NIENDE WAPI? ‘’Dunia imenichukia’’
IMELETWA KWAKO NA SIMULIZI MIX ENTERTAINMENT
MWANDISHI:
ZUBERY RAZUUR MAVUGO.
SEHEMU YA TISA.
ILIPOISHIA:
Mtoto Maduhu alimshuhudia mwanamke yule
wakati anajiandaa kummwagia maji yale ya moto kwa mara nyingine. Hakukubali,
hapo akajing’ang’aniza kuamka chini alipokuwa akiugulia maumivu na hapo
akaianza safari ya kukimbia kuondoka eneo lile huku bado kilio cha maumivu
aliyokuwanayo kikiendlea kumtoka. Mwanamke yule hata alipoyamwaga maji yake
tayari alikuwa amechelewa kwani mtoto Maduhu alikuwa tayari ameshafika mbali
kidogo, kwa ajili ya kujinusuru na maji yale ya moto.
ENDELEA... ‘’ Mjinga mkubwa wewe, na unabahati...
Mnakuja hapa mnatuharibia siku. Nitawamaliza mimi.’’ Mwanamke yule alifoka
kisha akaachana na jambo lile na kuendelea na mambo yake mengine aliyokuwa
akiyafanya hapo awali.
Mtoto kwa jina
la Maduhu muda huu alikuwa kama kichaa. Alikimbia huku na kule pasina msaada.
Hakuna hata mmoja aliyemjali kila aliyemtazama barabarani aliishia kumlaani,
hata wale waliyotaka kuonesha huruma mbele yake, waliyokuwanao waliwasihi.
‘’ Hivi
wewe unawajua machokoraa ama unawasikia tu? Hapo ametoka kuiba nd’o maana
wamemliza.’’
‘’ Hata kama, lakini yeye pia ni binadamu
kama sisi... Vipi ateseke namna hiyo mama?’’
‘’ Wakati mwingine inabidi uitumie akili
yako vizuri. Chokoraa ni mtu ambaye maisha yake yote yanapatikana mtaani hao
nd’o majizi kama hujui. Ukisikia mtu kaibiwa sijui kabomolewa nyumba,
wanaohusika na maswala hayo ni wao. Wewe si umetoka kijijini? Hujui lolote hapa
mjini, ukishajangaa unaachwa kwenye mataa... Ukijifanya mama huruma, utakufa
njaa.’’
‘’Mh! Lakini mama...’’
‘’ Hivi wewe mbona mbishi sana? Ayaah...
Nimesahau chenji yangu kwa yule mchaga muuza nyama!’’
‘’ Sasa itakuwaje mama? Kama umeisahau.’’
‘’ Halafu kama unavyojua, hapa namuwahi
shoga yangu, bado yupo nyumbani ananisubiri.’’
‘’ Au tuiache tutaichukuwa siku nyingine?’’
‘’ He! Wewe... Ushaona nani anaacha hela?
Hela huwa zinasahauliwa, zikikumbukwa hufuatwa... Acha upuuzi.’’
‘’ Wachamie niifuate halafu wewe utangulie
nyumbani, tutakutana ama unaonaje?’’
‘’ Hautopotea kweli wakati wa kurudi?’’
‘’ Hapana, siwezi mama... Nimeshapakariri,
nikishuka na daladala, napandisha na kufika hapohapo.’’
Ni maongezi yaliyoibuka kutoka kwa mama mmoja
pamoja na mfanyakazi wake. Wawili wale walionekana kutoka ndani ya soko kuu
huku kila ishara zikionyeshawazi kuwa, walikuwa wametoka kuhemea mahitaji
fulani. Mfanyakazi wa mama yule hakuwa mkubwa, alikuwa ni binti tena mwenye
miaka kumi na mmoja.
Kama ambavyo walivyokuwa wameongea ndivyo
ilivyokuwa, mama yule alitangulia na mizigo hadi kwenye daladala huku akimwacha
binti yule akirudi sokoni kwa ajili ya kumtafuta mchaga muuza bucha iliaweze
kumpatia kiasi cha pesa ambacho bosi wake alikuwa amekisahau.
Alitembea huku akiangalia maeneo tofauti
tofauti. Ingawa hivi sasa alikuwa na miezi kama minne tangu aingie ndani ya
jiji lile la Mwanza kutoka kijijini kwao, lakini bado ushamba ulikuwa umemjaa
ndani ya kichwa chake, hiyo yote ni kutokana na kutoka mara moja moja ndani ya
nyumba aliyokuwa akiishi kitendo kilichompelekea ashindwe kulitambua vyema jiji
lile. Hata alipofika kwa Mangi, alifanya alichotakikana kukifanya na baada ya
hapo, hivi sasa alikuwa akielekea upande wa magari ambayo yangeweza kumfikisha
alipokuwa akiishi.
Akiwa katika mwendo wake mara ghafla mwili
ulimsisimka baada ya kusikia sauti za kilio cha kwikwi. Macho yakatamani yajue
ninini kilichokuwa kikitoa sauti zile? Kwa harakaharaka akagunduawazi kuwa,
mwenye kutoa sauti ile hakuwa mbali na eneo alilokuwepo yeye, hapo kupitia
masikio akajikuta akibaini kuwa, mtu yule aliyekuwa akitoa sauti zile
zenyekubeba kilio cha kwikwi alikuwa amejikalia pembezoni mwa barabara. Hata
alimpomtazama, hakuamini alichokiona.
Mtoto mdogo ambaye hata yeye anamzidi umri
alionekana akihangaika eneo lile. Jiraha kubwa mkononi alilokuwanalo,
lilioneshawazi kwamba halikuwa likimtania bali lilimuuma kwelikweli, lakini
hakuwa na chakufanya zaidi ya kulimwagia mchanga ilikuliziba dhidi ya nzi
waliyokuwa wakilitamani. Kitendo kile kilimpelekea binti yule afumbe macho yake
kadri alivyokuwa akilitazama jiraha lile ambalo lilikuwa likitiliwa mchanga na
mtoto mwenye kutoa kilio.
Huruma zake zikamfanya amsogelee mtoto yule
kwa ajili ya kumuhoji ni kipi hasa kilichompelekea akawa namna ile? Na vipi
watu wanapita kama hawamuoni ilhali yupo pembezoni mwa barabara?
‘’ Wewe kaka...’’ Aliita huku akimtazama
mtoto yule.
Mtoto akamtazama kwa jicho lilelile alilokuwa
akilitumia kumwaga machozi yake.
‘’ Nini?’’ aliitika kwa mtindo huo.
‘’ Ha! Kumbe wewe?’’ Ni kama binti yule
alimkumbuka mtoto mwenye kutoa kilio cha kwikwi baada tu yakumtazama sura.
‘’
Wewe nd’o nini? Na wewe unataka nini hapa?’’ Majibu ya mtoto yule
yalionesha kuwa ni mtu asiye na masihara hata kidogo.
‘’ Wewe si yule uliyekuwa ukikimbia kule
maeneo ya nje ya soko huku ukilia wewe?! Vipi, umepatwa na nini? Na mbona upo
katika hali hii?’’ Binti yule alihoji.
‘’ We mwanamke, hebu achana na mimi... Tena
sipendi mazoea na watu mie, nitakuharibu sasa hivi... Ala!’’ Alikoroma.
‘’ Hahahhaha... Kumbe ingawa unahitaji msaada
lakini bado ni ngangari, we mtoto ukoje?’’
‘’ Nani unamwita mtoto? Nitakuharibia sasa
hivi.’’ Mtoto yule akainuka na kushikilia jiwe lililokuwa karibu nae.
Akamtazama binti yule kwa hasira za wazi.
‘’ Unataka kunipiga? Nipige sasa? Kwani
unashindwa nini? Nipige si hata kwenu nd’o umefunzwa hivyo? Ina maana wewe ni binadamu wa aina gani usiye
na utu. Usojua kumjali mtu kistaarabu... nakuja kukujulia hali unataka
kuniponda jiwe haya ponda hilo jiwe lako tuone nini utafaidikanacho.’’ Binti
aliongea maneno ambayo kwa kiasi kikubwa yalimuingia mtoto yule. Hapo hasira
zikamjaa kifuani.
‘’ Sitaki matatizo na wewe.’’ Mtoto yule
akasema kisha bila kuaga akaanza kuondoka eneo lile. Binti hakutaka kukubali
kumwona mtoto kama yule ambaye anaoneshawazi matatizo yamemjaa akiwa katika
hali kama ile. Akajifikiria sana kisha akili ikamwambia, ‘Mfuate.’’ Binti yule
akaanza kumfuatilia mtoto yule nyumanyuma huku akisahau kuwa alikuwa na safari
ya kuelekea nyumbani kwao.
Akiwa nyuma ya mtoto yule ambaye alionekana
amemzidi kwa hatua kadhaa, aliweza kujifikiria sana. Ni vipi mtoto kama yule
mwenye sura ya kipole awe na maneno ya ghadhabu? Ama ukali wake nd’o sababu
mpaka muda huo hajaupata msaada wa aina yoyote kutoka kwa wapita njia? Na je,
vipi, hana hata huruma na jiraha lake mbona anakuwa katika hali hiyo? Fikra za
binti yule zikamkumbusha maneno ya bosi wake aliyezoea kumwita kwa jina la
mama. Akakumbuka wakati anajuzwa kuhusiana na hawa watoto kwa jina la
machokoraa jinsi ambavyo huwa walivyo, hapo akatamani akate tamaa kumfuatilia,
lakini akiwa katika hali ile mara akamsikia mtoto yule akiongea.
‘’ Wewe mama nd’o umenimwagia haya maji ya
moto hadi nikaumia hivi. Hebu ona ulivyoniunguza... Kwani mimi niikuwa na kosa
gani? Nilikuja kwenye hoteli yako kufanya vurugu hadi unimwagie? Ama mimi ni
mbwa?’’ Ni maneno yaliyotoka ndani ya kichwa cha mtoto yule kumfuata mwanamke
mmoja aliyekuwa amekaa kwenye moja kati ya magenge yaliyokuwa eneo lile. Hapo
yule binti akajikuta akivutiwa na malalamiko ya mtoto, akaongeza umakini katika
usikilizaji iliaweze kujua jambo.
‘’ Bado umekuja eh! Yale maji ya moto
hayakukuingia sawasawa, unataka mengine? Matoto yaliyotelekezwa na wazazi wao
huwa yanatabu sana. Sasa kama umekoswa pakwenda, endelea kunitumbulia mimacho
nikuchemshie maji mengine... Mpuuzi wewe.’’ Mwanamke yule alijibu namna ile.
Yale majibu si tu yaliuumiza moyo wa mtoto
yule wa kiume bali hata yule binti yalimuumiza pia. Ndani ya kichwa chake
akaisoma jeuri ya yule mama. Akagundua sababu za mtoto yule kuwa na jiraha
mkononi mwake. Kumbe alimwagiwa maji ya moto?
Uvumilivu
ulimshinda mtoto yule, yaani hajaiba cha mtu halafu anaumizwa namna ile kwanini
hasa? Hapo akayachukuwa macho yake mawili na kuyaangazisha chini, kisha akaanza
kuyatembeza huku na kule mpaka hapo alipofanikiwa kuliona jiwe lililokuwa
limeshangaashangaa mchangani, tabasamu lakujilazimisha likamtoka. Akalifuata
jiwe lile kwa mwendo wa upesi, hata alipoliokota kitendo bila hata kuuliza wala
kuomba ushauri kwa yeyote alilivurumisha jiwe lile hadi alipokuwa mwanamke
yule.
ITAENDELEA.
KWENDA SEHEMU YA KUMI BOFY HAPA>> SEHEMU YA KUMI
0 comments:
Post a Comment