NIENDE WAPI? ‘’Dunia imenichukia’’
IMELETWA KWAKO NA SIMULIZI MIX ENTERTAINMENT
MWANDISHI: ZUBERY RAZUUR MAVUGO.
SEHEMU
YA KUMI NA MOJA.
ILIPOISHIA:
Alipoagana na mkewe akatoka, na moja kwa
moja akaelekea kwenye kituo cha daladala, hata alipofika alipanda magari
yaelekeayo mjini. Yalimtua na yeye akaanza safari ya kulifuata soko kuu.
Alipofika ndani ya soko hilo alielekea upande wa wauzaji wa kuku na moja kwa
moja akawafuata mabwana watatu waliyokuwa wamesimama pembeni kidogo, akawasalimu
na wao wakamwitika kama kwamba
wanafahamiananaye kisha, wakamlaumu kwa kuchelewa, alizikubali lawama zile na
mazungumzo yakaanza.
ENDELEA...
Mazungumzo yao hayakuonekana kuhusisha jambo jingine zaidi ya biashara. Mwisho
wa siku walielewana na bwana Mashaka akaachwa pale yeye pamoja na mabanda
kadhaa ya kuku ambayo ndani mwake yalihifadhi kuku wakubwa kwa wadogo.
Akiwa mwenyewe
aliwafuata wauza kuku majirani zake na kuanza kuwaulizia mambo kadha wa kadha
aliyoyajua mwenyewe.
‘’ ...
Vizuri, nashukuru sana. Mie kwa majina naitwa Kijogoo Hasani... Karibu sana.’’
‘’
Ahsante, nami pia nashukuru kukufahamu.’’
Walipomaliza kusalimiana alihoji maswali
kadhaa aliyohitaji na kupatiwa majibu yaliyomridhisha. Hadi anatoka pale tayari
alikuwa amesha jifunza mengi sana; Kujifunza kwake haikumaanisha kuwa wazo la
kuku katika maisha yake ni la jana ama leo. Kiufupi lilikuwa moja kati ya
mawazo yaliyosahaulika. Akikumbuka mshawishi mkuu wa jambo lile alikuwa ni baba
yake mzazi, mzee Magabe.
Mzee aliyekubali kuitwa kila aina ya majina
ilimradi aziheshimu nywele zake. Hakujali walipomuita manyewele, alichojali ni
kuhakikisha ana acha pesa kila siku nyumbani kwake na watoto wake wanapata
kusomo, ingawa alikuwa ni mtu wa watu lakini alikuwa na mawazo binafsi ya
kimaendeleo. Kila siku jioni alimwita manae mkubwa wa kiume kwa jina la Mashaka
na kumtoa kando kidogo kisha alimweleza nini maana ya maisha na ni vipi kijana
anapofikia umri wa kujitambua anapaswa awe.
Laiti kama kuna mtu mwingine angekuwa akiyasikia
maneno ya mzee Magabe dhidi ya mwanae, kiukweli angehisi huenda mzee yule
ameshachizika. Alifanya yote hayo huku akiamini na kumwambia mwanae kuwa, ‘
Hatuyajui ya kesho, hata sasa naweza kuondoka duniani ukakosa baba wa kukupa
maarifa.’ Mashska aliyatii maneno ya
baba yake na kufuata kila alichoambiwa.
Naam, hata hivyo Mashaka alisoma na kumsaidia
haswa baba yake, ukija katika swala la uuzaji na ufugaji wa kuku, hakuwa mtu
mwenye uwezo wa kawaida. Alipomtazama kuku fulani aligundua mpaka mambo yanayoweza
kumfanya akapatwa magonjwa, udhaifu wake baada ya magonjwa na kadha wa kadha.
Kitendo hicho kilimpelekea hata kuwa bora shuleni na kujiingiza kwenye krabu
mbalimbali za ujasiriamali ambako huko pia alijifunza mengi sana.
Alijipatia elimu ya kutosha kutokana na kazi
ile ya baba yake mpaka hapo alipoamua kujitegemea baada ya kupata kazi nzuri
yenye malipo ya kufaa. Muda kidogo alipotoka kwao, baba yake nae hakukawia,
mapafu yaliyokuwa yakimsumbua kwa muda mrefu nd’o hayo yaliyomuondoa duniani.
Tangu alipopata kazi na kupata pesa,
alijikuta akizisahau kabisa ndoto zake za kufuga na kuuza kuku. Akajidanganya
na kuiamini benki kuliko chochote maishani mwake huku akijua kununua nyumba na
magari ndivyo vitavyomfanya awe tofauti na hata kuendelea kwenye maisha mazuri,
hakujua kama kufumba na kufumbua, pesa zilizo kuwa benki zinaweza kuchukuliwa
zote na hata kumfanya awe mtu asiye na mbele wala nyuma. Baada ya kuteseka
mtaani, hapo ndipo alipoyakumbuka yale mawazo ya baba yake, alitamani aanzishe
mradi wa ufugaji kuku na hata kujiingiza kwenye uuzaji kuku lakini hakuwa na
pesa.
Hata alipofanikiwa kuzipata pesa zile ndipo
alipoamua kucheza na akili yake kwa haraka, na kuanzisha mradi wa uuzaji kuku
huku akiwaza endapo kipato kikieleweka basi atajitupia katika ufugaji, awe kama
marehemu baba yake.
Hivi sasa alikuwa akishughulika na wateja.
Atoke huyu aingie yule yote hiyo ni kutokana na kuuza kuku wa haja! Biashara
alijikuta akiifurahia ingawa nd’o kwanza alikuwa akianza, hata jioni ilipofika
alifunga banda lake na kuagana na wauzaji wenzake kisha akaianza safari ya
kurejea nyumbani kwake.
Alipofika alimkuta mkewe akiwa amejilalia
kwenye kochi huku akitazama televisheni.
‘’ Vipi mbona umeondoka tangu muda ule mpaka
sasa? Ulikuwa wapi?’’
‘’ Nilikuwa kazini?’’
‘’ Ha! Mume wangu? Kazi gani tena? Au
umeshasahau kama wewe huna haki ya kufanyakazi kutokana na yaliyotukuta.’’
‘’ Mke wangu, sifanyi kazi ndani ya kampuni,
nipo mimi kama mimi... Hivi sasa nafanya kazi ya kuuza kuku.’’
Waliongea mengi sana, mkewe alifurahi sana
baada ya kusikia jambo lile kutoka kwa mumewe, hapo akaanza kumuuliza mambo
kadha wa kadha kama mipango na malengo ambayo mumewe amejiwekea.
‘’ Sasa ni vyema ungepata maji ya kuoga
kwanza.’’ alisema na mumewe akaafiki.
Usiku huo waliufurahia kwa utani wa hapa na
pale, mambo haya na yale. Wakikumbuka maisha waliyopitia baada ya kufukuzwa
kazi, aibu walizozipata kiasi cha kutothaminiwa na yeyote, hapo waliishia
kusema, ‘Fadhili mbuzi utakunywa mchuzi binadamu atakuudhi’ na misemo mingine
mingi yenye maana kama hiyo ama zaidi yake.
***
Bado
aliendelea kurandaranda mitaani kama kawaida yake. Kila alliyepita katika mtaa
ule yeye alimpiga jicho na hata kumchunguza kutumia sayansi yake aliyeiita
‘sayansi ya kujikimu.’ Hakuwa na mtaji wowote ule zaidi ya yeye mwenyewe. Siku
hiyo ni kama ilikuwa ya manyanyaso kwake, mpaka usiku ule ni vipi hajapata
windo hata moja?
Akiendelea kutafakari kwa uchungu mara
alimwona bwana mmoja mwenye tumbo kubwa, aliyevalia suti ya haja, huku simu ya
kugusa kwa kidole ikiwa mkononi mwake, akionekana kama mwenye kuwasiliana na
mtu kwa njia ya ujumbe ama mwenye kuperuzi.
Mwindaji yule hapo kidogo roho ilimtulia
akajihisi amani na kuanza kulifuatilia windo lake. Ingawa alilihofia umbo la
bwana yule kutokana na yeye kuwa mdogo lakini alijikuta akitabasamu baada ya
kumtazama sura yake.
Alitamani kucheka lakini akajikaza. Bwana
mwenye umbo nene alikuwa na sura yenye kuwiana
na mtoto mchanga isiyo na kovu wala nini? Tangu lini mtoto yule kwa jina
la Maduhu aogope watu wenye sura za kitoto? Hapo akaingiwa na imani l kwamba;
lazma angeimiliki simu ile na kuitafutia mteja huku yeye akipata pesa ambayo
ingemwezesha kupata chakula.
Hata bwana yule mwenye sura ya mtoto mchanga
alipomkaribia hakumjali maana hakujua chochote kilichokuwa kikiendelea, mara
kufumba na kufumbua akajikuta hana simu mkononi mwake. Baada ya kutazama ndipo
alipomuona mtoto mdogo akikimbia kuelekea vichochoroni. Hapo akatamani
kumfuata, akiwa njiani akakumbuka jinsi ambavyo kumfuata mtoto yule kunaweza
mfanya hata ayahatarishe maisha yake.
Kwani simu kitu gani juu ya uhai? Akili yake
ilimwambia na hapo akaamua kuachana na mtoto yule kisha akaendelea na safari
zake.
Jambo lile lilikuwa kama dharau na kashfa
mbele ya kijana Maduhu; ni wazi kuwa, hajazoea kukwapua cha mtu na kutelekezwa
bila hata kutimuliwa. Alihisi huenda mtu yule mwenye sura ya mtoto mchanga
alikuwa akimjaribu, lakini aliziondoa hisia zile baada ya kukumbuka kuwa, ndani
ya dunia hii kuna watu kwa jina la matajiri.
Maadam yupo hai, hakuhitaji kuyajali sana
maswala hayo, akajipitisha sehemu tofauti tofauti zilizo changamka ndani ya
jiji hilo. Hapo akafika kwenye duka moja la simu na kukutana na muhudumu
aliyeonesha kufahamiana nae.
‘’ We mduanzi, hii kitu ina shilingi ngapi
hapo dukani kwako?’’
‘’ Kitu ina lakini na nusu hii.’’
‘’ Basi shega... Bunda, tutakutana baadae.’’
Baada ya maneno hayo machache akatoka ndani ya
duka lile la simu na kuelekea kwa jamaa yake mmoja mrusha miziki. Wakasalimiana
kwa salamu zao kisha akamwelezea kuhusu simu ile na kumwambia endapo atamtoa
shilingi elfu ishirini tu basi kila kitu watakuwa wamemaliza. Rafiki yake yule
hakutaka hata kuuheshimu uzuri wa simu ile, hapo badala aombe, yeye akashusha
bei na kung’ang’ana apewe kwa shilingi elfu kumi simu ile ya laki na nusu.
ITAENDELEA.
KWENDA SEHEMU YA KUMI NA MBILI BOFYA HAPA=> SEHEMU YA KUMI NA MBILI
0 comments:
Post a Comment