DUKA LA ROHO SEHEMU YA KUMI NA MOJA
IMELETWA KWAKO NA SIMULIZI MIX ENTERTAINMENT
MWANDISHI FRANK MASAI
ILIPOISHIA
"Ipo chini ya tajiri
mmoja Mkam......" Kimya kikamkumba dada yule. Hakumaliza sentensi yake.
Lisa alipomuangalia mwanamke mwenzake, alimshuhudia akidondoka kitandani kama
mzigo huku damu zikimvuja kichwani palipokuwa pana tobo la risasi. Ukuta nao
ulikuwa umechafuka kwa damu hizo.
ENDELEA
Yote hayo yalitokea saa
mbili usiku. Kwa bastola ambayo imefungwa kifaa cha kuzuia mlio wa risasi,
ikamtoa uhai mke wa Mofo.
Lisa akatazama huku na
huko lakini hakuona chanzo cha risasi ile.
Akajaribu kwenda dirishani, ndipo alipoona dirisha limefunguliwa kidogo.
Yeye akafungua lote na kisha akapita hapo kwa sababu kulikuwa hakuna kizuizi
kikubwa cha yeye kutopita.
Alipotoka alikutana na
teke zito la uso. Hajakaa sawa kiakili, akakutana tena na ngumi ya uso
iliyomrudisha nyuma zaidi kimawazo. Hadi anakuja kutulia na kukaa sawa, tayari
alishapokea kipigo cha maana toka kwa mtu ambaye hakumuona.
Alisikia vishindo vya
kukimbia ndipo naye akajaribu kukimbia wakati huo lile eneo la nyuma kulikuwa
hamna watu.
Katika kukimbia, alimuona
mtu yule akimalizia kuruka geti kubwa la nyumba ile. Hapo Lisa ndipo alipoamini
kuwa alikuwa hapamabani na 'kinyangala mafuta' bali chatu mwenyewe.
Naye akajitahidi kuruka
na kutua nje. Akakuta mtu wake anahangaika kuwasha pikipiki aliyokuja nayo, huo
ndio ukawa upenyo pekee wa Lisa kujitambulisha katika nyanja za mapigano.
Teke zito la kifuani
likamkuta yule mtu na kumrusha nyuma ya pikipiki ile. Kabla hajanyanyuka, Lisa
akateleza chinichini na kumkung'uta teke lingine la uso. Adui wa Lisa akadhani
yataishia hapo, kumbe mwenzake ndio kwanza anayaanza.
Sarakasi mbili za
kujibetua kwenda nyuma, zikapigwa na Lisa, kisha akamaliza kwa kujitupa kwenye
tumbo la adui yule. Hapo akasikia sauti kali ikitoka kwenye kinywa cha mtu
yule.
"Kumbe ni mwanamke."
Lisa akajikuta akiropoka baada ya sauti ile. Kwa mavazi ya kininja aliyovaa mtu
yule, ni ngumu kujua anajinsia gani. Baada ya kipigo akajitambulisha kwa mlio
huo wa kike.
Lisa akajisahau kidogo na
huo ndio uliokuwa wasaa wa yule adui kupitisha miguu yake shingoni kwa Lisa na
kisha kumkaba kwa nguvu bila kumuachia. Kila Lisa alipojaribu kufurukuta,
hakuchomoka na badala yake, roba ikawa inazidi kumbana hadi akasaliti amri kwa
kuzimia palepale.
Hapo yule Mwanamke ninja,
akawahi pikipiki yake na kuipa kiki ya nguvu, nayo ikakubali sheria. Mwendo wa
ajabu ukachukua nafasi yake baada ya kuwaka. Akaondoka eneo hilo huku akimuacha
Lisa hana fahamu. **** "Lisa, Lisa, Lisa." Sauti ya mwangwi ilisikika
kwenye kichwa cha Lisa. Akajaribu kufumbua macho na kuona nani anamuita.
Ilikuwa ngumu kwake kurudiwa na fikra zake lakini alijitahidi na kufanikiwa
kufungua milango yake ya fahamu.
Sura za rafiki au
wafanyakazi wenzake aliziona zikiwa zinamtazama. Akatulia dakika kama tatu
kisha akafyonza baada ya kukumbuka tukio zima lililotokea nyumbani kwa Mzee
Rofo.
"Mbwa yule ni kweli
hayupo peke yake. Leo nimepambana na mwanamke mwingine." Lisa aliongea
huku akinyanyuka kwenye kitanda ambacho alikuwa kalazwa. Ni katika nyumba ileile ya Kivule ndipo
aliporudishwa tena.
"Vipi hali yako
lakini?" Malocha alimuuliza Lisa.
"Nitakuwa vizuri.
Martina yupo wapi?" Lisa akamkumbuka mwanaye.
"Yupo chumba cha
mapumziko kalala." Akajibiwa.
"Kwani sasa hivi saa
ngapi?"
"Ni saa nne
hii."
"Oooh! Mungu wangu.
Sijui mume wangu atakuaje."
"Usijali tumempa
taarifa kuwa upo kwetu na utarudi kesho." Lisa akapumua pumzi ya ahueni
kisha akatulia kitandani na kuanza kusimulia mkasa mzima ambao ulimtokea.
"Daah! Hawa watu si
wa kuchezea kabisa. Wapo vema kila idara. Hapa cha msingi ni kujitahidi kucheza
na silaha." Mubah alitoa ushauri kabla hawajamuacha Lisa peke yake mle
chumbani.
"Sasa kama
ulivyoona, tumepoteza chanzo kingine. Hapa tumebaki na hicho kibanio tu!
Tumejaribu kufuatilia vinapotoka, tumegundua ni Malyasia. Huko itabidi uende
peke yako Mubah." Malocha alikuwa akimpa mchakato mwingine wa kufanya
Mubah.
"Mmmh! Mkuu, kwa
nini tusimwambie ukweli Lisa ili tushirikiane naye kupambana? Wajua siwezi peke
yangu. Tumwambie tu ukweli." Mubah alitoa ushauri ambao Malocha
aliinamisha kichwa chake chini kabla hajatoa maamuzi.
"Wajua ni ngumu
sana. Halafu maisha ya Lisa tutayaweka matatani zaidi." Malocha akatoa
jibu.
"Lakini hata hivyo
siku akijua tayari maisha yake yatakuwa hatarini." Mubah aliweka neno
ambalo nalo halikuwa baya.
"Okay. Tutamwambia.
Lakini siyo leo wala kesho. Hiyo ni kwa usalama wa.mwanaye zaidi." Malocha
aliongea.
"Kwani mtoto naye
ana nini. Mtoto wao halafu wamdhuru?" Mubah akapatwa na mshangao. Malocha
akamsogelea Mubah pale alipo kisha akaanza kwa kumgonga gonga bega.
"Jambo usilolijua,
ni sawa na usiku wa kiza. Tuyaache hayo, nishatoa neno na litimizwe. Utaenda
Malyasia." Malocha akamaliza.
"Sitaenda kama
huwezi kumwambia ukweli Lisa. Lisa yapaswa aambiwe ukweli." Mubah alimfata
mkuu wake na kumwambia maneno hayo kwa msisitizo.
"Mnataka kunificha
nini?" Lisa akatokea na kuwauliza Malocha na Mubah huku akiwaangalia kwa
zamu. "Mnataka kunifanya na mimi ni mtoto mdogo? Niambieni mlicho kificha.
Yawezekana hata yule mtu aliyemuua mke wa Rofo mlinitegea nyie. Tangu natoka
pale Kitunda, huyu alikuwa ananiangalia kwa mashaka. Sasa nataka mniambie
ukweli sasa hivi." Lisa akaweka mkazo kwenye akitakacho huku sauti yake
ikiwa katika hasira.
"Lisa tulia. Kila
kitu kitakuwa sawa. Na kila....." Hakumaliza kauli Malocha, ikawa imekatwa
na Lisa.
"Sitaki maelezo ya
kipumbavu kama hayo. Nataka muwe straight katika majibu nayoyataka. Nini
mnanificha?"
"Mume wako
anashirikiana na Lobo." Malocha akamwambia Lisa na kuondoka lile eneo huku
akiwa kakunja sura yake. Akabaki Mubah
ambaye alikuwa akimtazama Lisa aliyekuwa katika mkanganyiko wa hali ya juu
baada ya maneno yale.
"Haiwezekani."
Lisa akatamka hayo huku taratibu akishuka na kujikuta akikaa chini.
"Ni kweli Lisa. Na
ndiye niliyemuona mara ya mwisho kabla sijazimia ile juzi wakati nyumba yangu
inalipuliwa." Mubah alichomelea ukweli ambao anaujua. "Na hata hicho
kibanio cha mwanao, kinafanana na kile ambacho kilitema sumu na kuua wenzetu
kule nyumbani. Na yewezekana yule mtu uliyepambana naye, kakuacha sababu ya
ukaribu wako na Gunner." Mubah akamaliza huku naye akienda na kukaa pale
alipokaa Lisa.
"Yawezekana ile
picha ya Martina aliyonionesha Lobo wakati tumemkamata, kampa yeye Gunner. Kama
kampa yeye, basi tayari anajua siri nyingi sana zituhusuzo." Lisa akaamua
kufunguka.
"Ni kweli. Kakuwekea
GPS katika mifuko yako mingi unayokuja nayo kazini. GPS hizo ni ngumu
kujulikana pale unapokaguliwa na vifaa vya FISSA kwani GPS hizo ni za plastiki
na hazitumii aina yoyote ya umeme." Mubah akamtobolea ukweli uliokuwa
mgumu kuamini kwa yeyote mwenye mapenzi.
"Okay. Sasa naanza
kupata picha kwa nini anamfundisha Martina kutumia silaha. Mjinga sana yule,
kesho naenda kumuua." Lisa aliongea kwa kiapo na kunyanyua uso wake ambapo
alikutana na uso wa Malocha ukiwa unamtazama kwa makini.
"Lisa. Hata ukipewa
miaka ishirini ya kumuua Gunner, hutoweza. Yule umuonavyo, sivyo alivyo. Ni
heri ukutane na treni ya umeme relini, kuliko kukutana na uso halisi wa yule
mtu. Tutakupoteza dakika sifuri tu." Malocha alimtahadharisha Lisa kwa
maneno machache.
"Sasa
nifanyaje?" Lisa alimuuliza Malocha.
"Cha msingi ni wewe
kutulia hapa. Hatofika mtu hapa. Au kama waweza, rudi kwako na kujifanya hujui
lolote. Na kingine, mtoto wako anafundishwa kulenga huku akioneshwa picha ya
Frank." Malocha akamaliza na kuelekea chumba kilichokuwa na mitambo ya
kipelelezi.
Akamuacha Lisa akiwa
kakodoa macho asijue ni nini afanye kwa wakati ule. Mubah naye akanyanyuka na
kuondoka eneo lile akiwa na amani kiasi baada ya Lisa kuugundua ukweli.
ITAENDELEA
KWENDA SEHEMU YA KUMI NA MBILI BOFYA HAPA=> SEHEMU YA KUMI NA MBILI
0 comments:
Post a Comment