NIENDEWAPI? ‘’ Dunia inanichukia’’
IMELETWA KWAKO NA SIMULIZI MIX ENTERTAINMENT
MWANDISHI:
ZUBERY RAZUUR MAVUGO.
SEHEMU YA KUMI NA MBILI.
ILIPOISHIA:
Baada ya maneno hayo machache akatoka
ndani ya duka lile la simu na kuelekea kwa jamaa yake mmoja mrusha miziki.
Wakasalimiana kwa salamu zao kisha akamwelezea kuhusu simu ile na kumwambia
endapo atamtoa shilingi elfu ishirini tu basi kila kitu watakuwa wamemaliza.
Rafiki yake yule hakutaka hata kuuheshimu uzuri wa simu ile, hapo badala aombe,
yeye akashusha bei na kung’ang’ana apewe kwa shilingi elfu kumi simu ile ya
laki na nusu.
ENDELEA... ‘’ Ah!
Ndinga, ina maana hata huoni kitu kilivyo kikali hiki? Kiukweli kwa kumi
sifanyi... Yaani dude la laki na nusu wewe ulichukuwe kwa kumi?’’
‘’ Basi kama
hutaki acha... Ila kumbuka mimi nakulinda kishkaji, sawa dude la pei ndefu ila
kama kutatokea chochote unadhani wa kwanza kukamatwa ni nani? Si mimi
mnunuzi.’’
‘’ Kwahiyo
ndinga langu kumbe nimeyaweka maisha yangu lehani kwa ajili ya elfu kumi eh!’’
‘’ We
kimavi nini? Sasa pigo gani unaniletea... Kama hutaki sepa, sio unaanza
majungu. Mbona hata mimi ninayaweka maisha yangu hatarini kwakununua kitu cha
wizi. Wakija ulowaibia na kunikamata? Hebu tembea, tafuta washkaji wengine
ndinga.’’
Hata hivyo wawili wale kuzungumza mazungumzo
yaliyojaza lugha za kihuni, walifikia muafaka baada ya Maduhu kuikubali pesa
ile kwani alikuwa na njaa sana.
Hata alipopatiwa ile pesa, alielekea kwenye
moja kati ya magenge yaliyokaribunae hapo akaingia na kuagiza chakula
alichokuwa akihitaji, baada ya hapo alikula na kuanza elekea sehemu ambayo
huutafuta usingizi wake kwani usiku ulikuwa umeshafika muda.
Alitembea hadi kwenye nyumba moja
isiyopendeza; nyumba ambayo ukiitazama kwa nje basi unauwezo wa kuviona vilivyo
hifadhiwa ndani bila wasiwasi wa aina yoyote. Aliingia na kutandika sandarusi
kisha akaanza kuutafuta usingizi wake.
***
Siku hiyo bwana
Mashaka alichelewa kidogo kuamka, hiyo ni kutokana na usiku wa jana
kuusherehekea akiwa na mke wake, wakikumbushana mengi ya kimiili ambayo
walikuwa wameyakosa kwa kitambo. Hata alipoamka bado alikuwa juu ya kitanda
huku akiupa sifa mbalimbali usiku wa jana kimoyomoyo. Baada ya kukaa sana juu
ya kitanda hivi sasa aliamua kuamka na kuelekea moja kwa moja msalani,
alipotoka huko alifanya hatua zote za kuusafisha mwili wake.Wakati akifanya
yote hayo, tayari mkewe alikua kisha amka zamani wakati huo alikuwa akifanya
kazi nyingine za asubuhi, bila kusahau upishi kwani jiko kwa ajili ya kupikia
aliletewa siku iliyopita na mume wake pindi aliporudi kutoka mihangaikoni.
Baada ya Mashaka
kumaliza vyote alivyokuwa akivifanya, tayari alikuta mkewe ameshamaliza upishi
wa chai. Akakaribishwa chai na kunywa, baada ya hapo aliaga. Moja kwa moja
akaianza safari ya kuelekea mjini ambako ndiko biashara zake za uuzaji kuku
alipozianzishia.
Hata daladala
ilipomtua, nje kidogo ya soko kuu baada ya kumaliza kulipia. Aliamua kuelekea
moja kwa moja hadi ndani ya soko. Alipofika kazini alianza harakati zote na
kufanya mambo yote yaliyohusiana na kazi yake.
Wateja
waliendelea kumiminika na kumfuata yeye kutokana na jinsi alivyojua kuwajali
kwa kauli zilizo hifadhi maneno matamu kama sukari, kitendo kilichoanza
kuwakera wenzie waliyokuwa karibunae wakifanyanae biashara moja. Kwakuwa yeye
ni mzoefu wa biashara ile, aliligundua jambo hilo lakini hakutaka alijali maana
alitambua mambo kama hayo huwa hayaepukiki hata kidogo.
Saa tisa alasiri
kiu kililisumbua koromeo lake ipaswavyo huku njaa ikiliadhibu tumbo lake kana
kwamba alitoka nyumbani kwake bila kupata chai nzito kutoka kwa mkewe. Ilibidi
avumilie kwani bado wateja alikuwanao lakini baada ya muda kidogo aliamua
kutoka kwa ajili ya kuyatafuta magenge ya chakula ambayo yangeweza kumtatulia
shida ya tumbo lake.
Alipofika
magengeni alilifuata genge moja na kuagiza chakula. Wakati akiwa nje ananawa
mara alijikuta akisisimka mwili wake mzima, ni baada ya kuitazama sura ambayo
hakuwa ametarajia kuiona; haikuwa sura nyingine bali ni ya yuleyule mtoto
aliyewahi kumkaba na kumpora pesa ambazo zilimfanya apate mtaji na kuyaokoa
maisha ya mkewe. Ingawa alijua mtoto yule hakumuona siku ile lakini bado aliona
haya. Ajabu mtoto yule nae alikuwa akionekana kulifuata genge hilo.
‘’ Hata hivyo hanijui.’’ Mashaka alisema kisha
akaingia ndani ya genge na kukaa kisha akaanza kupata chakula alichokihitaji.
Wakati akipata chakula, mtoto yule kwa jina la Maduhu nae aliingia na kuketi
mkabala na sehemu aliyokuwa amekaa Mashaka. Amani ikamponyoka, akajikuta hali
kwa raha kabisa, mpaka mtoto Maduhu anamaliza kupata chakula chake, bado
Mashaka alikuwa hajakimaliza cha kwake.
Maduhu alitoka ndani ya genge lile na kulipia
kiasi cha pesa alichokuwa akidaiwa kisha akaianza safari ya kuondoka eneo lile.
Hapo kidogo Mashaka akajikuta akipumua kwa amani.
Wakati hata kabla Maduhu hajafika mbali
kutoka eneo lile, mabwana wawili waliweza kumuona na kumtambua. Ni yeye
aliyemuiba mmoja kati yao saa ya mkononi pindi alipotoka kuinunua siku mbili
zilizopita. Hawakutaka kumchelewesha baada tu ya kumuona hapohapo wakampigia
mwano.
Mtumee!
Wananchi weye hasira kali, wenye kuujua
uchungu wakuibiwa, wale ambao walisha apa katika maisha yao watakuwa radhi
kuhakikisha wanawaondoa wote wenye kuiba vya watu ndani ya dunia hii.
Walimfuata kijana yule huku wakiwa wameshikilia vya kushikiliwa na visivyo vya
kushikiliwa, huku wengine kutokana na hamu ya kupiga mwizi wakijikuta hata
wakisahau kushikilia vifaa vyovyote, badala yake wakajikuta wakienda hivyohivyo
na ngumi zao.
Hata walipomfikia mtoto yule ambaye na yeye
aliposikia neno ‘mwizi’ hakuuliza na kuanza kukimbia, hawakumtaka maelezo.
Hakuna hata mmoja aliyeuhurumia umri wa mtoto
yule mdogo, waliyompata walimpa kipigo cha haja; kipigo ambacho hupigwa mbwa asiye
na kwao, mbwa mwenye kurandaranda mtaani kila muda. Ndani ya dakika moja tayari
mtoto yule alikuwa chini huku damu zikimchuruzika maeneo mbalimbali ya mwili
wake, akijililia tu, lakini hiyo isiwe sababu ya yeye kuachwa na watu wale
wenye hasira kali.
Sauti
zile ziliweza kupenya hadi ndani ya ngoma za masikio ya mlaji mmoja kwa jina la
Mashaka, aliyekuwa gengeni akiendelea kukishughulikia chakula. Hakuzijali sauti
zile kwani ndani ya jiji hilo kubwa ni jambo la kawaida, mtu ama watu kuibiwa
na kukamata mwizi kisha kupiga hadi kuua endapo nafasi hiyo ikipatikana.
Hata hivyo alimaliza chakula chake vyema na
hivi sasa alilipa gengeni kisha akaanza kuondoka zake. Alipolifikia eneo la
tukio, hakutamani walau kwenda kumtazama mwizi yule aliyekuwa akipigwa kwani
endapo angeenda kwa ajili hiyo bila shaka nae angetaka kumpiga tu.
Chakushangaza.
Moyo ulimtuma aende walau kumtazama mwizi yule ambaye alitarajiwa kuuacha uhai
wake muda mfupi ujao kutokana na kipigo alichoendelea kukipata kutoka kwa raia.
Alipofika,
alisukumana na mabwana waliyokuwa wamezunguka eneo lile kisha akafanikiwa
kumwona mwizi yule. Kwa mara nyingine mwili mzima ulimsisimka, baada ya kumwona
mtoto aliyekuwa amevalia mavazi kama yale ya yule aliyekula nae, tofauti
ilikuwa ni kwamba; yule mtoto aliyekuwa naye gengeni yeye hakuwa na damu
mwilini ila huyo aliye hapo chini huku akipata kipigo yeye alikuwa na damu
nyingi mwilini mwake. Moyo wa kutamani kumsaidia mtoto yule ukamwijia maana
aliamini hata kipigo anachokipata mtoto yule kilifaa akipate yeye kwani ndiye
msababishaji wa maisha ya namna ile kwa mtoto yule.
Akawaza mbinu gani aitumie ilikuwashawishi
raia waweze kumwacha mtoto yule, akiwa katika hali ya kuumiza kichwa, ndipo
hapo wazo kuu lilipoichukuwa akili yake.
‘’ Jamani polisi wanakuja, tukimbieni,
tusije kamatwa.’’ Aliropoka, sauti yake ilisikika na hivi sasa raia walimsahau
mwizi wao na kuanza kukimbia. Ndani ya sekunde kadhaa eneo lile lilibaki jeupe
halina mtu isipokuwa Mashaka pekee. Hapo akawa amefanikisha adhma yake, akawaza
nini afanye kwa mtoto huyo ambaye alikuwa amepigwa sana. Hakuona mtu yeyote
aliyeonesha kumjali, hivyo akaamua kulisimamia jambo lile zima mwenyewe.
ITAENDELEA.
KWENDA SEHEMU YA KUMI NA TATU BOFYA HAPA=>SEHEMU YA KUMI NA TATU
0 comments:
Post a Comment