IMELETWA KWAKO NA SIMULIZI MIX ENTERTAINMENT
MWANDISHI: ZUBERY RAZUUR MAVUGO.
SEHEMU YA TATU.
ILIPOISHIA:
Macho ya wapita njia pamoja na wafanyabiashara waliyokuwa eneo lile walijikuta
wakikumbwa na mshangao, wapo ambao mishangao yao iliambatana na kuwaita mama zao, lakini
pia wapo waliyomuita Mungu wao. Kufumba na kufumbua mwili wa mtoto yule ulikuwa
nyang’anyang’a huku akionekana kusumbuka kama kuku aliyekatwa kichwa. Lahaulah! Gari
lililofanya kazi ile ya kumpitia lilibakiza vumbi tu wala lisijulikane lilipoelekea.
Masikini!
ENDELEA... Watu waliyokuwa pembezoni ilibidi wamsogelee na kumzunguka. Hata
walipomfikia kwa ajili ya kufanya utaratibu wa kumpeleka kwenye kituo cha tiba, tayari walikuwa
wamechelewa. Damu nyingi sana zilikuwa zimemtoka na uhai ulimuondoka palepale. Hata
walivyo hakiki, iligundulika hivyo.
Maduhu katika harakati za kumtafuta kaka yake iliaweze kumpatia habari za msiba wa baba
yao, alijikuta akipita eneo lile la tukio. ‘’Mbona watu wengi sana pale’’ Alijisemea, kisha
akajiongeza kusogea walau kutupa jicho lake. Hata alipofika aliisikia minong’ono ya raia kuhusu
jambo lililokuwa limetokea. Naam, hakujali, akaanza kujisukuma ndani ya kundi la watu
waliyojaa ili aweze kumtazama huyo aliyepata ajari. Hatimae alifika akautazama mwili wa mpata
ajari. Ulikuwa umelala chini, damu zikiwa zimeusaliti. Ingawa mwili ule ulikuwa ni mgumu
kutambulika, lakini yeye hakushindwa kumjua kaka yake kwanzia mavazi ya juu hadi yale ya
chini. Ikabidi ahakiki.
Hakuamini macho yake. Yaani mtu anaye mtafuta kumbe nayeye tayari ameshakufa? Akawa
kama amechanganyikiwa kidogo, misiba miwili kwa pamoja. Akatoka mbiombio kama mwehu
hadi nyumbani kwao kwa ajili ya kwenda kumjuza mama yake. Njia nzima alikimba huku akilia.
Hata alipofika alimkuta mama yake akiendelea kulia ingawa macho yalikuwa yamemvimba, sauti
imemkimbia.
Akamuomba mama yake amfuate mbiombio.
‘’ Twende wapi, mbona hivyo Maduhu?’’ Mama alihoji lakini mwana hakusema chochote
zaidi ya kumlazimisha mama yake waende. Wakaianza safari mbiombio, ndani wakiiacha maiti ya
baba yake.
Hawakukawia sana kufika. Tayari Maduhu alimuonesha sehemu ambayo ilikuwa ina rundo
la watu.
‘’Kuna nini kwani?’ Mama alihoji.
‘’ Sogea uone’’ Maduhu alijibu.
Mama yule akasogea eneo lile. Hata macho ya mama yule yalipofanikiwa kumtazama mtu
aliyekuwa amelala chini huku damu zikiwa zimetapakaa kwanzia mwilini mwake hadi pembezoni
mwa mwili wake, alimtambua mtoto yule. Hakuwa mwingine bali ni mwanae Shukuru; mwanae
ambaye muda si mwili alikuwa mzima akitembea na kuongea kama kawaida. Ni mwanae
huyohuyo aliyehusika kuwafanya wapate chakula muda si mrefu sana, iweje muda huo auone
mwili wake ukiwa pale chini tena katika hali ya kutisha kama ile?
Ni kweli, mwili wake mzima ulimsisimka, mapigo ya moyo yalimwenda mbio kuliko
kawaida. Hapo akajikuta anashindwa kuvumilia, msukumo wa damu ukamuijia ghafla palepale
akajikuta akianguka chini.
‘’ Mama... Mama...maaamaaa...’’ Mwanae akabaki akiita. Raia waliyokuwa pembezoni
walishuhudia tukio lile. Wakashauri apelekwe hospitali. Harakaharaka taksi ikaitwa na mama yule
akabebelewa hadi hospitali kwa ajili ya matibabu.
Hata walipomfikisha, hakuna walichofanikisha, tayari mama yule alikuwa ameshaiaga
dunia. Hakukuwa na kingine kilichosababisha isipokuwa msukumo wa damu uliyoletwa na
mawazo mengi yaliyopitiliza. Masikini! Mtoto mdogo Maduhu akashindwa nini afanye.
Alijiona asiyependwa na mwenyezi Mungu. Misiba mitatu yote imemtokea yeye tena kwa
siku moja? Akashindwa hata nini afanye, muda wote alikuwa wa kulia tu.
Hata hivyo, wananchi wenye mioyo ya upendo na wenye utambuzi wa neno matatizo,
waliweza kushirikiana na maaskari kuhakikisha miili yote mitatu inastirika vyema. Hata
walipomaliza, hakukuwa na yeyote aliyeonesha kumjali tena mtoto yule. Kila mmoja alionekana
kuwa na matatizo kama yeye, hivyo hakuna msaada aliyoupata zaidi ya kupatiwa pole nyingi tu.
Lakini pia hawakumwacha hivyohivyo mtoto yule, walimchangia vijisenti kwa ajili ya kumsaidia
kujikimu. Walipomaliza walimwacha peke yake, naye hakuwa na pakwenda zaidi ya palepale
alipokuwa akiishi na wazazi wake. Alibaki nyumbani kwao huku akiwa amejikunyata, watu
wachache wakipita nje na kumpatia pole. Muda wote wa upweke wake mawazo mengi sana
yalimpata hofu kuu lilimwelemea kila sekunde.
Alikaa nje ya nyumba yao mpaka usiku ulipoiingia, hatimae aliamua kuingia nyumbani kwao
iliaweze angalau kupumzika. Alipofika, alikikurubia kitanda kidogo sana kilichoweka godoro
lililoishaisha. Mwili wake ukawa juu ya godoro hilo na kuulazimisha usingizi ingawa alikuwa na
hofu muda wote.
Usingizi wa visa ulimpata; usingizi uliyoambatana na njozi za kutisha hswahaswa. Ati,
anaota jitu lisilo na jina lakini lenye sura mbaya likimfuata na kumuita huku likiiomba roho yake,
mdomoni mwake likitoa kicheko cha kejeli. alijitahidi sana kukimbia lakini kila alipojaribu
kukimbia hata miguu haikuweza kukimbia, ni kama alikuwa na sumaku miguuni. Jitu lile lenye
kucheka kwa kejeli, lilimsogelea na kumfikia, likisema, ‘’ Lazma uwafuate ndugu zako.’’ Huku
sauti yake ikiambatana na mwangwi. Mh! Lilichomoa kisu ambacho hata hakikujulikana
lilipokuwa limekificha. Hapo sasa likataka kumchoma. Ni kama hakuweza kuivumilia ndoto ile ya
kuogofya, ni kama hakuweza kukubali lile jitu liyatoe maisha yake. Akakurupuka kutoka
usingizini hapohapo huku akihema utadhani mtu aliyekimbizwa.
Uoga ukamjaa, hata kukaa ndani ya nyumba yao akashindwa, mawazo yake yakawa yanamtuma
wazazi wake pamoja na kaka yake wamo ndani mule, wakimwita na kumtaka. Pengine ni utoto
ama hofu ya kuondokewa, hata hivyo hakuweza kuvumilia kuitwa, ikabidi atoke nje. Tayari usiku
ulikuwa ni wa saa saba. Hata huko nje, hali ya woga iliendelea kumsumbua. Ingawa kuna wakati
alijua ni mawazo tu yanayomsumbua lakini hakuweza kuyavumilia pia, alitamani angalau awe
katikati ya kundi la watu iliawe na ujasiri dhidi ya jambo lile lililokuwa likimsumbua akili.
Usiku ule akaanza kutembea mtaani wala asijue wapi anaelekea, ndani ya moyo wake
alimuomba mwenyezi Mungu walau giza lile liondoke na mchana uingie iliamani imrejee.
Akiwa katika pitapita zake yeye pamoja na woga wake mara kwa bali alisikia sauti ya miziki.
Bila shaka huko miziki ilipokuwa ikitokea kulikuwa na jambo fulani lililokuwa likiendelea.
Akaongeza hatua za miguu yake kuelekea eneo ambapo sauti zile alikuwa akizisikia. Muda kidogo
alifika.
Kwa mara ya kwanza akaipata furaha ndogo ndani ya moyo wake, na hiyo ni baada ya kugundua
kumbe sehemu ile kulikuwa na watu waliyokuwa wakiserebuka huku wengine waliyowazunguka
wakiwatazama kwa furaha. Akajichanyanya na muda kidogo akagundua kumbe sehemu ile
kulikuwa na mkesha wa harusi. Akamshukuru sana menyezi Mungu na hapo akajikalisha karibu
na spika zilizokuwa zikitoa mkito wa nguvu. Alifanya hivyo ikiwa ni njia yake ya kuikimbiza
hofu aliyokuwanayo. Akiuambia moyo wake pamoja na nafsi, ‘’ Ondoeni shaka, msiogope hivi
sasa tupo watu wengi’’ ingawa mbu walimfanya chakula, lakini hilo hakulijali hata kidogo,
aliuchukuwa mkono wake na kujiwasha makofi sehemu mbalimbali ambazo mbu walimuuma.
Dakika kadhaa mbele hakuwa tena akijielewa. Alikuwa katika usingizi mzito. Usingizi ule
haukuwa na mauzauza hata kidogo, ingawa alilala mbu zikimuuma lakini alikuwa na uhuru wa
nafsi yake.
‘’ Wewe mjinga. Amka, mpuuzi wewe.’’ Sauti moja ilisikika na hata kumfanya mtoto yule
afumbue macho yake kutazama. Mh! aligundua kuwa, tayari asubuhi ilikuwa imeingia, ingawa
macho yake yalikuwa bado usingizini. Katika mtazamo wake, ni kama kulikuwa na watu kadhaa
waliyomzunguka eneo lile, lakini hakujali kutokana na usingizi aliyokuwanao ambao alikuwa
akiulazimisha umtoke.
‘’ Unadhani ni nani? Nd’o huyuhuyu choko aliyetuibia... Kwani nani mwingine.’’ Sauti
nyingine ilisikika ikikoroma. Mara ngumi moja ya kichwa ikatua mwilini mwa Maduhu, maumivu
yakaandamana na kilio cha nguvu kutoka kwake. Hajakaa sawa, mara akapokea kofi la uso,
kutoka katika mkono uliyoshiba kimazoezi. Akiwa katika sintofahau, mara akahisi kama harufu
fulani ya damu. Pakepale pua zake mbili zikaanza kutoa damu. Hakupata muda wa kuuliza
ama kujiuliza ni kipi alichokosea hadi kipigo kimuangukie?
ITAENDELEA....
USIKOSE MWENDELEZO WA HADITHI HII NZURI KUJUA NI HAPA HAPA KUJUA NI MAISHA GANI HUYU MTOTO ALIYAPITIA NA NINI ILIKUA HATIMA YA MAISHA YAKE IKIWA NDO KABAKI MWENYEWE NA NI ANA UMRI WA MIAKA SABA TU..
Home
»
»Unlabelled
» 03 NIENDE WAPI? ‘’ Dunia imenichukia’’
Tuesday, June 20, 2017
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment