NIENDE WAPI? ‘’Dunia imenichukia’’
IMELETWA KWAKO NA SIMULIZI MIX ENTERTAINMENT
ZUBERY RAZUUR MAVUGO.
SEHEMU YA KUMI NA TATU.
ILIPOISHIA:
‘’ Jamani polisi wanakuja, tukimbieni,
tusije kamatwa.’’ Aliropoka, sauti yake ilisikika na hivi sasa raia walimsahau
mwizi wao na kuanza kukimbia. Ndani ya sekunde kadhaa eneo lile lilibaki jeupe
halina mtu isipokuwa Mashaka pekee. Hapo akawa amefanikisha adhma yake, akawaza
nini afanye kwa mtoto huyo ambaye alikuwa amepigwa sana. Hakuona mtu yeyote
aliyeonesha kumjali, hivyo akaamua kulisimamia jambo lile zima mwenyewe.
ENDELEA... Ingawa alikuwa amevalia mavazi mazuri ambayo nd’o
kwanza yalikuwa katika hali yake ya upya, lakini bado moyo wake wa huruma
uliyomuingia haukujali hilo. Ni kama aliihisi damu iliyotapakaa mwilini mwa
mtoto yule ikiwa kama maji, hapo akambebelea mtoto yule mikono miwili.
Alikatiza barabarani mbiombio, watu wakimshuhudia na kumgeuza kama sinema wala
wasiwe msaada kwake. Hakujali ni jinsi gani wanaweza kumfikiria, alichojali ni
jinsi gani anaweza kuyaokoa maisha ya mtoto yule ambaye hakuwa hata akijielewa.
Miguu yake
ilimpeleka hadi kwenye kituo cha tiba ambacho kilikuwa karibu yake, huko
akapokelewa yeye pamoja na mgonjwa wake.
‘’ Dokta naomba mumsaidie, hali yake ni mbaya
sana... Msaidieni kwanza.’’
‘’Nijukumu letu, usijali.’’
Mgonjwa
alipokelewa na kupewa kitanda, kisha matibabu yakaanza.
Walijitahidi kadri ya uwezo wao kuyaokoa
maisha ya mtoto yule. Vyeti vyao havikuwa lolote wakati huo, mavazi yao
hayakuwa chochote wala ujuaji wao wa kushauri watu haukuwa na maana,
walichofanya ni kuhakikisha wanatumia taaluma yao kuunusuru uhai wa mtoto yule
kama ambavyo walivyojifunza.
Hata hivyo jambo lile halikuwa la dakika mbili
ama tatu. Ni jambo lililochukuwa muda. Baada ya kufanya waliyoyajua wenyewe
tayari walimwacha na dripu ya maji pamoja na nyingine ya damu wakati huo hakuwa
hata amezinduka mtoto yule.
‘’ Inabidi uende nyumbani, utakuja kumtazama
kesho maana mpaka hivi sasa bado haturuhusu yeyote kumuona.’’
‘’ Lakini dokta, mimi ni ndugu yake, siwezi
kumdhuru.. Kama mnafikiri labda ikienda kumwona naweza mdhuru...’’
‘’ Hatuna maana hiyo, tunapokwambia umwache
mgonjwa apumzike, hayo ni mambo yakitaalamu zaidi, hivyo ni vyema kufuata
ushauri wa kitaalamu.’’
Hapo bwana Mashaka alielewa na kuamua
kuondoka kwenye kituo kile cha tiba. Ingawa alikuwa na wasiwasi kuhusu hali
aliyoiacha kule kazini kwake, lakini alijikuta akijiondoa wasiwasi baada ya
kukumbuka kuwa; wakati anaenda kupata chakula aliacha amefunga vizuri. Hapo
kidogo pumzi nzito ikamuijia.
Alitembea kwa miguu hadi nyumbani kwake, si
kwamba hakuwa na pesa bali damu iliyokuwa imetapakaa mwilini mwake nd’o hiyo
iliyokuwa sababu ya yeye kutembea kwa miguu. Hata alipofika nyumbani,
alimstaajabisha na kumwogopesha mkewe.
Wakati anafungua mlango kidogo mkewe
akimbie, akidhani huenda moja kati ya mizimu imeamua kulisaliti kaburi na
kuingia ndani mwake, lakini mumewe alimuhakikishia kuwa yeye ndiye. Maswali
kama umekuaje hadi ukawa hivi? Hayakumsumbua sana Mashaka maana aliyajibu kama
mwenye kutafuna bigi ji. Hata alipomaliza alielekea maliwatoni na kujisafisha
huku ngu zile mpya akizifua hukohuko. Damu iliyoganda kwenye nguo zile
haikuweza kuliheshimu povu alilolitumia, wala hazikuweza kuyatii maji
aliyoyatumia zaidi ni kama ziliidharau mikono aliyokuwa akiitumia kufikinyia.
Hapo maudhi yakampata, akamwita mkewe.
‘’ Nafua lakini hazitakati... Kwanini madoa
hayaishi?’’
‘’ Hahahaha... Unaweza kujua kufua lakini
usijue mitindo ya kuifanya nguo itakate. Kufua sio fani ya mwanaume, wacha
kesho nitakutakatishia.’’
‘’ Mh! Ama kweli kila shetani na mbuyu
wake.’’
‘’ Na kila kichwa na mwili wake.’’
Kikatoka kicheko cha istihizai. Hapo wakarejeshana
ndani ya michezo yao ya kitoto. Wakaanza kucheka na kutaniana.
Hata muda wa kulala ulipofika, kila mmoja
alilitekeleza jukumu lile kwa manjonjo yote na majigambo yote pasina hofu.
Usingizi uliwachukuwa na wasijielewe.
***
Asubuhi ya siku hiyo ilikuwa ni asubuhi na
uasubuhi wake haswa. Jua lilitumbua macho yake utadhani halijawahi kuiona
dunia, anga ilimeremeta utadhani imetolewa posa, kitendo kilico ipelekea
asubuhi hiyo kupendeza haswa.
Kama ilivyoada mke alikuwa tayari ameshaamka
tangu kitambo, huku mume naye akiwa ameamka ingawa hakuwa amemtangulia mkewe.
Harakati zote zilipomalizika, mumewe aliomba
ruhusa nakuondoka zake kuelekea majukumuni. Hata hivyo, hakupitiliza moja kwa
moja majukumuni bali alipitia hspitali kwa ajili ya kumjulia hali mgonjwa wake.
Huko hakukaa sana maana bado taarfa zilikuwa
kama za siku iliyopita, kwamba; hauwa amezinduka hivyo asingeweza kuonana naye.
Hakuhitaji kusumbuana na madktari, akaichukuwa miguu yake na moja kwa moja
akaelekea kazini kwake.
***
Kadri
alivyozidi kujilazimisha yafumbua macho yake ndivyo alivyozidi kuyahisi ni
mazito huku yakimuuma. Hiyo haikuwa sababu ya yeye kutojilazimisha kuyafumbua,
hata alipofanikiwa bado alikabiriwa na mwanga mkali ambao ni kama macho yake
hayakuwa yameupata kwa muda; mwanga ule ulimpelekea ayafumbe macho yake kwa
mara ya pili, huku akiiomba akili msaada wa kufikiri ni kwanini yupo katika
hali ile?
Hakukoma king’ang’anizi, akayafumbua macho
yake kwa mara ya pili, hapo akakutana na nuru, akaipokea nuru ile kistaarabu
iliasiyakorofishe macho yake kama alivyofanya awali. Kwa mbali akaanza kuona
kama yumo ndani ya chumba, ingawa mwanzoni ilimuwia vigumu kutambua kama yumo
ndani ya chumba, lakini alipotambua alijikuta akikumbwa na maswali ndani ya
kichwa chake.
Niko wapi hapa? Na kwanini niko hapa?
Akapata wazo la kunyanyuka, wakati anataka kunyanyuka mara akahisi kitu kama
kamba kwenye mkono, ikabidi atazame, hapo ndipo alipouona mrija wa dripu
kutazama juu akaiona dripu ya maji ikimcheka na kumwambia kimafumbo kuwa, ni
yeye aliyeyatumia maji yote yaliyokuwemo ndani ya dripu ile na hata kubakiza
machache ambayo yalikuwa yakiendelea kuingia mwilini mwake.
Nimepatwa na nini? Hata kabla hajakumbuka
chochote, akaanza kuyahisi maumivu mwili mzima. Zaidi kichwa kikaanza kumgonga,
hapo akakosa jinsi, ikabidi akirejeshe kichwa chake kitandani kwani kilikuwa
kikimgonga sana.
Katika hali ya utulivu wake, ndani ya dakika
kadhaa ndipo kumbukumbu zilianza kumrejea, akakumbuka mara ya mwisho kabla
hajawa kwenye hali ile, alipokea kipigo cha haja kutoka kwa raia.
Mbona nipo hapa? Ina maana kuna mtu gani
aliyeniokoa? Hapo akaendelea kukumbuka kwa kinazaidi kwamba, wakati akiwa chini
kipigo cha raia kikimuendelea, aliweza kusikia sauti ya mtu mmoja kwa mbali kabla
fahamu zake hazijamwondoka; sauti ile ilikuwa ni yakuwataarifu wale wapigaji
wakimbie kwani polisi walikuwa wamefika.
Akh! Ina maana kumbe hapa nilipo ninatibiwa
na ma afande? Swali hilo lilipita kichwani mwake. Akazikumbuka vyema roho za ma
afande zilivyo na ukatili, akayafikiria mateso ya mahabusu. Akawawaza mbu wenye
roho mbaya, ambao wanasifa ya kuwinda kuliko simba. Akayafikiria marungu ya
maafande.
Hakuna, haiwezekani, akili yake ikasema kisha
hapohapo bila hata kuuliza. Akajinyanyua pasina kujali maumivu aliyokuwanayo.
Akachomoa mrija wa dripu na hapo akajilazimisha kutembea hivyohivyo kwa taabu
ilimradi atoke ndani mule. Kujilazimisha kwake kuliweza kumfanya ajikute
akitonesha vidonda vibichi vilivyokuwa mwilini mwake na kumfanya apate maumivu
haswa.
Hivi sasa aliufikia mlango, alifanikisha
kuufungua na kuanza safari yakutoka ndani ya chumba kile alichokuwemo. Akiwa
njiani, huku akitegemea usaidizi wa ukuta katika kutembea, alijikuta akiishiwa
nguvu zaidi kitendo kilichompelekea aanguke chini kama mzigo na kujitonesha
zaidi, hapo akajikuta akipiga makelele kutokana na maumivu aliyoyapata kufuatia
tukio lile alilokuwa akilifanya.
ITAENDELEA.
0 comments:
Post a Comment