NIENDE WAPI? ‘’Dunia imenichukia’’
IMELETWA KWAKO NA SIMULIZI MIX ENTERTAINMENT
MWANDISHI ZUBERY RAZUUR MAVUGO.
SEHEMU YA KUMI NA NNE.
ILIPOISHIA:
Hivi sasa aliufikia mlango, alifanikisha
kuufungua na kuanza safari yakutoka ndani ya chumba kile alichokuwemo. Akiwa
njiani, huku akitegemea usaidizi wa ukuta katika kutembea, alijikuta akiishiwa
nguvu zaidi kitendo kilichompelekea aanguke chini kama mzigo na kujitonesha
zaidi, hapo akajikuta akipiga makelele kutokana na maumivu aliyoyapata kufuatia
tukio lile alilokuwa akilifanya.
ENDELEA...
Aliendelea kugaagaa pale chini, baada ya kukumbuka kuwa hakuhitajika kupiga
kelele hapo akajilazimisha kulia kimyakimya. Ni kama tayari alikuwa amechelewa,
sauti yake iliwafikia vyema wauguzi wawili ambao walikuwa mkabala na eneo lile,
tayari walitoka mbiombio na kwenda kutazama kipi kilichokuwa kikiendelea.
Walimkuta akiwa chini huku vidonda vyake vikitoa damu, yeye akiwa makini na
kichwa chake kilichokuwa kikimuuma sana kwa wakati huo.
Wauguzi
wale wawili walijitahidi kumsimamisha kwa tabu na kumrejesha hadi ndani ya
chumba alichokuwamo kisha wakamsihi ajaribu kuwa mvumilivu maana bado hajapona
vizuri.
‘’... Hicho unachotaka kukifanya, kinaweza
kukugharimu maisha yako mwanangu. Tupo kwa ajili ya kukuokoa nasi kukupoteza.’’
Muuguzi mmoja mwenye umri uliyoenda kidogo alisema.
‘’ Mimi sipo radhi kuchukuliwa na mapolisi...
Bora mniache nijiondokee zangu, nikafie mbele kwa mbele.’’ Mtoto Maduhu
alisema. Hakuishia hapo tu, aliendelea kulalamika zaidi na zaidi kitendo
kilichowapelekea wauguzi wale wamdunge sindano ya usingizi. Wakapumua na
kumrejeshea mrija wa dripu pamoja na kuvisafisha vidonda vyake na kuviwekea
dawa nyingine.
Baada ya hapo walitoa taarifa kwa daktari kuwa;
mgonjwa tayari amezinduka lakini wamemchoma sindano ya usingizi ilikumfanya
apumzike, kisha wakamuelezea hali halisi jinsi ilivyokuwa.
***
Mashaka alipotoka kazini aliamua kupita moja
kwa moja hadi hospitali kwa ajili ya kujua maendeleo ya mgonjwa wake. Hata
alipofika alikutana na habari njema kutoka kwa daktari; kwamba, mgonjwa wake
tayari amezinduka, kilichobaki ni kupona kwa majiraha aliyokuwanayo tu. Hapo
furaha ya ajabu ikamfika Mashaka.
‘’ Kwahiyo ninaruhusiwa walau kumuona hata
mara moja?’’
‘’ Bila shaka, lakini hutoweza kuongeanae
maana amepumzika kwa sasa.’’
Mashaka akachukuana na daktari hadi kweye
chumba alichokuwam Maduhu. Hapo akapata muda wa kumtazama, aliporidhika aliamua
kuondoka na kuelekea nyumbani kwake.
***
Siku hiyo ilipita, ikafuata siku nyigine.
Tayari mgonjwa kwa jina la Maduhu alikuwa akiendelea vyema na hivi sasa alikuwa
ameshapatiwa ushauri pamoja na nasaha mbalimbali zilizomuondoa woga
aliyokuwanao, lakini hakuwa mbali na jeuri yake.
Ingawa siku hiyo Mashaka alitamani kumuona
mgonjwa wake lakini shughuli zilimbana na kumfanya achelewe kitendo
kilichompelekea apitilize moja kwa moja nyumbani kwake. Siku iliyofuata
alijitahidi na kwenda kuonana na mgonjwa wake.
‘’ Naitwa Mashaka, ni mimi niliyekusaidia
dhidi ya raia wenye hasira kali.’’
‘’ Ahsante
kwa msaada wako, lakini hukuwa na haja ya kufanya yote hayo kwangu.’’ Maduhu
alijibu na kumpelekea Mashaka abaki hoi kidogo.
‘’ Una
maana gani? Ina maana mimi kukusaidia nimefanya makosa?’’ Mashaka alisaili.
‘’ Wewe unadhani
hujafanya makosa? Tangu lini mtoto kama mimi nikawa na thamani? Nilitamani kufa
mara nyingi sana, na nafasi ya kukipata kifo ilikuwa ni ile, vipi wewe
unisaidie? Kwani nilikutuma?’’ Maduhu alisema.
Hapo
Mashaka akashindwa kuuepuka mshangao wake, akiwaza. Ni vipi mtoto mdogo kama
huyo anakuwa mwongeaji? Kila akimkadiria umri wake unaonesha ni mwenye miaka
nane, saba ama tisa. Iweje anajua kuyamiliki maneno namna ile? Hapo akajikuta
akitamani sana kuongeanae.
‘’ Kwani wewe ukiwa mtoto wa mtaani nd’o
hupaswi kusaidiwa?’’
‘’ Ndio. Kwanza wewe ni binadamu hali yakuwa
mimi si binadamu, huoni hatuendani?’’
‘’ Kivipi unasema wewe si binadamu?
Unaushahidi gani?’’
‘’ Mkubwa, tusiulizane maswali mengi, hata
wewe naweza kukubadilikia na usiamini macho yako... Mimi nitatafuta hata bisu
nikuchome tumboni, kwanza achana na mimi... Halafu unaniuliza maswali ya
kipuuzi, kama ningekuwa binadamu kama wewe, unadhani ningeweza kugombania
chakula na mbwa? Unadhani ningeweza kuishi na kulala kwa kuungaunga? Unadhani
wazazi wangu wangeondoka na kuniacha peke yangu, unadhani mimi nina ukoo kama
wewe? Achana na mimi.’’ Mtoto yule aliongea kwa uchungu haswa, hapo akajikuta
akishindwa kuvumilia, machozi yakamdondoka bila aibu.
Mashaka alijikuta akigudua kitu cha ziada
kutoka kwa mtoto yule. Akaona endapo atamchukuwa yule mtoto na kumsaidia bila
shaka ipo siku atamfaa.
Hata alipoondoka na kwenda zake nyumbani bado
jambo lile aliendelea kulifikiria kwa mapana na marefu. Akamwita mkewe na
kumuhusisha kwenye jambo lile.
‘’ Ha! Mume wangu, ina maana tuseme
umechanganyikiwa kiasi chakutaka niletea wizi humu ndani? Tazama, maisha
yenyewe haya si tutaibwa hata wenyewe baada ya kukosekana chakuiba.. Mimi
nakuomba lifikirie jambo hili kwa upana zaidi.’’ Mke wa Mashaka alisema.
‘’ Lakini mke wangu, yule mtoto ni wamuhimu
sana, istoshe anaonekana kuwa na akili ya kuzaliwa...’’
‘’ Hata kama angekuwa na akili ya kupewa. Sina
maana ninaroho ya chuki, bali ninakuhadhari... Matoto ya mitaani siku zote huwa
ni majizi, hayabadili tabia.’’
Waliongea mengi sana na mwisho wa siku bado
hawakufikia muafaka. Ikabidi Mashaka arejee tena ndani ya akili yake na
kulitafakari jambo lile kiupana zaidi, akiwa peke yake sehemu tulivu. Aliiomba
akili yake iweze kumpatia majibu ya nini afanye?
Ikiwa nitamuacha mtoto huyu kisa ni
chokoraa, hata Mungu hatonisamehe. Mimi ni sababu ya maisha yake kuharibika,
yeye ni mwokozi wa mke wangu ingawa hajui. Hivi sasa ninafanya kazi zangu kwa
mbali naiona dira ya mafanikio kwasababu ya huyo mtoto... Hata hivyo, ni mimi
niliyesababisha aingie mtaani na kukutana na mateso yote. Iweje nimwache? Hata
ule msamaha ninaomuomba kila siku Mungu, utapokelewa kweli? Potelea mbali,
liwalo na liwe, mimi ninamchukuwa na uishinae, haijalishi. Hilo nd’o likawa
hitimisho la mawazo yake.
***
Siku hiyo nd’o ilikuwa siku ya mtoto Maduhu
kuruhusiwa maana tayari alikuwa vizuri ingawa kuna baadhi ya majiraha yalikuwa
bado hayajapona vyema. Ni siku hiyohiyo ambayo pia Mashaka alikuwa kaiandaa kwa
ajili ya kumchukuwa Maduhu na kumpeleka nyumbani kwake iliakaishinae na auage
utoto wa mtaani.
Hata dokta alipotoa ruhusa, tayari walitoka
hadi nje ya hospitali wakiwa pamoja, Mashaka na Maduhu.
‘’ Sasa, siku moja nitakuja kukulipa kwa
msaada wako, wacha nijichenge zangu.’’ Maduhu alisema, kisha akaianza safari ya
kuondoka huku akimuacha Mashaka akimshangaa.
Huyu mtoto anwazimu? Ndani ya kichwa cha
mashaka, ilisikika sauti ikisema hivyo.
‘’
Wewe...! Wewe, mtoto hebu simama bwana,’’ Alisema, lakini mtoto yule hakutii
aliendelea na safari yake. Hapo ikambidi Mashaka asikubali, akakimbia hadi
mbele ya mtoto yule kisha akasema, ‘’ Hupaswi kuondoka namna hiyo... Mimi
nataka kwenda na wewe, sihitaji uishi tena maisha ya mtaani.’’
‘’ Kwahiyo? Nini unataka?’
‘’ Nataka kukusaidia.’’
‘’ Ha... Unisaidi mimi?!’’ Kicheko cha dharau
kikamtoka Maduhu, mpaka akaenda chini huku amezishikilia mbavu zake kama kwamba
zinataka kumchomoka kisha akasema, ‘’ Sihitaji msaada wako.. Kama unaona msaada
ni mali, ama ni utajiri basi nenda kawasaidie masikini wanao ishi wakiombaomba
lakini si mimi... Tena nipishe usije ukajiletea mabalaa...’’
Ha! Ni vipi mtoto mdogo akose adabu? Hapo
mkono wa Mashaka ukashindwa kuvumilia upweke ule, akatengeneza kofi na
kumuwasha mtoto asiye na adabu wala kujua anaongea na nani.
ITAENDELEA.
0 comments:
Post a Comment