Yaani
mimi nina hangaikia milioni tatu. Ha! Tena mtoto mdogo? Hebu ngoja
niwafuatilie.’’ Aliongea taratibu sana kiasi cha kujisikia yeye mwenyewe, kisha
akaanza kuwafuata mabwana wale.
Walifika kwenye kiwanja kimoja kikubwa ambacho
kilikuwa na nyumba ndogo isiyotamanisha. Nje ya nyumba ile macho ya bwana
Mashaka yaliweza kuwashuhudia watu wa tatu wengine huku mmoja kati ya watatu
wale akiwa ni mtoto mdogo.
Hakuwa mjinga kiasi cha kutojua kamba; mtoto
yule kama ni muhusika basi wale wengine mmoja kati yao angekuwa bwana
aliyemtafutia wateja huku mwingie akiwa kiongozi wa eneo lile. Mabwana wale
watatu wakaingia ndani ya nyumba ile yeye akiwa nje huku hatua moja baada ya
nyingine akiisoma.
Eh! Mungu wagu, nadhani unayatambua matatizo
yangu tena kuliko hata mimi. Nakuomba nisaidie hizi pesa zote ziingie mikononi
mwangu. Tazama, endapo nitazikosa bila shaka mke wangu atapoteza maisha
nakuomba mwenyezi Mungu naomba unihurumie mimi. Najua pengine hii ni njia ya
wewe kuniokoa hivyo naomba pia unisimamie. Bwana Mashaka aliongea maneno yale
huku akiwa amejibanza sehemu, akifuatilia kila kilichokuwa kikiendelea. Mate
yakitamani kumtoka, moyo ukimwenda mbio, hakuna alichokuwa akikifikiria zaidi
ya kuokoa maisha ya mke wake.
ITAENDELEA.
KWENDA SEHEMU YA SABA BOFYA HAPA>> SEHEMU YA SABA
0 comments:
Post a Comment