DUKA LA ROHO SEHEMU YA NANE
IMELETWA KWAKO NA SIMULIZI MIX ENTERTAINMENT
MWANDISHI FRANK MASAI
ILIPOISHIA
Lisa alijitahidi
kuonesha furaha yake, lakini ukweli ni kwamba, hakuwa na furaha hiyo hasa baada
ya kusikia mkasa ambao Frank na Malocha umewakumba kipindi hicho. Mkasa wa Jina
la Chude Bobo. Walikuwa wanatafutwa kama dhahabu machimboni.
ENDELEA
Na baada ya ndoa hiyo
wakaenda nchini Uswiss kula fungate lao la miezi mitatu. Baada ya kutoka huko,
Gunner ndipo alipopewa taarifa kuwa mkewe anamimba yake. Jamaa alifurahi kupita
maelezo na kumnunulia kila kizuri huyu mwanamke baada ya taarifa hizo za faraja
kwake. Hakutaka kuhesabu muda alioutumia na Lisa katika mapenzi, alichojua yeye
katundika ampendaye mimba.
Hatimaye mtoto akazaliwa
na wakampa jina la Martina, jina la mama wa Lisa. Mwaka mmoja mbele, ndipo Lisa
akamuacha mwanaye katika kituo cha kulelea watoto na yeye akaenda kusomea mambo
ya ujasusi kwa miaka miwili. Alipotoka,
moja kwa moja akaingizwa katika shirika la FISSA wakati huo linaongozwa na
Juvenile. Shirika likiwa lina uchafu mwingi kuliko shirika lolote la kipelelezi
duniani. Shirika ambalo halikuwa na usawa kwa wananchi wake.
Pale Malocha alipokataa
kusema ukweli kuhusu Jina la Chude Bobo, FISSA walimtuma mdunguaji wao hodari
kwenda kuiangamiza familia ya Malocha.
Hayo yalifanyika kipindi Lisa yupo chuoni.
Baada ya Lisa kutoka
chuoni, maisha na mumewe yakaendelea huku akiwa mtu wa kuficha siri katika ndoa
yake.
Miaka minne akatimiza
Martina, Gunner akawa na uhitaji wa mtoto mwingine. Bila kumwambia mkewe shida
yake, akawa mtu wa kusaka mtoto huyo kwa kila hali lakini hakufanikiwa. Ndipo
alipoamua kwenda kuchukua vipimo vya uzazi katika hospitali moja iliyopo nchini
Afrika Kusini. Huko akaambiwa kuwa hana uwezo wa kumpa mwanamke ujauzito na
tatizo hilo kazaliwa nalo. Roho ilimuuma sana Gunner baada ya kugundua kuwa
analea kiumbe kisicho chake. Akarudi Tanzania na kupekua pekua nyaraka
mbalimbali za Lisa na ndipo alipokutana na picha ambayo ilimuonesha Martina
akiwa na miaka miwili na kwa nyuma iliandikwa "Ndoto zimekuwa kweli
Man'Sai, mtoto wetu huyu. To Frank
Masai."
Ni wazi picha hiyo
ilitakiwa kutumwa kwa Frank Masai wakati Martina ana miaka miwili, lakini haikumfikia
mlengwa na Lisa akaihifadhi. Mbali na
picha hizo, Gunner alikuta siri mbalimbali zikiwemo za FISSA. Akajizuia
asifanye chochote kwa wakati ule lakini akijiahidi kuwa ipo siku Lisa atatakiwa
kuujua ukweli na atatubu.
******
"Lisa, ni asubuhi mke wangu." Sauti
nzito ya Gunner ilimtoa usingizini Lisa ambaye alikutana na chai nzito ya
maziwa aliyoandaa mumewe. Kwa kiingereza wanaiita 'Bed and Breakfast' yaani
kifungua kinywa kiandaliwachwo wakati mtu bado yupo kitandani.
"Mmmh! Swetie. Haya
mambo umeanza lini tena." Lisa akamuuliza mumewe huku akinyanyua mgongo
wake tayari kwa kukitafuna kile alichoandaliwa.
"Siyo mimi peke
yangu. Na Martina kachangia kukuandalia." Gunner akaongea huku kagubikwa
na pambo zito la tabasamu usoni pake.
"Mmmh. Miaka sita
tu! Kishajua hadi ku........" Lisa hakumaliza kauli yake akaweka mkono
wake mdomoni huku macho akiwa kayaweka kama mtu asiyeamini kitu fulani. Wakati
huo na Gunner alikuwa kachanua tabasamu lake kama kawaida. "Ni birthday ya
Martina leo." Lisa aliongea huku akimuangalia Gunner kwa hali ya
sintofahamu.
"Najua majukumu ya
kazi ndio yanakufanya uikumbuke birthday ya mwana wetu sasa hivi." Gunner
aliongea huku bado tabasamu halimuondoki katika uso wake.
"Asante Gunner.
Sijui hata nimpe nini aisee."
"Usijali, nimekwisha
kuwakilisha. Na kaipenda zawadi niliyompa kwa ajili yako."
"Asante Baby."
Lisa akashukuru na kumkumbatia Gunner kwa upendo wa hali ya juu.
"Labda ananipenda
kwa sasa na hamkumbuki mtu wake. Ni kwa sababu sina uwezo wa kuzalisha tu!
Naamini kama ningekuwa naweza kumpa ujauzito mwanamke huyu, basi sidhani kama
Martina angekuwa tatizo. Ngoja niendelee kuvuta subira." Gunner aliwaza
hayo kichwani wakati wamekumbatiana na Lisa.
"Kula sasa baby.
Baadae nendeni mkatembee huko na Martina ili naye afurahi." Gunner
aliongea hayo huku akimtoa Lisa mwilini mwake na kummiminia chai hiyo ya maziwa
kwenye kikombe alichokiandaa. Lisa akatabasamu kwa furaha kwa matendo yale toka
kwa mumewe.
Akaanza kunywa taratibu
na vitafunwa kadha vilivyoambatanishwa na chai hiyo.
"Mamiee." Sauti
ya Martina iliita kwa nguvu na kumrukia mama yake ambaye alikwishamaliza kunywa
chai ile.
"Ooooh! Malaika
wangu. Hujambo eeh." Lisa akamkumbatia mwanaye huku anazilaza nyuma nywele
za singa alizoumbwa nazo. Nywele zinazofanana na baba yake, Frank Masai.
"Nipo salama mama.
Baba kanipa zawadi, na kila siku natoka naye. Leo nataka na wewe tutoke."
Martina aliongea kwa deko mbele ya wazazi wake waliokuwa wanatabasamu kwa
maneno mengi ya mwana wao.
"Kwani mimi sijakupa
zawadi?"
"Umenipa na nitaivaa
leoleo tukitoka."
"Haya basi,
kajiandae twende tukacheze cheze huko mbali." Baada ya maneno hayo,
Martina alitoka nje akikimbia kwa ajili ya kwenda kujiandaa na mtoko
ulioandaliwa na mama yake.
"Alikumiss
sana." Gunner akimwambia Lisa.
"Nilimmiss pia. Vipi
wewe, huendi na sisi?"
"Mi nitabaki. Labda
twende bafuni kuoga tu! Si wajua kitambo kidogo." Gunner akichombeza na
kubakiza tabasamu ambalo Lisa alilipokea kwa tabasamu pia. Hapo Gunner akachukua jukumu la kumbeba hadi
bafuni mkewe na kuanza oga naye hadi pale walipodhika. **** Ni furaha tele
zilitwala katika nyuso za mama na mwana, yaani Lisa na Martina. Michezo kama
bembea na kuteleza, vilikuwa vinajenga raha hiyo.
Masaa mawili yote
yaliishia kwenye kucheza na kufurahi kwa pamoja, lakini hali hiyo ilikatishwa
kwa simu iliyopigwa na Mubah.
"Hey Lisa. Unaweza
kuja huku Kitunda." Mubah alimuuliza Lisa.
"Mmmh! Nipo Mwenge
huku. Leo birthday ya Martina, nafurahi naye hapa."
"Njoo mara moja.
Kuna jambo la muhimu sana nataka unisaidie."
"Okay. Nakuja. Nipe saa
moja na nusu." Simu ikakatwa na Lisa akamchukua mwanaye mida hiyo ya saa
tisa alasiri tayari kwenda alipoambiwa na Mubah.
Baada ya saa moja na
dakika zipatazo kumi na tano, tayari Lisa alikuwa uso kwa uso na Mubah eneo la
Kitunda kabla Mubah hajachukua simu ya Lisa na kuifunga kisha kuitupia kwenye
ndoo ya uchafu.
Baada ya hapo, akampa
simu nyingine kama ileile na kupachika kadi ambayo Lisa huitumia kuwasiliana na
watu wake.
"Okay. Sasa twaweza
kwenda Lisa. Lakini si kwa gari lako bali lile pale." Mubah alimuonesha
Lisa gari lingine ambalo wangelitumia kwenda makao mapya ya Mubah. Lisa akaliweka gari lake katika usalama,
kisha akamchukua Martina na kwenda naye kwenye gari la Mubah bila kipingamizi.
"Hey Martina. Happy
Birthday." Mubah alimtakia heri ya kuzaliwa Martina huku akimlaza nywele
zake kwa nyuma wakati huo dereva wa gari hilo alishakamata njia ya kwenda
Kivule.
Wakati Mubah anakamata
nywele za Martina, mkono wake ukwama kwenye banio la nywele alilobania
Martina. "Hey. Kibanio chako kizuri.
Umekipata wapi?" Mubah alimuuliza Martina baada ya kukiangalia kibanio
hicho.
"Zawadi ya mama hii.
Kanipa leo." Martina akajibu na kumfanya Mubah amtazame Lisa kwa macho ya
kiulizo.
"Embu simamisha gari
mara moja." Mubah akamuamuru dereva wake na yeye akatii. "Lisa naomba tushuke mara moja."
Sauti ya Mubah ikatoa ombi dogo ambalo Lisa akalitimiza na kwenda naye mbali
kidogo kisha wakaanza kuteta kitu.
"Kile kibanio umempa
wewe kweli?" Mubah akamuuliza swali Lisa.
"Hapana. Kapewa
zawadi na baba yake. Lakini aliambiwa mimi ndiye niliyempa kwa sababu sikuwa na
zawadi hii leo. Kwani vipi Mubah?"
"Hamna tatizo. Ila
ni kibanio ghali sana kile, hadi nimeshtuka." Mubah alidanganya lakini
ukweli ni kwamba kile kibanio alichokuwa nacho Martina, ndicho ambacho mjomba
wake alipewa na Lobo. Yaani vinafanana. Ndicho kile kilichotoa sumu hatari
kutoka kwenye Yellowstone.
ITAENDELEA
KWENDA SEHEMU YA TISA BOFYA HAPA>> SEHEMU YA TISA
0 comments:
Post a Comment