Friday, July 7, 2017


DUKA LA ROHO SEHEMU YA TISA
IMELETWA KWAKO NA SIMULIZI MIX ENTERTAINMENT
MWANDISHI FRANK MASAI
ILIPOISHIA
"Hamna tatizo. Ila ni kibanio ghali sana kile, hadi nimeshtuka." Mubah alidanganya lakini ukweli ni kwamba kile kibanio alichokuwa nacho Martina, ndicho ambacho mjomba wake alipewa na Lobo. Yaani vinafanana. Ndicho kile kilichotoa sumu hatari kutoka kwenye Yellowstone.
ENDELEA
Wakarudi kwenye gari baada ya maongezi machache na kisha gari likakaza mwendo kuelekea Kivule.
Kichwa cha Mubah hakikutulia hata kidogo kimawazo. Akiwa katika mawazo hayo, ndipo akakumbuka sura ile iliyompita kwenye gari wakati yeye anazimia. Akakurupuka tena na kumuangalia Lisa kwa macho ya kushuku kitu. Lisa akabaki mwenye mshangao wa hali ya juu kwa matendo nadra ayafanyayo Mubah.
"Yule ni Gunner, mume wa Lisa. Mshenzi anashirikiana na Lobo. Mungu wangu." Mubah akajisemea mwenyewe moyoni huku akimkodolea macho makali Lisa.
"We' Mubah unamatatizo gani!? Hiyo tabia umeitoa wapi." Ikabidi Lisa amuulize Muhah jambo linalomsibu hasa baada ya kuona macho ya Mubah hayakauki usoni pake.
"Hakuna Madam. Basi tu!" Mubah alijichekesha huku akijaribu kuumba tabasamu la mbao usoni pake.
"Usinifanye mimi mtoto Mubah. Mi' ni Jasusi na pia ni mpelelezi kuliko wewe. Najua unafahamu kitu, haya haraka eleza nini kipo nyuma ya pazia." Lisa akauliza tena akiwa katika uso usio na masikhara. Wakati huo, gari lao lilikuwa likizidi kusonga mbele na Martina akionekana kufurahia mwenendo mzima wa safari ile.
"Hamna kitu madam Lisa. Nitakwambia tukifika kwani kwa sasa kidogo, itafanya kazi yetu kugoma." Mubah alijitetea huku akijing'ata ng'ata bila kujua sababu ya kufanya hivyo.
"Basi sitaki unitazame tena usoni. Acha kabisa." Lisa alifoka na kumuangalia mtoto wake ambaye alikuwa anacheza kwa kumrusha mdoli fulani aliyenunuliwa na mama yake.
Mubah akaamua kutulia kama si yule wa mwanzo. Na kwa bahati mbaya au nzuri, alikuwa anajali kazi zaidi kuliko matukio yaliyompata. Akili yake yote ilijaa kisasi kuliko jambo lolote lile.  Gari ikazidi kutitia kwa mwendo wa madaha hasa kwa sababu ya barabara mbovu ya kuelekea Kivule.
"Mama, baba ananifundishaga kupiga kwa kutumia hiyo." Martina alimwambia mama yake huku akisonta kidole kwenye kiuno cha dereva wa gari lile.  Alikuwa kapachika bastola yake ambayo ilionekana vema baada ya shati lake kujivuta na hiyo ndio ikampa wasaa Martina kuongea hayo.
"Anakulengeshaga nini?" Mubah alimuuliza Martina kwa hamasa huku Lisa akiwa kama haamini kile ambacho anakisikia.
"Anakunywagwa bia, halafu ananiwekea chupa nilenge. Siku nyingine ananipeleka porini na kuniwekea mbao zikizochongwa kama watu, ananiambia niwe nawapiga kichwani au kifuani. Hao ni maadui." Mtoto Martina alizidi kutiririka bila uoga.
"Na kingine anachokufanyiaga." Mubah akatupa swali lingine.
"Ananipaga picha na kuniambia huyo ni adui yetu, nikimuona kama nina bunduki nimpige kichwani."
"Picha hiyo yupo nani?"
"Mubah muache mwanangu. Nitashuka sasa hivi. Sitaki huo ujinga kuusikia ukimuuliza mwanangu." Ikabidi Lisa amfokee Mubah kwa sababu ya maswali makavu amuulizayo mtoto wake wa pekee.  Mubah akameza mate ya hasira lakini akakaa kimya kwa sababu angeendelea, angemkosa Lisa katika mipango yao. Kimya kikachukua nafasi yake na safari ya kwenda Kivule ndio ilikuwa inaendelea kwa wakati huo. **** Malocha alikuwa hajui cha kufanya baada ya kuisubiri simu ya jamaa aliyemtegemea labda atapiga baada ya kusikia kuwa hata Lisa atakuwa matatizoni. Akawa amechoka kuisubiri kwa sababu jamaa hakupiga wala kubipu au kutuma meseji.
Usiku wa manane Malocha akawa analanda landa ndani ya FISSA bila kujua ni nini anatafuta au nini anataka kufanya. Mara anaenda huku mara huko ili mradi awe anatembea tu.
Mwisho wake ulikuwa ni ofisini kwake na mawazo tele yakimwandama hasa kwa sababu ya mtu wake kutopiga wala kuitikia anachokitaka.
"Ina maana Masai amekwisha sahau ahadi yetu? Kasahau kabisa kuwa nitakapomuhitaji nitamtaarifu? Lakini hilo si kitu, inamaana pia kamsahau Lisa? Kamsahau kabisa mtu aliyesema anampenda kila mara. Frank atakuwa anamatatizo huyu mtu." Malocha alijisemea peke yake muda wa saa kumi usiku.  Ama kwa hakika alikuwa kapagawa hasa kwa matendo kama kuwafukuza wafanyakazi wake wote usiku huo.
Asubuhi ya saa moja, akiwa kidogo kapitiwa na usingizi, simu ya ofisini kwake ililia kwa nguvu na kumfanya akurupuke kama mwenye kuwehuka. Alipoangalia kioo kodogo cha simu ile ya mezani, aliona ni namba ya Ikulu ndio yenye kupiga.
"It's over now. (Yameisha sasa)" Malocha aliongea hayo wakati akiiangalia simu hiyo ikiita.
"Hallow mkuu." Malocha aliita kwa sauti ya taratibu.
"Sijawahi kuona mtu mpumbavu kama wewe. Jinga la kutupwa kama mbwa lililokosa matunzo. Yaani unadiriki kufukuza wafanyakazi wote usiku kama vile shirika ni lako. Unavunja sheria za shirika kama vile umelianzisha wewe." Rais alikuwa anaongea kwa sauti ya juu kana kwamba alikuwa anaongea na mtu wa maili kadhaa mbali.
"Kwa hiyo unataka nini mkuu. Nimeshafanya." Malocha akamuuliza mkuu wake kwa nyodo.
"Unasemaje we mbwa? Dharau umezianza lini? Sasa kwa taarifa yako, nimekwisha andaa uongozi mpya. Wewe, na mbwa wenzako hao wawili, Mubarak na Lisa, wote mtakuwa nje ya FISSA. Katafuteni pa kufanyia kazi, si hapo. Sihitaji washenzi tena." Maneno hayo yakaenda sanjari na kukata simu. Malocha akatabasamu kisha akaanza kukusanya kilicho chake kabla ya huo uongozi mpya haujafika. **** "Usafiri uwatoao nje wafanyakazi wa FISSA ni usafiri ambao si rahisi kwa mtu wa ndani kuona nje. Na hata Malocha alipoamua kwenda kuupanda, ilikuwa ni vivyo hivyo.
Usafiri huu hutambua sauti za wafanyakazi wote wa shirika lile la siri. Na pindi wapandapo, basi hutoa sindano ndogo ambazo zinachomwa mikononi na usingizi mzito huwachukua waliopanda usafiri huu. Pia hujiendesha wenyewe kwa kuwa umetengenezwa maalumu kuwafikisha wafanyakazi wake sehemu husika.
Muda wa saa sita, Malocha tayari alikuwa amekwishakwea kwenye usafiri mwingine ambao huo ulikuwa ni wa wananchi wa kawaida. Wale wazoefu wa jiji na miji wanauita usafiri huu ni tax, na ndio Malocha alikuwa kaupanda.
"Mkuu tunaelekea wapi." Dereva mmoja mchangamfu alimuuliza mteja wake ambaye alikuwa kama katoka kulewa pombe kali usiku wa jana.
"Nipeleke Kivule Kamanda." Malocha alijibu na dereva yule hakujali gharama ambayo itatokea kwa sababu muonekano wa Malocha, haukuwa wa kukosa fedha ambazo atamtajia.
"Hallow Mubah." Malocha alisikika kwenye simu.
"Ndio mkuu."
"Hatuna chetu FISSA. Fanya hima tukutane Kivule ukiwa na ripoti nzima ya Lobo."
"Sawa mkuu. Rais ndio katutoa au?"
"Yaap. Ni mkuu."
"Na nani mwingine kamtoa."
"Lisa naye katolewa."
"Okay. Basi na mimi nakuja huko Kivule sasa hivi." Mubah aliongea kwa shahuku kubwa.
"Na mimi ndio nipo Posta hapa, nakuja taratibu." Malocha akamalizia kabla ya kuanza maongezi mengine ya kijamii na maisha na Mubah kupitia simu.
****
"Najua umeona hilo bomu lilivoenda na kulipua nyumba yako. Lakini sasa unatakiwa kuangalia mazingira ambayo bomu hilo limetokea. Rudisha huo mkanda nyuma na kuanza kuchunguza kimoja baada ya kingine." Sauti ya Malocha ilikuwa ikimuelekeza mtaalamu wa mmoja wa kompyuta aliyekuwa anacheza mkanda mzima ambao ulionesha tukio zima lililotokea nyumbani kwa Mubah.
Nyumba hiyo ya Kivule, ilikuwa ni nyumba moja kubwa kiasi na huwezi kujua ndani kunafanyika nini kama hujaingia na kuchunguza.
Ndani ya nyumba hiyo kulikuwa kumetapakaa dhana mbalimbali za Kijasusi na kipelelezi. Bunduki za kila aina na vifaa vya kipelelezi, vilipendezesha chumba ambacho Mubah na Malocha walisimama wakiwaangalia wale jamaa wanaocheza video nzima ya tukio la Mubah.
"Hapo hapo Banchi. Umeona hilo gari jeusi?" Mubah alimsimamisha jamaa mmojawapo wa kompyuta na kumuonesha gari ambalo alilishuku vibaya. "Hilo ndilo nililiona wakati nazimia. Naomba ulichunguze."
"Kama ndio hilo, basi tutaanzia kazi zetu hapo. Cha msingi tupate namba za usajili za gari hili (plate number)." Malocha aliongea huku kafumbata mikono yake kifuani.
"Namba hizi hapa mkuu. Ni T 900 QJG." Opareta wa kompyuta zile, alitoa taarifa hizo na kuwafanya Mubah na Malocha kusogea kwa karibu na kuzitazma.
"Okay. Safi Banchi. Sasa Mubah, hapa tunamuhitaji sana Lisa kwa sababu yeye ni mwanamke awezaye kuwavuta watu wowote na wakafungua vinywa vyao kusema siri. Cha msingi, mpigie simu sasa hivi mwambie muonane Kitunda. Halafu mkikutana, mpe hii hapa simu halafu ndio mje huku." Malocha alimpa maelekezo ambayo Mubah alikuwa anatikisa kichwa kukubaliana nayo.
"Sasa kwa nini unampa simu hii?" Mubah akamuuliza Malocha.
"Lisa yupo hatarini bila yeye kujitambua. Mume wake si mtu kama anavyodhani, muda wowote anamgeuka. Huyo ndio sababu ya Lobo kujua njia nyingi za FISSA kwa sababu anamuwekea GPS kila anapojua zimetolewa. Nakwambia haya lakini usimwambie chochote kile. Atakuja kuju a ya kumaliza mambo haya." Malocha alimuelekeza Mubah mambo kadhaa, kisha kuanza kumpa siri za Lisa ambaye alikuwa anacheza na mwanaye anayesheherekea siku yake ya kuzaliwa.
"Kwa hiyo mume wa Lisa anashirikiana na Lobo."

ITAENDELEA

KWENDA SEHEMU YA KUMI BOFYA HAPA=> SEHEMU YA KUMI


0 comments:

Post a Comment