Friday, July 7, 2017


DUKA LA ROHOSEHEMU YA KUMI NA TATU
IMELETWA KWAKO NA SIMULIZI MIX ENTERTAINMENT
MWANDISHI FRANK MASAI

ILIPOISHIA
Sijui alitumwa na nani kunichunguza. Akakosea akagusa pasipogusika. Nikampa roho yake Lobo. Na Lobo hafanyi makosa, akampa masaa. Akashindwa kutimiza kuachia madaraka na kuondoka nchini. Roho yake ikawa yetu baada ya kushindwa kuinunua." Gunner alizidi kumtisha Lisa ambaye alikuwa anatetemeka kama mwenye ugonjwa wa tetenasi.
ENDELEA
Gunner akazidi kushuka chini ya mwili wa Lisa. Akafika kwenye kitovu chake na kuanza kukifikicha kwa chati na kumfanya Lisa azidi kutetemeka lakini kwa kujisikilizia.
Gunner akaenda mbali zaidi na kuingiza mkono wake ndani ya sketi matata aliyovaa Lisa. Akaanza kuukita mkono wake ndani zaidi.
Kwa mwanamke anayejiheshimu na kujitambua, hiyo ni dharau isiyo na kifani. Na Lisa alitambua hilo. Kwa nguvu zake zote, akazitumia kumsukuma Gunner kutoka kwenye maungo yake.
Gunner kweli aliyumba na ilikuwa kidogo adondoke.
Wakati Gunner akitafuta balansi kutokana na ule msukumo, Lisa tayari alishajiachia kwa kuruka juu kidogo akiwa tayari kwa kumpa pigo la teke Gunner. Lakini bahati haikuwa yake, Gunner tayari alishamuona na teke la Lisa lilidakwa kiustadi na kisha akamrusha juu mwanamke yule ambaye naye alikubali hali ile. Mwisho wake ulikuwa ni kutua kwenye meza ya kioo iliyokuwapo sebuleni mle, ikavunjika vipande vipande.
Gunner tayari alikuwa kajaa gesi ya hasira. Akamfuata Lisa pale chini na kuanza kumpa kipigo cha haja. Ngumi zisizo na idadi zilipigwa katika uso wa Lisa. Gunner hakuishia hapo, akazidi kumsulubu yule mtoto wa kike.
Akamuinua na kumkwida blazia yake aliyokuwa kaivaa.
Ngumi nyingi za tumbo zikaanza kupigwa kwenda kwa Lisa. Mtoto wa kike akawa anakohoa pumzi nyingi zisizo na idadi. Akalegea na kuwa tayari kwa kifo au kwa lolote toka kwa Gunner.
"Nilikuwa naisubiri siku hii kwa hamu. Sasa imetimia. Nakuua kama nilivyomuua baba yako." Gunner aliongea hayo huku kamsukuma Lisa ukutani na kumkabia hapohapo hadi macho ya Lisa yakawa yanageuka na kuwa meupe. Hakika mwisho wa Lisa ulikuwa umewadia.
Ilikuwa ni kama ndoto ambayo Lisa alikuwa anaiota kila wakati ili itokee. Kama ni sala, basi yawezekana MUNGU aliijibu haraka kuliko sala zake zote ambazo kawahi kuzisali.
Gunner akiwa katika hatua za mwisho kummaliza Lisa kwa roba nzito aliyokuwa kamkaba, alishituka mlango wake ukifunguliwa na kabla hajakaa sawa alikutana na teke zito la kuzunguka kutoka kwa mvamizi huyo. Akiwa anayumbayumba kama mlevi, wakati huo kamuachia Lisa aliyekuwa anagaa gaa chini akikohoa kutokana na roba ya mumewe, akapokea teke lingine la kifuani na kumrusha hadi kwenye kochi lake. Akili ilikuwa haijakaa sawa kabisa kichwani kwa Gunner. Akijitahidi kuiweka sawa, anakutana na makonde mazito toka kwa mvamizi wake. Gunner ikabidi asaliti amri na kutulia pale kwenye kochi.
Na hiyo ndiyo ilikuwa pona yake. Yule mvamizi akaenda hadi kwa Lisa na kumuinua kwa kumkalisha katika sakafu ya sebule lao.
"Hahahaaa. Malocha Malingumu. Naona unajitahidi kuwalinda watu wako. Safi sana tena sana. Lakini kuna jambo moja ambalo hauwezi kutuzuia, Jumamosi hii, Rais wa Urusi tunamuangamiza. Itakuwa raha sana." Gunner aliongea huku meno yake yakiwa yamejaa damu
"Hayo hayatuhusu tena. Ni kazi ya watu wengine. Go to hell Gunner." Malocha akampiga teke la kisogoni Gunner na hapohapo fahamu za yule bwana zikamtoka.
Malocha haraka akamnyanyua Lisa na kuanza kutoka naye nje. Akaenda upande mwingine wa gari lake na kumpakiza Lisa aliyekuwa bado hajarudiwa na nguvu zake kama kawaida. Akampakiza nafasi ya mbele karibu na dereva kisha yeye akazunguka upande wa dereva na kutaka kuingia kwa ajili ya kuondoka. Lakini ni kama aliyekuwa kasahau kitu, akatoka haraka garini na kutaka kwenda ndani kwa Gunner ili amchukue.
Lakini kabla hajafanya hayo, yaani hata hajafunga mlango wa gari lake, ilitokea pikipiki moja kubwa kiasi na mtu ambaye alikuwa kavalia kofia maalumu ya kuendeshea pikipiki, alitoa bunduki aina ya SMG na kuanza 'kumwaga njugu' kwenda kwenye gari la Malocha. Zaidi alikuwa anavamia upande wa Lisa ambaye aliingia chini ya uvungu baada ya kuona hali ile.
Malocha naye alichutama huku akiwa makini kutokana na risasi ambazo zilikuwa zinamwagwa bila mpangilio.
Baada ya sekunde kadhaa ya patashika kutoka kwa yule mtu mwenye pikipiki, risasi zikamuishia na alikuwa anaikoki tena kwa ajili ya kuendeleza 'tifu' alilolianza. Lakini kitendo cha kumaliza risasi, kikawa ni nafasi kubwa kwa Malocha ambaye alitoka eneo alilokuwa kajificha na kwa haraka akapanda juu ya boneti ya gari lake, na kwa ustaha wa ajabu, akaruka huku katanguliza mguu. Na mguu huo ukamkuta yule mwenye pikipiki na kumrusha pembeni ya pikipiki yake huku bunduki yake akiitupa pembeni kabisa na yeye.
Wakati anajiuliza akiwa chini, Malocha alishafika na kumtwanga teke zito la kidevuni kama vile mpira na kuifanya kofia ya pikipiki kumvuka.
Nywele ndefu zikavurugika na kupepea hewani baada ya kofia lile kuvuuka.
"Ooh! Ni Zakia. Nadhani mwisho wako unaishia hapa leo. Umekutana na Israel mtoa roho, mbwa jike wee." Malocha hakuwa na maneno mengi mdomoni mwake, akakimbia kwa mwendo wa hatua za karibu~karibu lakini za haraka na Zakia bila kutambua, alikuta mtoto wa kiume yupo naye uso kwa uso.
Ngumi za haraka toka kwa Malocha zilitiririka kwenda usoni kwa Zakia kabla hajamalizia kwa ngumi nyingine nzito ya kidevu iliyomrusha yule mwanamke hadi karibu na bunduki yake. Zakia kwa haraka akaishika bunduki yake tayari kwa kuinyanyua, lakini haraka yake haikuwa kitu mbele ya kasi ya Malocha.
Tayari mwanaume alikuwa kafika na kuikanyaga ile bunduki. Zakia akashangaa kuona kiatu kizuri cha harusi kikiwa kimekanyaga bunduki yake. Akaangalia juu na kumshuhudia dume la mbegu likiwa ndani ya suti mwanana kana kwamba yupo harusini, na kumbe mapambanoni.
Teke lingine la kidevu likatua kwa Zakia na kumsukuma hadi kwenye gari la Malocha ambalo alikuwa kaliharibu kwa risasi zake.
Zakia akasimama tayari kwa mpambano wa ana kwa ana maana mbinu za kuchukua silaha yake zilishindikana. Akawa kakunja ngumi tayari kwa mpambano mkali. Lakini kwa bahati mbaya alikuwa kasimama karibu na mlango wa gari la Malocha ambapo Lisa alikuwa sehemu hiyo.
Na Lisa hakufanya kosa la kipumbavu kama wengi wanavyodhani. Kwa nguvu zake za kike, akausukuma ule mlango na kumkumba Zakia ambaye alipiga yowe la maumivu na kusukumika mbele ambapo Malocha alikuwepo. Hapo naye Malocha aliruka teke zito likamkuta yule mwanamke kwenye shingo na kumgongesha tena kwenye mlango wa gari. Zakia akiwa kakubali yaishe, Malocha ndio kwanza alikuwa kafunguliiwa.
Akamfata palepale na kuanza kumpa ngumi nyingi zilizoanzia kwenye tumbo zikafata kifuani, shingoni na kumalizikia kwenye paji la uso ambapo ngumi ile ilimfanya Zakia ajigonge kisogo kwenye gari la Malocha.
Damu zikaruka kama kuku aliyechinjwa, lakini Malocha hakuona kama inatosha, akamdaka na kumkaba vilivyo Zakia na kilichofuata ni kumvunja shingo mwanamke yule.
"Shit." Malocha aliongea neno hilo huku akitema mate pembeni baada ya kuuacha mwili wa Zakia ukiwa hauna uhai tena.
"R. I. P Zakia." Sauti ya Lisa ilisikika nayo, huku akifungua mlango wa gari yao iliyoshambuliwa.
"Tuondoke hapa haraka Lisa." Malocha aliongea hayo huku akiifuata ile pikipiki ya Zakia na kuiwasha. Lisa ambaye alikuwa karudiwa na nguvu, naye akaenda na kukwea nyuma ya pikipiki hiyo.
Lisa akaangalia maskani yake kwa mara ya mwisho, hapo akamuona Gunner akitoka nje ya nyumba yao na macho yake yakaenda kwenye gari la Malocha. Akakimbia na ghafla alikuwa kama kaishiwa nguvu baada ya kuuona mwili wa Zakia ukiwa hauna uhai.

Gunner akaufuata ule mwili na kisha kwa uchungu akaupakata na kulia kwa sauti ya juu. Wakati huo pikipiki inayoendeshwa na Malocha, ilishatimua vumbi na kuacha tafulani pale mtaani.

ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment