NIENDE WAPI? ‘’Dunia imenichukia’’
IMELETWA KWAKO NA SIMULIZI MIX ENTERTAINMENT
MWANDISHI ZUBERY RAZUUR MAVUGO.
SEHEMU YA NANE.
ILIPOISHIA:
Hata hivyo, kila alipokumbuka umuhimu wa
maisha ya mkewe, hofu yote ilimwondoka. Akijisemea, ‘ Mungu anisamehe, maana
sijafanya vile kwa kupenda’ huku akiiombea siku mpya iweze kuingia na yeye
aelekee moja kwa moja hospitali kwa ajili ya kupeleka pesa na mkewe aanze
kufanyiwa uparesheni maana alikuwa katika hali mbaya sana. Alijing’ang’aniza
kuutafuta usingizi, ingawa hofu lilimchukuwa na kuutwaa usingizi wote lakini
baada ya muda pasina hata mwenyewe kujielewa alijikuta akisinzia.
ENDELEA... Jua
lilichomoza na kuurejesha ufahari wake katika dunia. Huyu na yule wakaonana kwa
umakini huku likileta ofa yake ya vitamini ndani ya dunia. Kuchomoza kwa jua
kulimpelekea bwana Mashaka atambuewazi kuwa tayari siku mpya ilikuwa imewadia.
Akanyanyuka kutoka juu ya godoro lake dhoofu, lisilo na kitanda, lakutandika
ardhini. Kisha akalifuata jagi moja ambalo kwa ndani lilikuwa limehifadhi maji.
Mswaki uliyotumika mpaka ukasema naomba usinitumie tena, nd’o huo aliyoufuata
tena bila haya, badala auwekee dawa yeye alichukuwa chumvi na kupakaa juu ya
mswaki ule kisha akaelekea kujisafisha.
Muda kidogo
alirejea ndani mwake, jicho la kwanza alilitupia kwenye mkoba uliyohifadhi
pesa. Akakenua meno yake baada yakuuona ukiwa juu ya godoro. Akaendelea na
mambo yake. Hata alipomaliza kila kitu, hapo aliuchukuwa mkoba ule kisha
akaufunua kwa ndani na kukutana na pesa za kumwaga. Hakuwa na muda wa
kuzihesabu bali alichojali ni kuhesabu pesa alizotakiwa kuzipeleka hospitali
kwa ajili ya kuyaokoa maisha ya mkewe.
Alipopata fungu
alilolihitaji, aliamua kuuficha mkoba ule ndani ya mfuko wa rambo ambao alikuwa
akiutumia kwa ajili ya kuhifadhia nguo zake, kisha akaondoka huku pesa zile
akiwa amezifunga kwenye kitambaa alichokikuta ndani mwake.
Usafiri
wa daladala ni kama aliuona utamchelewesha, ikabidi aite taksi.
‘’
Nipeleke Bugado hospitali... Fasta.’’ Alisema.
Sekunde kadhaa mbele
dereva aliwasha gari na kuianza safari ya kuelekea Bugando. Hawakuchukuwa muda
sana, tayari walikuwa wameshafika, akashuka na kumlipa dereva kiasi cha pesa
alichohitaji kisha kwa mwendo wa kuwahi akaichukuwa miguu yake hadi ndani ya
hospitali. Humo tena alichukuwa muda hadi kuonana na daktari, hata
alipoonananae aliongeanae kwa nyodo na maringo. Mwisho wa siku suala zima la
ukoaji wa maisha ya mkewe lilianza bila tabu wala wasiwasi.
Madaktari bingwa wa
upasuaji waliihifadhi miili yao ndani ya mavazi maalumu kwenye chumba cha upasuaji. Mwili wa mke wa Mashaka
ukiwa juu ya kitanda maalumu, huku madaktari wakifanya mambo ya kutisha juu ya
mwili wake na wala wasihofu chochote kile.
***
Mpaka majira ya saa
tano, mtoto Maduhu bado alikuwa ndani kafungiwa. Akiwa katika hali ya mchoko
haswa. Hakutaka kuamini kama ni yeye aliyelala usiku wa jana ndani mule.
Hakutaka kujikumbusha mateso aliyoyapata kulala katika nyumba ndogo iliyojaa
kila aina ya kinyaa, kuachilia mbali yeye kujikunyata juu ya mikojo mpaka
asubuhi, vilevile alishindwa kuwasahau mbu wenye roho mbaya kuliko hata
magaidi. Mbu wenye sifa za kuwinda zaidi hata ya simba wa nyikani. mbu wale
nd’o waliyomfanya usiku wa jana aufananishe na usiku wa kwanza wa jahanamu
yake.
Hata hivyo bado
alikuwa katika mawazo makali sana, ni vipi amewekwa rumande ilhali hana kosa
ama ndivyo sheria za nchi yake zilivyo? Alitamani aonane na mtaalamu wa maswala
ya sheria iliangalau aweze kukiomba hicho kifungu kinachoruhusu mambo hayo,
lakini tamaa zake zilikuwa ni sawa na bure.
Muda huohuo nd’o
muda aliyomuona afande mmoja akichungulia ndani ya chumba kile kupitia uwazi
mdogo; afande yule hakuongea chochote zaidi ya kufungua mlango na kumtazama
Maduhu kwa jicho la hasira.
‘’ Shikamoo...’’
Maduhu kama ilivyo kawaida yake ya kuheshimu wanaomzidi umri alisalimu. Afande
yule alimsikia lakini hakumwitika, Maduhu akabaki amemtumbulia macho afande
yule.
‘’ Mbona
unaniangalia utadhani unataka kunimeza..’’ Afande alisema kisha akaongeza, ‘’
Usinitazame namna hiyo mimi... Alaaa! ’’ huku rungu likitua mwilini mwa Maduhu.
Ingawa aliyapata
maumivu lakini hakulia, alibaki akijishika eneo aliloumia huku macho yake
safari hii akiyaweka chini.
Afande yule
akamchukuwa na kwenda kumpatia mavazi yake pamoja na viatu alivyokujanavyo siku
ya jana.
‘’ Leo
tena unakaribishwa uje kulala kama ukikosa pakulala.’’ Alisema hivyo na
kuwafanya maafande wenzie wabaki wakikenua meno yao . Wakamsifia na yeye kichwa
chake kikakua. Hapo Maduhu akaruhusiwa kuondoka.
***
Hata alipokuwa akielekea hakuwa akipajua, njaa
iliendelea kulisumbua tumbo lake pia. Hakujua ni wapi angeweza kupatia chakula.
Aliona sehemu pekee ni yeye kujipitisha katika maeneo mbalimbali yenye magenge.
‘’ Eeeeeh! Wewe, hebu toka hapa.’’ Mama mmoja
aliyekuwa akiuza genge, aliongea maneno hayo baada ya kumuona kijana yule.
‘’ Kwani nimekosea nini Mama... Mbona namimi
ni binadamu kama wengine?” Alijibu huku akijitazama katika hali yamshangao.
‘’ Bado husikii? Binadamu?! Hivi nanyie
machokoraa mnaubinadamu gani? Eh! Licha ya mimi kuwa mwema na kuwapatia ukoko
bado mnaniibia mpaka pesa zangu... Tena toka. Sina huruma nanyie hata kidogo,
panya mabaka ninyi.’’
Ingawa hakupenda kuitwa chokoraa lakini
hakuwa na jinsi, alikubaliana na jina lile. Taratibu akaanza kuondoka huku mama
yule akitoa maneno ya kashfa pasina kujua ni mateso gani kijana yule anayapitia
na ni kiasi gani utumbo wake unahitaji chakula.
Katika pitapita zake kama mpita njia mwenye
ndoto za kulikomboa tumbo lake, aliweza kupita kwenye genge jingine, huko
akashuhudia kitu cha ajabu. Ati, wali na mfupa wa nyama vinawekwa katika mfuko
wa kumwagia uchafu. Alimtazama mwanamke yule aliyeuweka wali ule kwa jicho la
shukurani, kisha taratibu akaanza kulifuata fuko lile la kuhifadhia uchafu kama
hataki.
Akiwa njiani mara ghafla aliweza kushangaa,
baada ya kumuona mbwa mmoja akiukimbilia mfuko ule huku ulimi wake ukiwa nje,
udenda ukimtoka kwa fujo; mbwa yule ambaye hata mwili wake mzima ulikuwa
umenyonyoka manyoya yake kutokana na kuyazoea maji ya moto aliyokuwa akimwagiwa
kila mara, bado hakuwa amekata tamaa, ingawa pia alikuwa amejawa na madonda
kutokana na kupigwa ovyo kitendo kilichompelekea aonekane dhohofulhali na
mwenye magonjwa ya kila aina. Aliufuata mfuko ule.
Mtoto mwenye njaa kali hakuhitaji kukubali
jambo lile litokee hata kidogo. Ni vipi angeweza kulinusuru tumbo lake dhidi ya
njaa kali aliyokuwanayo? Akaona njia pekee ni yeye kushindana na mbwa yule hadi
kukiwahi chakula.
Hapo
akakaza mwendo mpaka akaufikia mfuko ule wa chakula, lakini ni kama mbwanae
alikuwa ametambua kuwa, mtoto yule alihitaji kumuharibia rizki yake. Hakukubali
pia. Tayarinae alikuwa kaufikia mfuko ule.
Hata Maduhu alipoinua mikono yake na kuchukuwa
chakula; mbwanae alifanya hivyo kitendo kilichosababisha mfuko ule uliyokuwa
umebeba uchafu, umwagike chini.
Ha! Hapo ikawa kesi nyingine. Wakati Maduhu
akiparangana kuuokota mfuko ule iliaweze kutafuta wali wake, muda huohuo nd’o
muda aliyojikuta akitoa ukelele mkali sana. Baada ya kuyahisi maumivu ya maji
ya moto ambayo yalikuwa mwilini mwake. Hapo akabaki akilia.
‘’ Washenzi wakubwa nyie, kwanza nilikuwa
nawatafuta sana. Na bado, tena ngoja niongeze mengine.’’ Maneno hayo aliyatamka
mwanamke mmoja aliyeshikilia sufuria ambalo bila shaka lilikuwa na maji ya
moto.
‘’ Mondesta?’’
Mwanamke yule aliita.
Akaitika binti mmoja aliyekuwa akioshaosha
vyombo.
‘’
Niletee hayo maji kwa ajili ya kunyonyolea kuku nimuoneshe huyu mtoto wa mbwa,
naona yale hayajamwingia.’’ Mwanamke yule alisema, hapohapo binti aliyekuwa
akiosha vyombo aliachana navyo na moja kwa moja akachukuwa jagi kisha akachota
maji yaliyokuwa yameshaanza kupogoma na kumpelekea mwanamke yule.
Mtoto Maduhu alimshuhudia mwanamke yule
wakati anajiandaa kummwagia maji yale ya moto kwa mara nyingine. Hakukubali,
hapo akajing’ang’aniza kuamka chini alipokuwa akiugulia maumivu na hapo
akaianza safari ya kukimbia kuondoka eneo lile huku bado kilio cha maumivu
aliyokuwanayo kikiendlea kumtoka. Mwanamke yule hata alipoyamwaga maji yake
tayari alikuwa amechelewa kwani mtoto Maduhu alikuwa tayari ameshafika mbali
kidogo, kwa ajili ya kujinusuru na maji yale ya moto.
ITAENDELEA.
KWENDA SEHEMU YA TISA BOFYA HAPA>> SEHEMU YA TISA
0 comments:
Post a Comment